Nimepokea
kwa masikitiko taarifa kuwa ndugu yangu Zitto Kabwe amefukuzwa kwenye
chama cha Chadema. Ni habari ya kusikitisha unapotafakari demokrasia
tunayojitahidi kuijenga.
Zitto
amekuwa mwanachama wa Chadema tangu akiwa kijana mdogo. Mwenyekiti wa
chama hicho , Freeman Mbowe, amenukuliwa mara kadhaa akikumbushia jinsi
alivyoshirikiana na Zitto kuhamasisha vijana wengine waliokuwa vyuoni
kujiunga na Chadema.
Kwenye siasa za vyama kuna kutofautiana kifikra na kimitazamo. Na mara
nyingine migongano huwa inahusu kugombania nafasi za uongozi. Haya ni
mambo ya kawaida kwa chama cha siasa. Hayapaswi kuwa sababu za viongozi
wa vyama kuwafukuza wanachama.
Kwenye
siasa tofauti humalizwa kwa hoja, kwenye vikao. Na anayekiuka taratibu
za chama kumfukuza kwenye chama ni adhabu kubwa na kali kama ya kifo.
Maana, anayejiunga na chama hufanya hivyo kwa mapenzi. Anapokosea
anaweza kuonywa au kuadhibiwa, lakini, kufukuzwa kwa misingi ya
kutofautiana kifikra na kimitazano si hulka njema.
Zitto
Kabwe ni mwanasiasa kijana na mahiri. Chadema ilipaswa imvumilie na
ishindane nae kwa hoja, lakini, si kumtupa nje kwa staili
tuliyoishuhudia.
Chadema, kama chama cha
siasa, isijiandalie mazingira ya wanachama wake kuwa na hofu ya
kufukuzwa pindi wanapotofautiana na viongozi wa juu. Itapoteza kisiasa.
Na
hili la Zitto Kabwe linatukumbusha kile ambacho binafsi nimeandika mara
kadhaa, juu ya udhaifu kwenye Katiba yetu. Kwamba Mbunge aliyechaguliwa
na Wananchi anaishi kwa hofu ya rungu la chama.
Kwamba
leo Wananchi wa Kigoma Kaskazini wanampoteza Mbunge wao waliyemchagua
kwa maamuzi ya Chama anachotoka Mbunge wao. Haya ni mapungufu makubwa.
Wananchi hapaswi kuadhibiwa kwa maamuzi ya vyama.
Nachukua
fursa hii kumtakia kila la heri ndugu yangu Zitto Kabwe, nikimuasa
asikate tamaa, akipata fursa nyingine, aendelee na siasa na hususan
uongozi wa uwakilishi wa wananchi. Aendelee kuwa sauti ya wasio na
sauti, popote pale.
Maggid Mjengwa,
Dar Es Salaam.
Post a Comment