Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi kuendelea kuzisaidia redio jamii kwa lengo la kuhakikisha sauti za wanyonge zinapazwa na kusikika ili kukuza demokrasia nchini.
Mwalikishi
wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye
pia ni mshauri na mkufunzi wa Redio Jamii, Bi. Rose Haji Mwalimu
akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO Tanzania, Zulmira
Rodrigues kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo hicho cha redio jamii
Uvinza FM uliofanyika wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Kutoka
kushoto ni Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi,
Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya, Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwalimu Hadijah Nyembo.
|
Mwalikishi wa shirika hilo ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio
jamii Bi Rose Haji Mwalimu aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Redio
Jamii cha Uvinza FM kilichozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali
Mstaafu Issa Machibya.
Bi Haji alisema kwamba jitihada hizo ni kutokana na ukweli kwamba watu
wengi wanaishi vijijini ambako hawapati fursa ya kupata habari kwa wepesi kwa
ajili ya maendeleo yao kwa sababu wanaishi katika sehemu ambazo
hazifikiki kwa urahisi kutokana ya miundombinu duni ya mawasiliano.
“Takwimu zinaonyesha kwamba nchini Tanzania watu wenye uwezo wa kuangalia
telelvisheni ni asilimia 7 tu, kwa hiyo redio bado inachukua nafasi kubwa zaidi
ya upatikanaji wa taarifa kwa haraka, wepesi, urahisi na kwa mapana zaidi,”
alisema Bi. Rose Haji.
UNESCO ni shirika la Umoja wa Mataifa ambalo kwa muda mrefu limekuwa
likitoa msaada kwa redio jamii Tanzania katika kuzianzisha, kuzipatia vifaa na
kuzijengea uwezo kiufundi na mafunzo ili zijiendeshe zenyewe.
Redio zilizoanzishwa na UNESCO ziko chini ya mtandao maalum ujulikanao
kama Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA).
Mtandao huo, hutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuharakisha
maendeleo ya wananchi na ushirikishwaji wa wananchi kupitia redio jamii hususan
matumizi ya Tehama, mchakato wa Rasimu ya Katiba, uchaguzi wa serikali za mitaa
na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Takribani Redio za Jamii zipatazo 30, ikiwemo ya Uvinza
zinatekeleza mradi maalum wa Uchaguzi unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la (UNDP) kwa kushirikiana na UNESCO, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bara
na Unguja (NEC na ZEC) na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini (RPP).
“Redio zipatazo 30 zimeshapatiwa mafunzo yanayohusu maadili ya vyombo vya
habari, jinsia, na masuala ya jinsi ya kuandika habari za migogoro kwa
mtazamo chanya.
Viongozi wa serikali za mitaa pia watashiriki katika mradi huu
kuhakikisha uhalali wa mradi huo, wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na
makundi maalum pia katika kuhakikisha mwendelezo wa utamaduni wa
kuvumiliana, kujadiliana bila kugombana ili kuwezesha uchaguzi mkuu ujao
ufanyike kwa amani na utulivu.
“Nina uhakika kuwa ushirikiano huu utaendelea baada ya mafunzo haya na
kwamba redio jamii zitaleta mabadiliko makubwa kuhakikisha kuwa migogoro haina
nafasi katika jamii zetu. Vyombo vya habari vina wajibu wa kuhakikisha kuwa
vinaelimisha jamii juu ya athari za migogoro na kuhamasisha utulivu, amani na
uvumilivu katika jamii, ” alisema Bi. Rose Haji Mwalimu.
Wakati huo huo mwakilishi huyo wa UNESCO Bi Mwalimu ameuomba uongozi wa
halmashauri na wanajamii wa Uvinza kushirikiana na Redio Jamii Uvinza FM katika
mradi huu ambao utawanufaisha sana wanajamii wa Uvinza na Kigoma kwa
ujumla katika kuharakisha maendeleo.
“Redio hii ni yenu sio ya Kalufya, yeye ameianzisha kwa ajili ya maendeleo
ya Uvinza, kitumieni, kitunzeni na mshiriki kikamilifu ili mpaze sauti zenu kwa
maendeleo yenu na kudumisha Amani, upendo na utulivu kuelekea uchaguzi
Mkuu mwaka 2015,” alisema Bi Mwalimu.
Nae Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Bi. Hawa
Bayumi alisema kwamba Kampuni hiyo kwa kushirikiana na UNESCO bila kujali
biashara, imejikuta inalazimika kujihusisha na masuala ya kijamii katika
maendeleo kama shukrani za pekee kwa jamii kuruhusu minara ya kampuni kujengwa
sehemu zao.
“Ikiwa ni njia ya kuishukuru jamii kwa kuiruhusu kampuni kujenga minara
yake sehemu zao za kuishi, njia pekee ni kutoa msaada kwa wanajamii hao kuleta
mabadiliko katika changamoto zilizopo ambazo ni umaskini, unyanyasaji wa
kijinsia, na imani potofu za kishirikina kwa kuboresha miundombinu na
mawasiliano”, alisema Bi. Bayumi.
Kwa kupitia redio jamii Bi. Bayumi amesema changamoto hizo zitaisha kwa
kuhakikisha vipindi bora vinatayarishwa na kuhamasisha elimu kwa watoto, afya
masuala ambayo yanaipa kampuni ya Airtel alama kuwa ilichangia maendeleo katika
halmashauri ya Uvinza.
Kampuni ya simu ya Airtel imeahidi kuendelea kushirikiana na asasi husika
hususan redio za kijamii kwa lengo la kukuza majadiliano ya kidemodrasia
nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio hiyo. |
Mtangazaji wa kituo cha redio jamii Uvinza FM, Kadisilaus Simon akitekeleza majukumu yake kwa furaha kabisa mara baada ya kupewa baraka na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya. |
Post a Comment