NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ambaye alikwishatangaza kutogombea tena ubunge katika Jimbo lake la Kigoma Kaskazini kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, amesema anatafakari upya uamuzi wake wa kuachana na siasa baada ya kushuhudia hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi mkoani Tabora.

Alisema kutokana na hali duni ya maisha ya wananchi aliyoishuhudia katika maeneo mbalimbali kwenye majimbo ya Sikonge na Igalula, atahakikisha kwa kushirikiana na viongozi wenzake ndani ya CHADEMA wanakifuta Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Kanda ya Magharibi.

Zitto alitoa kauli hiyo juzi katika mikutano ya hadhara, katika majimbo ya Sikonge na Igalula, ukiwa ni mwendelezo wa ziara 

yake ya ujenzi wa chama katika kanda hiyo.

Maeneo aliyoyatembelea na kukuta hali ya wananchi ikiwa hairidhishi hususan katika kupata huduma ya maji ni kata za Ipole, Kitunda na Sikonge, zilizo jimboni Sikonge na kata za Miswaki, Kigwa na Loya zilizoko Igalula, wilayani Uyui.

Alisema kuwa licha ya wabunge wa mkoa huo kutokana na chama kinachotawala kwa zaidi ya miaka 50, wamekosa sauti ya kuzungumzia matatizo ya wananchi kwa sababu ya kulinda masilahi binafsi.

Zitto alifafanua kuwa ni jambo la kusikitisha kuona mikoa ya magharibi ikiwa nyuma kimaendeleo licha ya kuchangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni katika pato la taifa kupitia kilimo cha tumbaku: “Ninatafakari upya uamuzi wangu wa kuachana na siasa, ni vigumu kama sitashirikiana na wenzangu kuhakikisha hali hii ya watu kugombea maji ya kunywa na wanyama katika shimo moja inakwisha,” alisema.


Aliwataka wananchi wawaunge mkono pale wanapopambana bungeni hata ikibidi kupanda juu ya meza au kutoka nje pindi masilahi ya watu yanapopuuzwa, kwa sababu ya kuwapo kwa wabunge wengi wa CCM ndani ya Bunge.

Zitto aliongeza kuwa serikali ya CCM imechoka na haiwezi kuongoza na kwamba kama ilishindwa kusimamia reli iliyojengwa na wakoloni haiwezi kuongoza nchi iliyogubikwa na umaskini licha ya kuwa na utajiri kila sehemu: “Laiti kama mngejua yale tunayoyajua na kuyapigania bungeni hususan ufisadi unaofanywa na serikali ya CCM, naamini wananchi mngeingia barabarani kuhakikisha serikali hii inatoka madarakani,” alisisitiza.

Akizungumzia uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kujadili muswada wa sheria wa Katiba, Zitto alisema ni wazi amedhihirisha kwamba Waziri Stephen Wassira alikuwa akiongea kitu ambacho hakijui.

Alisema wakati wapinzani walipotoka bungeni kupinga muswada huo, Wassira alisimama hadharani na kusema kwamba wapinzani hawatapata fursa nyingine ya kujadiliana na Ikulu kuhusu Katiba.

Akiwa katika Kata ya Loya, Jimbo la Igalula, Zitto alisema kitendo cha serikali kuwanyanyasa wafugaji ni udhalilishaji dhidi ya utu, kwa kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi sehemu yoyote ili mradi asivunje sheria.

Alisema viongozi wa CCM wamekuwa wakiwatumia wafugaji kama mifuko yao ya hifadhi, kwa kujipatia fedha kinyume cha sheria, hali aliyoelezea kuwa ni ukiukaji wa utawala bora.

Zitto alieleza kusikitishwa na taarifa ya walimu wa Kata ya Loya kuwa wanatumia sh 20,000 kwa ajili ya kuweza kufika barabara kuu ya kuelekea mjini Tabora kufuatilia mishahara yao. --- via TanzaniaDaima.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.