Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar
es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema, amemsamehe Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye hivi karibuni
alimtolea maneno makali kutokana na kutofautiana naye juu ya msimamo wa
viongozi wa Kikristo kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
“Natumia nafasi hii kueleza juu ya maneno ambayo yalitolewa na mchungaji fulani, sikumbuki anaitwa nani… nasema nimemsamehe kutoka ndani ya moyo wangu wote anaweza kuwa na sababu zake ila nimemsamehe kabisa” Kardinal Pengo |
Kardinali Pengo alitoa msamaha huo mbele ya
waumini katika Kanisa la St Joseph, Dar es Salaam jana, siku mbili baada
ya Askofu Gwajima kuhojiwa na Polisi kwa madai ya kumkashifu kiongozi
huyo, mbele ya hadhara.
Askofu Gwajima anadaiwa kutoa kauli za kumkashifu
kiongozi huyo kwamba amewasaliti wa viongozi wenzake wa Kikristo kwa
kuwataka waumini wa dini hiyo kuamua wenyewe suala la Katiba
Inayopendekezwa kinyume na msimamo wa waraka wa kupinga katiba hiyo
uliotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (CCT).
Baada ya kutolewa kwa waraka huo ulioagiza waumini
kuipigia kura ya hapana katiba hiyo, Askofu Pengo alinukuliwa akisema
viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuzuia wananchi kuikubali Katiba hiyo
huku akisisitiza waachiwe uhuru wao wa kuamua.
Akizungumza jana wakati wa ibada ya Jumapili ya
Matawi, inayoadhimishwa wiki moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, Kardinali
Pengo, bila ya kumtaja jina alisema: “Natumia nafasi hii kueleza juu ya
maneno ambayo yalitolewa na mchungaji fulani, sikumbuki anaitwa nani…
nasema nimemsamehe kutoka ndani ya moyo wangu wote, anaweza kuwa na
sababu zake ila nimemsamehe kabisa.
“Sina ghadhabu wala chuki ila kinyume chake,
naomba tumwombee yeye na watu wote waliokuwa wamehusika pengine nyuma
yake ili Mungu aweze kutulinda na kutudumisha katika hali ya amani ya
Taifa letu.”
Alisema hatua ya Polisi kumkamata ni sehemu ya kutekeleza utaratibu wa jeshi hilo tu, lakini yeye kwa nafsi yake ameshamsamehe.
Atolewa ICU, wafuasi wakamatwa
Katika hatua nyingine, Askofu Gwajima ametolewa
kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na
kuhamishwa katika wodi ya kawaida baada ya afya yake kuendelea vizuri.
Askofu huyo alikuwa ICU kwenye Hospitali ya TMJ,
Mikocheni, alikofikishwa usiku wa Ijumaa baada ya hali yake kubadilika
ghafla alipokuwa akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam.
Askofu huyo alijisalimisha kituoni hapo akiitikia
wito wa polisi uliomtaka kufanya hivyo kutokana na tuhuma za kutoa lugha
chafu dhidi ya Kardinali Pengo.
Akizungumza jana, mke wa Askofu huyo, Grace
Gwajima alisema baada ya madaktari kumuona anaendelea vizuri, wameamua
kumtoa ICU na kumpeleka kwenye wodi ya kawaida.
“Tunamshukuru Mungu sasa hivi anaendelea vizuri tofauti na
alivyokuwa jana (juzi) alikuwa hawezi kula chakula na kuongea lakini
sasa hivi anaongea na anakula chakula,” alisema na kuongeza:
“Tunashangazwa ni nini kimetokea Polisi wakati
akihojiwa. Alitoka nyumbani akiwa mzima na ametolewa polisi akiwa
amebebwa hajitambui.”
Mke wa Askofu huyo alisema wakiwa hospitalini hapo
usiku wa kuamkia leo, walikuja askari polisi na kuwakamata baadhi ya
viongozi na walinzi wa kanisa hilo na kuchukua magari yao.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema inawashikilia na
kuwahoji watu 15 ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama pamoja na
kujaribu kumtorosha Askofu Gwajima.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana,
Kamanda Kova alisema jana saa 9.30 usiku watu hao 15, katika hali isiyo
ya kawaida walifika hospitalini hapo wakidai kwamba walikuwa wanataka
kwenda kumuona mgonjwa huyo.
“Askari ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia
shaka hivyo waliwakatalia kuingia. Kundi hilo la watu 15 lilijaribu
kutumia nguvu kuingia katika chumba alicholazwa Askofu Gwajima lakini
walikamatwa na kikosi maalumu cha Polisi ambacho kabla ya tukio hilo
kilikuwa kinafuatilia mwenendo wa kundi hilo.”
Alisema baada ya kukamatwa, watuhumiwa hao
walipekuliwa hapohapo TMJ na kukutwa na begi ambalo lilikuwa na vitu
mbalimbali mojawapo vikiwa ni bastola aina ya Berreta ikiwa na risasi
tatu, risasi 17 za bunduki aina ya Shortgun, vitabu viwili vya hundi na
hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Josephat Mathias.
Alisema baada ya upekuzi kukamilika, watuhumiwa
walifikishwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa mahojiano zaidi ikiwa ni
pamoja na kupata uhalali wa wao kumiliki silaha hizo na risasi.
“Upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni
ya kubaini sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote
zilizotumika kutaka kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.”
Chanzo cha habari na gazeti la kila siku la Mwananchi
Post a Comment