Rais
wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame amesema kuwa hatua ya
Mwenyekiti wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Rais
Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Nchi Zilizoungana
Kutekeleza Miradi ya Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern
Corridor Projects ni hatua muhimu katika kufungua utekelezaji wa miradi
ya miundomninu katika kanda nyingine za EAC.
Aidha,
Rais Kagame amemshukuru Rais Kikwete kwa uamuzi wake kuhudhuria Mkutano
huo uliofanyika leo, Jumamosi, Machi 7, 2015, katika Ukumbi wa Mikutano
wa Hoteli ya Serena mjini Kigali, Rwanda.
Rais Kikwete amefanya ziara hiyo ya siku moja kuhudhuria Mkutano huo kwa mwaliko wa Rais Kagame.
Naye
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba
Rais Kikwete ameweza kuhudhuria Mkutano wa leo, kwa sababu sasa njia
imefunguka kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa
Central Corridor unaokatisha katikati ya Tanzania.
Marais
Kagame na Kenyatta walikuwa wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi
za Mkutano huo uliofanyika kwa kiasi cha saa mbili unusu mara baada ya
Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es Salaam kiasi cha saa sita
mchana.
Akifungua
Mkutano huo, Rais Kagame alisema: “Nawashukuru waheshimiwa marais wote
kwa kuja. Lakini hasa hasa, namshukuru sana mwenyekiti wetu wa EAC Rais
Kikwete kwa kupata muda wa kuja kujiunga nasi katika mkutano huu.”
Aliongeza Rais Kagame huku makofi yakiendelea kumkaribisha na
kumshangilia Rais Kikwete:
“Kuwepo
kwake hapa leo, kunaongeza matumaini kuwa miradi mbali mbali na mingi
zaidi katika kanda mbali mbali za nchi zetu wanachama wa EAC, sasa
inaweza kutekelezwa kwa haraka zaidi. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais.”
Mbali na Marais Kikwete, Kagame na Kenyatta, Mkutano wa leo pia
umehudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Salva Kiir wa Sudan
Kusini, Makamu wa Rais wa Pili wa Burundi na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Ethiopia.
Nchi
za Kenya, Uganda,Rwanda na Sudan Kusini ndizo wanachama wa Northern
Corridor na kwenye mkutano wa leo, Burundi pia imetangaza kuwa imeamua
kuwa mshiriki kamili wa mikutano ya Ukanda huo badala ya kuwa
msikilizaji kwa muda mrefu.
Akizungumza
katika Mkutano huo, Rais Kenyatta amesema: “Tunafurahi sana kwamba
Mwenyekiti wetu wa EAC yuko nasi leo kwa sababu uwepo wake utaongeza
msukumo wa kutuwezesha kuanza utekelezaji wa miradi mingine hasa katika
Ukanda wa Kati. Tanzania ina mengi kuchangia katika jambo hilo. Kwa
mfano, umeme mwingi ambao utaanza kuzalishwa na Tanzania mwaka huu,
unahitajika kwa nchi zote za EAC na Northern Corridor.”
Rais
Kikwete ambaye alikuwa msikilizaji tu kwa sababu Tanzania inaendelea
kuwa mwanachama wa EAC bila kuwa mshirika wa Northern Corridor
amezugumza kwa ufupi tu akisema kuwa kwa sababu yeye ni mwalikwa na
msikilizaji asingeweza kusema mengi.
Amewaambia
viongozi wenzake: “Nakushukuru Rais Kagame kwa kunialika. Kama
unavyojua, mimi ni msikilizaji tu na hivyo siwezi kusema sana. Lakini
napenda kuwapongezeni nyote kwa kazi mnayoifanya. Sote tunajua kuwa
hakuna utengamano bila kuendeleza miundombinu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kinachoendelea kule Northern Corridor
kitasaidia sana katika mawazo na utekelezaji wa kazi ambayo tunajiandaa
kuianza kwenye Ukanda wa Kati. Nawatakieni mafanikio zaidi na kasi ya
Mwenyeji Mungu katika utekelezaji wa miradi yenu.”
Chini
ya Northern Corridor nchi hizo zimebuni miradi 14, ambayo baadhi yao
imeanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha visa moja ya kusafiria
ya watalii.
Nchi
hizo ziliunda kundi hilo mwaka mmoja na miezi tisa iliyopita na wakuu wa
nchi wanachama hukutana kila baada ya miezi miwili kwa mashauriano na
maamuzi.
Rais kikwete amerejea nyumbani usiku wa leo baada ya kumalizika kwa
Mkutano huo.
Mwenyekiti
wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Jakaya Mrisho
Kikwete akipokea kwa furaha sahada la maua baada ya kuwasili Kigali,
Rwanda, tayari kwa mkutano na viongozi wenzake wa Jumiya hiyo katika mkutano wa tisa wa wakuu wa nchi hizo kujadili miradi iliyoko katika Ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor Integration Projects) katika Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Mkutano wa leo pia umehudhuriwa
na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda. Mbali na nchi hizo
na mbali na Tanzania, nchi za Burundi na Sudan Kusini pia zilialikwa kuhudhuria mkutano huo. Mkutano
huo ni ulijadili hatua za utekelezaji wa miradi mbali mbali
iliyokubaliwa kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa nane
wa namna hiyo uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana, 2014.
Mwenyekiti
wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Jakaya Mrisho
Kikwete akiongea na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wa Rwanda kabla ya
kuanza kwa mkutano wa tisa wa wakuu wa nchi hizo kujadili miradi iliyoko katika Ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor Integration Projects) katika Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na viongozi wenzake wa Jumiya hiyo katika mkutano wa tisa wa wakuu wa nchi hizo kujadili miradi iliyoko katika Ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor Integration Projects) katika Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe
Paul Makonda baada ya kuwasili uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere jijini Dar es salaam jioni leo Machi 7, 2015 akitokea Kigali
Rwanda, alikohudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Kati ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe Sophia Mjema. PICHA NA
IKULU
Post a Comment