Dar/Dodoma. Wakati Katiba inayopendekezwa
ikikabidhiwa kesho kwa Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hata akialikwa
katika sherehe hizo hatahudhuria kutokana na majukumu aliyonayo kwa
sasa.
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.PICHA|MAKTABA |
Jaji Warioba alisema angependa kuhudhuria sherehe
hiyo ambayo pia itahudhuriwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
wakuu wa mikoa, mabalozi na wageni mbalimbali, lakini kutokana na
dharura aliyoipata haitawezekana.
Sherehe hiyo itafanyika mkoani Dodoma kesho na
Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta
atakabidhi nakala ya Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Katika hafla hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa
Jamhuri, wajumbe wa Bunge hilo walioshiriki mchakato huo kuanzia mwanzo
mpaka mwisho watapewa vyeti.
Akizungumza na gazeti hili jana, Jaji Warioba
alisema hadi jana hakuwa amepata mwaliko lakini hata kama akipewa
hataweza kuhudhuria. “Siwezi kutoka nje ya Dar es Salaam kwa siku mbili
tatu hizi kwa sababu nina dharura. Kama wakinialika nitawaomba radhi
kwamba sitaweza kuhudhuria,” alisema.
Alipoulizwa iwapo Jaji Warioba ni miongoni mwa
waalikwa katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi
alisema angetoa majibu leo kuhusu suala hilo lakini anaamini mkongwe
huyo ni miongoni mwa viongozi wastaafu, hivyo kualikwa ni lazima.
Sherehe yenyewe
Mkuu huyo wa mkoa alisema sherehe hizo
zitatanguliwa na dua ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza Bunge hilo salama
ambayo itafanyika leo mchana katika Bustani ya Mwalimu Nyerere.
Wageni wengine walioalikwa ni pamoja na wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na wengine wastaafu.
“Hatuna uhakika na viongozi wengine kutoka nje ya nchi maana mwaliko
umetoka kwa muda mfupi, lakini mabalozi waliopo nchini wote tumewaalika
na makundi mengine yote kama wakulima, wasanii, wavuvi, wafugaji na kila
anayeguswa na Katiba mwakilishi wake lazima atakuwapo,” alisema Dk
Nchimbi.
Kuhusu orodha kamili ya waalikwa alisema: “Kesho
(leo) naweza kuwa na majibu mazuri kwa kila kitu maana tunashirikiana na
vyombo vingine katika kazi hii, kwa hiyo nitawaambia kwani vikao bado
vinaendelea.”
Awali, Naibu Katibu wa lililokuwa Bunge la Katiba,
Dk Thomas Kashililah alisema maandalizi ya sherehe hiyo yamefanyika
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Chanzno na gazeti la kila siku la www.mwanananchi.co.tz
Chanzno na gazeti la kila siku la www.mwanananchi.co.tz
Post a Comment