Mwanamapinduzi
na Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara alisema kuwa ili
kuleta mabadiliko ya kimapinduzi ni lazima kuwa na hali fulani ya
uendawazimu. Ila tusiufikirie uendawazimu huu wa kuokota makopo bali ule
ukichaa mzuri wa kuamini katika mambo au misingi fulani na kuisimamia
kwa dhati pamoja na changamoto nyingi.
Zitto akiwashukuru wananchi wa Kigoma |
Kwa
kuamini kwa dhati katika mabadiliko haya na kutaka kuboresha maisha ya
wanakigoma, mwaka 2005 nilikuja kwenu kuwaomba ridhaa ya kuwatumikia
kama mwakilishi wenu Dodoma. Nikiwa na umri wa miaka 29 tu. Labda
ulikuwa ni msukumo wa matumaini yangu makubwa yanayoambatana na ujana
yaliyowashawishi, kwani mliniamini na kunipa kazi hiyo ya heshima kubwa
ya kuwawakilisha.
Mwaka
2010 mliniamini tena, naamini kutokana na utekelezaji wangu mzuri wa
kazi na mafanikio tuliyoyaweza kuyapata katika jimbo letu. Hivyo kwa
miaka kumi tumekuwa bega kwa bega katika safari hii ya pamoja ya kujenga
na kuiendeleza jimbo letu, na leo nimekuja kuwashukuru kwa fursa
mliyonipa kwani safari yetu inafikia mwisho. Fursa mliyonipa ni ya
kipekee kwani ilikuwa fursa si tu ya kuwatumikia ninyi bali kulitumikia
Taifa langu.
Katika
miaka kumi hii kuna mambo makubwa tumeyafanya pamoja na kufanikiwa; na
kuna mambo ambayo hatukuweza kuyafanya. Kwa yale ambayo hatukuweza
kuyafanya naomba radhi. Kwa yale ambayo tumeweza kuyafanya naomba
kuwapongeza sana kwa kufanikisha. Kwani kama Mwalimu Nyerere
alivyotuambia kuhusu Uhuru na Maendeleo: “Uongozi
ni kuongea na kujadili na wananchi, kuwaelewesha na kuwashawishi.
Uongozi ni kufanya kazi pamoja na wananchi na kuonyesha kwa vitendo
mnachotaka kufikia. Uongozi ni kuwa mmoja wa wananchi na kutambua kuwa
mko sawa…. Wananchi hawawezi kuendelezwa bali wanajiendeleza.” Na ndivyo tulivyofanya kwa miaka kumi, na kwa ushirikiano wenu tumeweza kufanikisha miradi mikubwa katika Jimbo letu.
Mwaka
2005 tulikuwa hatuna barabara ya lami hata moja. Leo hii, ninapoongea
nanyi tuna barabara za lami zenye zaidi ya kilomita 100 kuunganisha
Jimbo letu na majimbo mengine kwa pande zote za nchi kavu. Vilevile tuna
mradi mkubwa wa kuunganisha vijiji vya ufukweni mwa Ziwa Tanganyika kwa
barabara. Kiujumla
kwa mkoa wa Kigoma tumefanikiwa kumaliza daraja la Malagarasi na hivyo
kuunganisha mkoa wetu na mkoa wa Tabora kwa lami jambo ambalo lilikuwa
kilio chetu cha muda mrefu sana tokea enzi na enzi. Muhimu
zaidi ni kuwa barabara hizi zinatumika na wananchi, wafanyabiashara na
wakulima ili kuwasiliana, kufanya biashara na kupanua masoko.
Tumefanikiwa
kuongeza huduma ya Nishati ya Umeme kwa kuunganisha vijiji zaidi ya 16
hivi sasa. Changamoto kubwa iliyobakia mkoani kwetu ni uzalishaji mdogo
wa umeme na wenye gharama kubwa sana. Suluhisho la kudumu ni kufanikisha
mradi wa Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha 44MW ambao utakuwa nafuu
na kuwezesha pia kusambaza umeme mikoa jirani ya Katavi na Tabora, na
hata kuuza nchi jirani ya Burundi. Viongozi wa kisiasa wa mkoa wa Kigoma
watakaoingia kwenye uongozi baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka
2015 hawana budi kuweka kipaumbele kikubwa kwa mradi huu. Bila ya umeme
wa uhakika na nafuu hatuwezi kupiga hatua ya kuongeza thamani ya mazao
yetu kwa kujenga viwanda vya usindikaji na kuongeza ajira ya vijana
wetu.
Tumefanikiwa
kuanza miradi ya Bandari na Soko kubwa kijiji cha Kagunga. Lengo likiwa
ni kukuza biashara ya bidhaa kati yetu na nchi ya Burundi. Kigoma ni
mji wa biashara kiasili na biashara ilichukua nafasi kubwa ya uchumi wa
mkoa huu kwa miaka mingi sana. Kuimarishwa kwa miundombinu ya Biashara
ni sehemu ya miradi ya kimkakati katika kuuweka mkoa kuchukua nafasi
yake ya kiuchumi katika nchi yetu. Katika muktadha huo ndio maana
tunaendelea na miradi ya Bandari Kibirizi na Bandari ya Nchi Kavu
Katosho. Ndio maana tunaendelea na mradi wa Kituo cha Usafirishaji
Mwandiga ( Mwandiga International Transportation Terminal ) na eneo
maalumu la kiuchumi Ujiji. Haya yote tuliyaanzisha kwa pamoja nanyi ili
kuhakikisha kuwa uchumi wetu unazalisha ajira kwa watu.
Tumefanikiwa
kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekondari kwa kuwa na shule katika
kata na baadhi ya kata tumejenga shule kila kijiji. Hata hivyo, tuna
changamoto kubwa sana ya ubora wa elimu katika mkoa wetu. Katika jimbo
la Kigoma Kaskazini zaidi ya 90% ya watahiniwa wa Kidato cha Nne
wanapata madaraja ya mawili ya chini, wakati ule daraja la nne na daraja
la sifuri. Tumeanzisha mradi wa majaribio ya kutoa motisha kwa Walimu
ili kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha elimu inaboreshwa. Shirika la
Twaweza linaendesha mradi mkubwa wa motisha kwa walimu na baada ya mwaka
huu tutakuwa tumejifunza njia bora za kuongeza ubora wa elimu kwa
watoto wetu. Bila Elimu bora miradi yote niliyoeleza hapo awali haina
maana yeyote. Serikali imetoa Sera mpya ya Elimu, ni wajibu wetu kuona
namna ya kuitekeleza katika ngazi yetu ili kupata mafanikio. Hata hivyo,
uongozi wa kisiasa utakaoingia baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu hauna
budi kujielekeza vya kutosha katika elimu ya ufundi ili kujenga stadi za
kazi kwa vijana waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Tumefanikiwa
kupanua huduma ya Afya kwa kuboresha Zahanati zetu chache zilizokuwepo
na kujenga zahanati kadhaa mpya na miradi ya vituo vya afya vya Mahembe
na Nyarubanda. Hata hivyo nasisitiza sana umuhimu wa kinga kuliko tiba
kwani gharama za afya zimekuwa kubwa sana. Ndiyo maana tulipojadili hili
suala, ilionekana kuwa suluhisho linatakiwa lipatikane kwa kufanya kile
ambacho hatujawahi kufanya ili kuleta maendeleo ya kweli. Na mniruhusu
hapa kunukuu wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipotuasi kuwa
“Maendeleo ni maendeleo ya watu. Barabara, Majengo, kuongezeka kwa
uzalishaji wa mazao na masuala mengi kama haya si maendeleo, bali ni
vitendea kazi tu vya maendeleo” Ndiyo maana kulikuwa na umuhimu wa
kutafuta njia mpya na mbadala kuboresha maisha ya mwananchi, hususan kwa
upande wa afya. Uthibitisho wa ubunifu wetu ni kuwa katika kipindi hiki
cha miaka 10 tumefanikiwa kuanzisha hifadhi ya jamii kwa wakulima.
Tulianza
na Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wa RUMAKU ambapo wananchi walijiunga
na NSSF na hivyo kupata mikopo ya muda mfupi, huduma za afya bure na
kujiwekea akiba kwa ajili ya mafao ya muda mrefu. Mafanikio makubwa
yaliyopatikana yamewezesha wazo hili kusambaa nchi nzima na hivi sasa
wakulima wa Korosho, Chai, Pamba, Tumbaku wanafuata nyayo za Wakulima wa
Ushirika wa RUMAKU. Hapa Kigoma wazo hili sasa linatekelezwa kwa wavuvi
wa mwambao mwa Ziwa Tanganyika. Ndoto yetu ni wananchi zaidi ya
theluthi moja kwenye nguvu kazi wawe na Hifadhi ya Jamii. Natoa
wito kwa wananchi wengine wenye uwezo wa kuchangia hifadhi ya jamii
wajiunge na vikundi vya ushirika na kuchangia ili kufaidika na mafao ya
muda mrefu kama pensheni lakini pia yale ya muda mfupi kama bima ya
afya, mikopo kupitia SACCOS na mengine yatakayoanzishwa kama bima ya
mazao.
Tumefanikiwa
kujenga heshima ya watu wa Kigoma hapa nchini. Hivi sasa watu wa Kigoma
tunatembea kifua mbele bila woga kuliko hapo awali. Kujiamini na
kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano ni wajibu wetu
kama raia. Changamoto za kujiona raia wa daraja la pili zimeondoka na
zinaendelea kutokomezwa. Juhudi zetu ni silaha kubwa katika kuhakikisha
tunakuwa sehemu ya Jamhuri yetu katika kila Nyanja za maisha yetu.
Nafurahi kupata fursa ya kushiriki nanyi katika kujenga heshima hiyo ya
Mkoa wetu. Nitaendelea kushiriki katika kudumisha heshima hiyo.
Nimejifunza
mengi sana katika safari hii ya utumishi kwenu. Kama nilivyosema hapo
awali, mliamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa ya nchi yetu kwa
kunipa jukumu hili nikiwa kijana mdogo. Naamini kuwa ule ukichaa wangu
mzuri wa kusimamia misingi ya kuleta maendeleo kwa wananchi wangu na
kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia nimezipigania. Na katika safari
hii nimejenga marafiki wengi sana na pengine hata maadui ingawa hao ni
wachache. Lakini haijalishi kwani mi binafsi sina uhasama na binadamu
mwenzangu.
Katika
utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inaendeshwa.
Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na
mengine ni makosa. Mliniruhusu kufanya makosa na kuyarekebisha makosa
hayo kwa hiyo kukomaa zaidi. Shukrani za dhati ziwaendee wazee wangu
ambao mliniongoza mpaka hapa tulipofika na kunishauri hata kunionya pale
palipohitajika. Kwa ujumla nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi
yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndio maana hamkunisikia tu
kutetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi yetu na
makundi mbalimbali ya kijamii kama Wakulima, Wafanyakazi, Wasanii,
Wavuvi, Wana michezo na wana habari.
Katika
safari hii ya miaka 10 kuna watu nimewafurahisha na kuna watu
nimewaudhi. Kwa wale niliowaudhi ninaomba radhi. Kwa wale
niliowafurahisha ninaomba wasiache kuniongoza na kunishauri kila wakati.
Haikuwa safari rahisi na sikutegemea iwe rahisi. Kiuhalisia
ilikuwa safari ngumu yenye mafunzo makubwa kwangu. Ilikuwa ni safari
yangu kama kiongozi na pia safari yangu binafsi ya kupevuka kifikra na
kupata mafunzo kuhusu maisha. Ukifika ulikokuwa unakwenda katika safari,
unaweza kutathmini mengi kuhusu safari hiyo, lakini mwisho wa siku
unatakiwa ujue kama safari hii ilikuwa njema ama la. Ninajivunia safari hii na ninasema kwa dhati kabisa ilikuwa ni safari njema.
Ni
wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza Jimbo letu. Kushika
kijiti pale ninapoishia. Kurekebisha pale nilipokosea. Kuimarisha pale
nilipofikia.
Sitakuwa
mbunge wenu baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba lakini nitaendelea
kutetea maslahi ya Mkoa wa Kigoma na Taifa letu kwa njia nyingine.
Sitaacha
ule uendawazimu mzuri aliyoizungumzia Thomas Sankara unaoleta maendeleo
ya kimapinduzi. Na misingi ni ileile na maadui ni walewale ambao
mwasisi wetu Mwalimu Nyerere aliyokuwa anasema tupambane nao, yaani
umaskini, ujinga, maradhi na sasa tumeongeza ufisadi. Kizazi chetu kina
jukumu la kipekee kuendeleza mapambano haya na nitaendelea kuhakikisha
tunafanya mapinduzi na kuwa na Taifa lenye misingi madhubuti ya
uwajibikaji ili kuondoa kila aina ya ufisadi na kutumia rasilimali za
nchi kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.
Asanteni sana Kigoma Kaskazini!
Post a Comment