IMEGUNDULIKA
kwamba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) ndiye mfadhili mkuu na mpanga
mikakati mkuu wa kundi linalomfuata Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(CHADEMA), ambalo limeanzisha chama kipya cha siasa, Allaince for Change and
Transparency (ACT-Tanzania).
|
Mbunge wa Monduli, Mh Edward Lowassa |
Kwa wiki kadhaa za hivi karibuni,
makundi ya wanachama, washauri na wapanga mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa
wakikutana katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo
kuu likiwa ni jinsi ya kumega Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
katika mapande ili kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu 2015.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya
habari, Lowassa amejiaminisha kwamba ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia
CCM. Kazi kubwa anayoona mbele yake ni kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili
kupunguza upinzani wakati wa kampeni utakapofika.
Zitto naye, ambaye uanachama wake
kwa CHADEMA umebaki kwenye makaratasi tu, anatajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa
ACT, na amekuwa na uhusiano wa “kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye
matata ya wazi na chama chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua vyeo
vyake vyote vya uteuzi ndani ya CHADEMA kwa tuhuma mbalimbali.
Katika hatua mojawapo, chanzo
kimoja kilicho karibu na Lowassa kimesema kwamba mapema mwaka juzi, Zitto
alimwendea Lowassa na kumwambia kuwa mustakabali wake kisiasa ndani ya CHADEMA
si mzuri, na kwamba alikuwa tayari kumsaidia Lowassa kufanikisha malengo yake,
lakini kwa sharti kwamba iwapo mbunge huyo wa Monduli atafanikiwa kupata urais,
basi amteue kuwa Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kauli
hiyo kwanza ilimstua Lowassa kwa sababu ilimuonesha Zitto kama kiongozi asiye
mwaminifu, ambaye yupo tayari kufanya hujuma dhidi ya chama chake, jambo ambalo
lilimfanya Lowassa atilie shaka lengo la ombi hilo.
Jambo la pili lililomshtua Lowassa
ni cheo kilichopendekezwa na Zitto, maana kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri
Mkuu lazima atokane na wabunge wa majimbo, na awe kwenye chama chenye wabunge
wengi.
Kwa kuwa hoja hiyo ilitolewa
katika mazingira ya Katiba ya sasa, na kwa kuwa haikujulikana wakati ule kama
Zitto alikuwa bado ni mwanachama na kiongozi wa CHADEMA, Lowassa hakuipata
nafasi kauli hiyo, lakini amekuwa anaitumia kujadili sura halisi ya Zitto.
Hata hivyo, taarifa zinasema
uhusiano wao umeimarika baada ya Zitto kuchukuliwa hatua na CHADEMA, huku
wapambe wa Lowassa wakipita huku na kule kusambaza propaganda kuwa CHADEMA bila
Zitto inakufa.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa
zinasema Zitto anatarajiwa kujiunga rasmi na ACT mwanzoni mwa mwezi Septemba
mwaka huu, na timu ya Lowassa imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya
mpasuko ndani ya CHADEMA, na kuipa CHADEMA mpinzani mpya ambaye ataifanya
ishindwe kumfuatilia na kumshambulia Lowassa.
Katika kikao cha mwisho
kilichofanyika kati ya timu ya Lowassa na “Vijana wa Zitto” kilijumuisha baadhi
ya wapambe wakuu wa Lowassa wenye kauli ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, watu
wa karibu kifamilia na Lowassa na washauri wa karibu wa Zitto, akiwamo Mhadhiri
mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ajenda zao nje
nje
Moja ya ajenda zao kuu ni
kufadhili na kupandikiza watu ndani ya mfumo wa CHADEMA ambacho kinaendelea na
uchaguzi wa ndani, ili wapate nafasi za uongozi, wazitumie kupata taarifa na
mipango ya chama, na baadaye wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT, na kuleta
msisimko wa kitaifa.
Gazeti hili lina taarifa kutoka
kwa baadhi ya viongozi wa sasa wa CHADEMA ambao “Vijana wa Zitto” wamekuwa
wakiwapigia simu na wakati mwingine kuwatembelea na kuwashawishi ahadi ya fedha
na vyeo ili wajiondoe CHADEMA.
Baadhi hao ni viongozi wa majimbo
na mikoa ambao katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hawana uhakika wa
kuchaguliwa kutokana na upinzani mkubwa unaojitokeza baada ya chama kukua na
kuvutia wasomi na wafanyabaishara wenye mvuto katika maneo yao.
Baadhi ya viongozi walioendewa au
kupigwa simu wamechukua tahadhari, na wametoa taarifa panapohusika ndani na nje
ya chama.
Mbinu mojawapo ambayo imekuwa
inatumiwa na “Vijana wa Zitto” kujaribu kuvunja ngome za CHADEMA ni
kuwatangazia viongozi hao kwamba ipo idadi kubwa ya wabunge wa CHADEMA
wanaotarajia kujiunga na ACT. Wanawataja majina kama njia ya kujenga ushawishi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi hao
wameliambia gazeti hili kuwa wanajua hizo ni mbinu za kipropaganda. Na baadhi
ya wabunge wanaotajwa wamesema hizo ni mbinu za Zitto kutaka kuwagombanisha na
chama chao na kujitafutia njia mpya kwa kutumia majina yao.
Mmoja wao alisema, “Zitto mwenyewe
ameshalikoroga. Sasa hii ni tabia ya kututaja baadhi yetu, mimi na wenzangu
kadhaa tumeshasikia, ni ile ile roho mbaya ya tukose wote. Kwa kuwa yeye
amekosana na chama, anatafuta watu wa kufa naye.”
Mbali na kupandikiza wagombea
nafasi za uongozi na kuvizia viongozi wanaoogopa joto la uchaguzi ndani ya
chama, wamekuwa pia na mbinu ya kushawishi baadhi ya “wagombea watarajiwa”
katika baadhi ya majimbo, wanaotajwa kuweka nia ya kugombea nafasi za uongozi
kupitia CHADEMA.
Makada kadhaa kutoka maeneo
mbalimbali ya nchi wamezungumza na gazeti hili na kutumia kauli zijazofanana.
Kwa mfano, makada sita walioweka nia ya kugombea ubunge katika majimbo kadhaa
ya kanda ya Ziwa Mashariki na Magharibi, wamekiri kwamba kila wanapojadili
mkakati huu na “Vijana wa Zitto,” kila mmoja wa nafasi yake anapewa ahadi ya
kupewa pesa zote za kufanyia kampeni.
Vile vile, baadhi yao wamesema
kuwa wanaambiwa kwamba iwapo watakubaliana na mpango huo wa ACT, moja kwa moja
watakuwa wamepitishwa, maana chama hicho hakina mpango wa kupata wagombea kwa
kutumia kura za maoni.
Taarifa zinasema sehemu ya malengo
ya vikao ya Zitto na Lowassa ni kutafuta pesa kwa ajili ya mradi huu.
Zipo taarifa zisizothibitishwa
kwamba mwezi uliopita Lowassa aliambatana na Zitto katika ziara ya kimya kimya
ya Mkoa mmoja wa kanda ya Ziwa ambako anasemekana anataka kujenga ngome nzito
ya ACT.
“Ninachojua ni kwamba iwapo ACT
itafanikiwa kupunguza makali ya CHADEMA, Mzee atapita kirahisi, maana kikwazo
kikubwa alichonacho hadi sasa hakipo ndani ya CCM, bali CHADEMA,” alisema mtoa
taarifa wetu aliye karibu na Lowassa, ambaye hakutaka kuthibitisha kama wawili
hao walisafiri pamoja kwenda Kanda ya Ziwa.
Mkono mrefu wa
CCM ndani ya ACT
Mbali na ufadhili wa Lowassa,
imebainika pia kwamba makada wengi wa CCM wamewekeza raslimali zao katika
kuinua ACT na kudidimiza CHADEMA.
Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa
mbali na Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, mmoja wanaoratibu kazi ya Zitto
ni kada wa CCM, ambaye ni mdogo wa mmoja wa mawaziri waliojiuzulu katika sakata
la Operesheni Tokomeza, anayetokea kanda ya Kusini.
Wengine wanaotuhumiwa kujihusisha
na mradi huu wa Tokomeza CHADEMA ni Naibu Waziri mmoja ambaye ni bingwa wa
propaganda za CCM, na ambaye amewahi kutangaza hadharani kuwa ifikapo 2015
CHADEMA kitakuwa kimekufa. Wamo pia wabunge na viongozi kadhaa waandamizi wa
CCM, ambao licha ya kwamba hawamuungi mkono Lowassa, wanafurahia msukosuko
wowote utakaokipata CHADEMA kuelekea 2015.
Mwingine ambaye anadaiwa kufadhili
ACT ni mtoto wa kigogo, ambaye katika miaka ya karibuni ameingia kwenye kashfa
nyingi, kabla ya kukwaa ubunge hivi karibuni.
Madiwani
waliohama waomba radhi warejeshwe
Wakati huo huo, madiwani wawili
waliohamia CCM kutoka CHADEMA, katika kata za Ngokolo na Masekelo, Shinyanga,
Sebastian Peter na Zacharia Machafuko, wameibuka na kusema wanajutia uamuzi
wao, na sasa wanafanya jitihada za kuomba warejeshewe uanachama wa CHADEMA
baada ya kukerwa na hila za CCM na ACT.
Madiwani hao wanadai kuwa
walihamia CCM kwa muda kwani waliambiwa kuwa ACT kitakapokuwa kimepata
usajili wa kudumu wangejiunga nacho ili kuimarisha upinzani nchini.
Madiwani hao walijiunga na CCM
Februari mwaka huu na kupokelewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nauye. Baadaye, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa alikituhumu CCM kwa
mchezo mchafu.
“Tukishawishiwa kuhamia CCM kwa
muda kwa lengo la kuhamia ACT ili kikipata usajili wa kudumu tuhamie huko
pamoja na baadhi ya wanachama wa CCM.
“Tuliambiwa tufanye siasa za
harakati, lakini tulichobaini ni kuwa tangu tukubali mawazo hayo ya viongozi wa
ACT tukijua tunaimarisha upinzani imekuwa tofauti. Mkakati huo ulianza
kuratibiwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Abbakari Gulam ambaye ni mtoto wa Meya wa
Shinyanga, wakiwa na Habib Mchange, kisha tuliona mkakati unatekelezwa na
mbunge wa Shinyanga mjini, Stephen Masele, Nape Nauye, Januari Makamba, Mwigulu
Nchemba na Ridhiwani Kikwete,” walisema katika taarifa yao mbele ya waandishi
wa habari jijini Mwanza.
Wakisimulia mkakati huo walisema
walifikishwa Tinde na kiongozi huyo wa UVCCM kisha wakiwa huko walipigiwa simu
na Stephen Masele na kuzungumza Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyewahakikishia
kuwa baada ya kuondoka CHADEMA watajiunga na ACT ili iwawezeshe kupata nafasi
za uongozi wa kitaifa katika chama hicho kipya, pamoja na kupatiwa kitita
kikubwa cha fedha.
Chanzo chetu cha habari kutoka
Shinyanga kimeelezwa kuwa baada ya kuhamia walipatiwa kiasi kikubwa cha pesa
bandia, na katika kitita hicho waliambulia laki mbili ndio zilikuwa halali,
pesa hizo zimetajwa kuwa zilikuwa ziwe milioni kumi na mbili lakini bada ya
kuhesabu zilipatikana halali laki mbili tu, na zinadaiwa kutolewana na msaidizi
wa Masele akiwa na Mchange katika hoteli ya Karena iliyopo Shinyanga, kabla ya
madiwani hao kuondolewa na gari hadi Mwanza na kusafiri kwa ndege hadi Dar es
Salaam kwa maelekezo ya Nape.
Tamko hilo linaongeza kuwa “kwa
kipindi chote cha kudanganywa tulidhani Zitto anaonewa, hivyo tukaamua kujiunga
na Chama chake ambacho alituhakikishia lakini tumebani kuwa ACT na CCM hawana
tofauti, mikakati inatengenezwa na ACT ila watekelezaji ni CCM, baada ya
kubaini ghiliba hizi tumeshindwa tumetafakari kuwa hata barua zetu tuliandika
zikiwa na makosa ya kikanuni hivyo sasa tumemwandikia tena Meya kumuuliza ni
kwanini hajatualika kwenye vikao viwili kwa kuwa tulikuwa hatujajiuzulu
kisheria.
“Ili mtu kujiuzulu udiwani, kanuni
zinasema kuwa diwani anaandika barua kwa Meya, unaambatanisha na kitambulisho
cha udiwani, na hati ya ushindi ya udiwani ambayo hatujawapa wala vitambulisho
vyetu, tulichokifanya ni kama kuandikiana barua za kawaida tu, na mtu kutangaza
kujiunga na Chama kiingine bila kuchukua kadi yao sisi sio wanachama wao na kwa
kuwa Chama chetu hakijachukua hatua zozote dhidi yetu basi tunarejea kwetu
upinzani kushindana na CCM,” alisema Sebastian mbele ya waandishi wa habari.
Walisema CCM na ACT waendelee na
kamari zao kuhadaa watanzania, “jamaa hao wana umakini kidogo ndio maana hawakubaliani
kuwa bado hatujajiuzulu kisheria wakakimbilia kutupeleka jukwaani kushangilia,
sasa sisi tunarudi kutumikia wananchi wetu kwani hatujavunja sheria,
hatukukiuka kanuni za kujiuzulu furaha ya CCM na ACT ni ya muda tu, tulionda
huko tumewabaini.
Kufuatia hali hiyo,madiwani hao
waliandika kuwa “tunapenda kuomba radhi viongozi wote wa CHADEMA, wanachama na
watanzania wote watusamehe, watupokee tukapambane kufanya kazi ya siasa za
upinzani wa kweli kuleta ukombozi wa kweli kwa nchi yetu, tulichokiona huku
tumekijua, tunawatahahadharisha wengine wakionga inafaa wajiunge huko kwa
hasara yao ya maisha yao kisiasa na kufanya kazi ya kujenga CCM.”
Mkakati huu unaratibiwa na mmoja
wa wabunge wa upinzani mwenye mahusiano ya karibu na viongozi wa CCM na
serikali anayedaiwa hadi sasa kuifadhili ACT mabilioni ya shilingi kwa ajili ya
kujiimarisha mikoani kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Kazi ya wanazi
wa ACT waliofukuzwa CHADEMA
Kwa sehemu kubwa, imebainika pia
kwamba nguzo kuu za ACT ni makada wa zamani wa CHADEMA ambao kwa sababu kadhaa
walipata misukosuko ndani ya chama hicho na kuchukuliwa hatua kali au kufukuzwa
katika maeneo kadhaa ya nchi.
“Sisi hapa Mwanza tunatambua fika
kwamba. Meya Henry Matata, Diwani Adam Chagulani wa Igoma, na Mushumbusi ndio
vinara wa ACT wanaotumika kujaribu kusambaza ACT kanda ya Ziwa, na kujaribu
kupenya na kubomoa ngome ya CHADEMA. Kwa sasa hata Habib Mchange wa Pwani, yupo
Mwanza anaratibu mipango ya uzinduzi wa chama chao utakaofanyika mapema
mwezi ujao.
“Lakini hapa kuna ukweli ambao
haupingiki, kwamba watu hawa walishafukuzwa CHADEMA, na sasa wanafanya siasa za
chuki na visasi, wakiajribu kurubuni wanaCHADEMA. Pili, ni ukweli kwamba
CHADEMA ni imara kuliko wanavyodhani. Haiwezi kubomolewa na wanachama wake wa
zamani waliaoamua kuwekeza katika Siasa za usaliti. Hata huko waendako
watasalitiana tu,” alisema kada mmoja wa CHADEMA mkazi wa Mwanza, ambaye
hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji.
Alipotafutwa John Nchimbi kwa simu
alisema jina lake litakuwa linachanganywa kwani yeye hajishughulishi na siasa
bali ni mdau wa michezo ambaye historia yake iko Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), huku Dk. Kitila naye akikana kushiriki mpango wowote wa
kuhujumu CHADEMA.
Alisema kuwa yeye ni mwanataaluma
ambaye hajihusishi na siasa za vyama na kwamba kama wako viongozi wa CHADEMA
wanarubuniwa na kukubali badi chama kinapaswa kujiuliza walipataje uongozi.
Fred Lowassa, Mwigulu Nchemba,
Nape Nnauye, Mshumbusi simu zao ziliita bila kupokelewa.