Shirika la AMREF Tanzania linaikubusha jamii kuhusu chakula cha hisani cha kuchangisha fedha kwa ajili ya kusomesha wakunga kupitia kampeni ya “Simama kwa ajili ya mwanamke wa Tanzania”.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la AMREF Tanzania Dkt. Festus Ilako alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

Dkt. Ilako amesema kuwa chakula hicho cha hisani kitakuwa siku ya Ijumaa Oktoba 11, mwaka huu, ambapo Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ambaye ataongoza uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kampeni hiyo. 

“Kampeni hii itasaidia uboreshwaji wa afya ya mama na mtoto, na pia kuongeza idadi ya wakunga wenye utaalam nchini. Nia ya AMREF ni kusaidia Serikali ili kufikia malengo iliyojiwekea ya millennia (MG), hususani mpango wa tano unaozungumzia uboreshwaji wa afya ya mama na mtoto”, amesema Dkt. Ilako.

Dkt. Ilako amesema kuwa fedha zilizopatikana mwaka uliopita zimeweza kusomesha wakunga 10 mkoani Tanga wilaya ya Kilindi na zaidi ya wanafunzi 70 kutoka mikoa ya Simiyu na Mtwara wanatarjiwa kwenda kwenye mafunzo ifikapo Novemba mwaka huu. 

“Tunawaomba watanzania wote, wake kwa waume kuungana na kusaidia uchangishaji wa fedha katika mpango utaendelea mpaka 2015,” alisisitiza Dkt. Ilako.

Dkt. Ilako amesema kuwa michango ya kusaidia kampeni inaweza kupokelewa kupitia M- Pesa simu namba +255 752167286, Tigo Pesa +255716032441 na benki ya NBC Makao Makuu akaunti namba 011103000458.

Naye Mkurgenzi Mtendaji wa kampuni ya Montage Teddy Mapunda aliwashukuru washirika wanaoendelea kuunga mkono kameni ya “Simama kwa ajili ya mwanamke wa Tanzania”.
Mapunda aliwataja washirika hao kuw ni ITV/Radio One, Clouds Media Group, Banki Kuu Tanzania (BOT), Serena hoteli, benki ya NBC, Toyota Tanzania, Tanzania One, DSTV, PPF, TACAIDS, WHO, MSD, Kampuni ya Guardian, Benki ya Biashara ya Afrika, Songas, Kampuni ya bia ya Serengeti na Coca cola.

Kampeni ya “Simama kwa ajili ya Mwanamke wa Kiafrika” ilianzishwa kwa ajili ya kusaidia kuboresha afya ya mama na mtoto ambapo vitaboreshwa viwango vya wakunga 2800 na wataalam1000 kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo njia za mitandao ifikapo mwaka 2015.
Mwisho
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.