Raia Mwema: Unazungumziaje suala la Katiba mpya?

Jaji Warioba: Sina hakika kama viongozi wetu wanaelewa ni kitu gani kilicho muhimu. Nadhani tunaingia katika tatizo hili la kila mmoja anatazama manufaa yake.

Katiba hii msingi wake ulikuwa ni chama kimoja. Tumefanya mabadiliko kuna mambo ambayo yametokana na chama kimoja lakini ni ya msingi katika kuendesha nchi. Ni muhimu tuyatazame na kati ya hayo ni Tanzania ya aina gani tunayotaka kuijenga.

Moja ambalo limetokana na mfumo wa chama kimoja ni kwamba TANU, ASP na CCM vilikuwa na itikadi ambayo ilikuwa inafafanua tunataka Tanzania ya aina gani na wananchi wakaielewa.
Bila kujali ulikuwa unakubaliana na Ujamaa na Kujitegemea ulijua huu ndio mwelekeo wetu tunataka Tanzania ya Ujamaa na Kujitegemea. Ni Ujamaa na Kujitegemea na miiko yake ilikuwa inaeleweka nchi nzima. Wananchi walikuwa wanatoa uamuzi kulingana na itikadi.

Sasa hakuna. Hatujui ni Tanzania gani tunayotaka kuijenga na hapo nadhani tunapokwenda kwa wananchi tutarajie hilo kwamba kubwa tunalotaka kutoka kwa wanannchi ni Tanzania gani wanataka tuijenge.

Tusiende kwamba kulazimisha kuyazungumza haya tunayoona ni makubwa kwa sababu watazungumza kwa jinsi wanavyoona mambo yao. Unaweza kwenda sehemu ukakuta tatizo lao ni ardhi. Wengine wanaweza kuzungumzia madini. Tuyasikilize yote haya na kutokana na hayo utaona Watanzania wanataka Tanzania ya aina gani.
Katika kile kifungu cha malengo muhimu ya Taifa haya yaelezwe ndani ya Katiba kwamba Watanzania malengo waliyonayo ni haya.

Kwa hiyo, kwangu hili ni muhimu la sivyo tutabaki katika yale yale ya kujidanganya kwamba Tanzania ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea wakati ile misingi haipo. Lazima tujipange kuhakikisha tunajenga Tanzania tunayotaka. Katiba ni wananchi na wananchi waachwe waamue mambo yao muhimu.

Tusipofafanua Tanzania tunayoitaka bado tutakuwa na mgogoro kwa sababu hapatakuwa na yard stick ya kuwapima viongozi na Tanzania tunayotaka kuijenga.

Kuna suala la msingi kuwa wananchi ndiyo wenye madaraka. Lazima tueleze ni madaraka gani yako kwa wananchi, kwamba wana uwezo upi wa kukataa viongozi.

Saa hivi kuna kujichanganya, unakuta tunasema madaraka yako kwa wananchi lakini tumeyahamisha kwa kiwango kikubwa kwenda kwenye dola au kwenye vyama vya siasa.

Serikali utakuta imepewa madaraka makubwa lakini wanasema ni kwa niaba ya wananchi. Vyama vya siasa navyo ni hivyo, vimepewa madaraka makubwa nao wanasema ni kwa manufaa ya wananchi.

Sasa hivi pamoja na Katiba kusema kwamba msingi wa madaraka ni wananchi kwa hiyo wanachagua wawakilishi lakini bado msingi huo unabanwa kwamba unawaambia kama unataka mwakilishi lazima ufuate taratibu hizi. Kama wewe si mwanachama wa chama cha siasa basi huna nafasi hiyo.

Kwamba watu wanaweza kumchagua mwakilishi lakini chama cha siasa kinaweza kumfukuza huyu mwakilishi. Wanakorofishana ndani ya chama wanamfukuza na anapoteza mandate ya wananchi kama vile mwakilishi huyo alichaguliwa na chama. Lazima mipaka iwekwe ndani ya Katiba.

Baada ya hapo tuangalie zile taasisi muhimu, Bunge, Serikali na Mahakama tuangalie upya mgawanyo wa madaraka haya, ile separation of powers iwepo lakini pia lazima kuwapo checks and balances.

Sasa hivi nadhani itabidi tuimarishe Mahakama. Iwe na uhuru wa kifedha, wasitegemee hisani ya Katibu Mkuu wa Hazina.

Kama tumefika mahali unasema Bunge litapata bajeti kiwango fulani na vyama vya siasa vinapata bajeti fulani, Mahakama nayo lazima tuseme wanapata asilimia fulani.

Tuingie kwenye utendaji, tuangalie mgawanyo wa madaraka kati ya Rais na taasisi za utendaji. Najua Rais lazima atakuwa na madaraka lakini kuna mahali pengine ama madaraka haya yanaweza kwenda kwenye taasisi au utendaji wake Rais lazima ashauriwe.

Inawezekana tukaamua, je, kuna umuhimu wa kumpa Rais madaraka ya kuteua mawaziri lakini wawe wanathibitishwa mahali? Ateue majaji lakini wathibitishwe mahali.
Sasa hivi naona kuna watu hawataki Rais awe na madaraka makubwa lakini mimi nafikiri Rais lazima awe na madaraka isipokuwa tuangalie yale mengine awe nayo lakini kwa kushauriwa. Lazima katika Taifa kuwe na mtu mnasema lazima awe na madaraka haya, isipokuwa ni kutengeneza utaratibu.

Hata kama tunataka Rais wa kikatiba tu ingawa sioni hilo kama ni zuri katika nchi, kama tunataka awe waziri mkuu sawa. Lakini suala la madaraka ni muhimu.

Katika mabadiliko ya mwaka 1984 nia ilikuwa kupunguza madaraka ya Rais, Waziri Mkuu asimamie zaidi utendaji lakini sasa hivi unaona kama Waziri Mkuu hana madaraka ya kusimamia utendaji.

Imejitokeza Rais anasimamia utendaji, anakwenda wizara kwa wizara, anatoa maagizo ya utendaji, Katiba haijamzuia lakini imemuwekea mtu wa kumsaidia, nimeona kwenye Bunge Waziri Mkuu anaulizwa maswali ya papo kwa papo anazumgumzia sera. Sera si ya kwake, iko chini ya Rais.

Kwa hiyo tutakapozungumza Katiba ni lazima hapa tufafanue nini kazi za waziri mkuu au kama kuna sababu ya kuwa na waziri mkuu. Tuzungumze, je, mawaziri wawe kama walivyo kutokana na Bunge?
Bunge nalo liangaliwe, madaraka yake yafafanuliwe. Unajua wakati mwingine Bunge limeingilia mambo ya utendaji, lazima sasa iwepo mipaka kati ya Serikali na Bunge na tujue nani anastahili kuchaguliwa kwenda bungeni, tujue utaratibu wa kupiga kura.

Sasa hivi wanazungumzia sana Tume ya Uchaguzi. Tuzungumzie hili. Kuna watu wanafikiri lazima iwakilishe makundi fulani fulani. Zanzibar wanazungumzia uwakilishi wa vyama. Kwingine, Afrika Kusini wanaye kamishna. Ghana wanayo tume ambayo mwenyekiti ni yule yule, amekuwapo kwa muda kwa sababu yuko huru.

Naamini Tume yetu ikiwa na wajumbe kutoka vyama vya siasa haitakuwa huru. Nadhani utaratibu wa Katiba mpya utuwezeshe kupata maoni ya wananchi.

Ninachokiona sasa ni kila kundi kwa maslahi yake linatumia hoja ya wananchi kuwa wanataka utaratibu fulani. Vivyo hivyo, Serikali nayo inataka kuweka mipaka fulani kwa maslahi ya wananchi.

Tusiweke mipaka. Wananchi watoe mawazo yao.

 Kuna vyama vya siasa vinasema kwa manufaa ya wananchi tuwe na Bunge la Katiba ambalo litachagua Tume na kutoa hadidu za rejea na kusimamia mchakato na baada ya kupitisha watakwenda kwa wananchi.

Sikubaliani na hilo. Wananchi waachwe wazungumze yote wanayotaka, Katiba yao iweje. Wakishakuzungumza, hiyo tume itengeneze muswada wa katiba urudi kwa wananchi. Wazungumze, kusiwe na kikundi hapa katikati kinasema kwa manufaa ya wananchi. Hapana.

Wananchi wazungumze muswada na chombo cha kupitisha kipitishe baadaye. Wasilete vikao hapa katikati huku wanajitafutia nafasi. Mchakato huu uende moja kwa moja kwa wananchi. Tusiwawekee mawazo.
Kuna wanaharakati wanataka kuleta mambo ya kuwajaza wananchi. Nina hakika wananchi wakiachiwa uhuru, watasema na wataalamu watapanga vizuri. Nasisitiza la msingi ni kuwaacha wananchi waseme wanataka nchi ya namna gani.

Suala la Muungano pia liwe katika Katiba. Tusipokuwa makini kwa maneno yanayozungumswa sasa tutavunja Muungano.

Muungano huu una misingi yake na upo kwa manufaa ya wananchi. Tufafanue manufaa hayo ni nini kwa mwananchi wa kawaida.

Wakati wote kwa mwananchi wa kawaida, kumekuwa hakuna matatizo ya Muungano. Matatizo yanatoka kwenye midomo ya viongozi.

Shughuli za wananchi wa kawaida haziangalii orodha ya mambo ya Muungano, bali haki yao kama raia. Wanajiona ni raia katika shughuli zao za kibiashara au nyingine. Mwananchi wa kawaida anaona anayo haki ya kufanya biashara mahali popote.

Wananchi wamezoa hivyo. Msiwafikishe mahali wakajiona kuwa kwenda Zanzibar au kuja Bara inabidi wafuate taratibu za kwenda Kenya au Uganda.

Tunayo matatizo ya madaraka, kwamba unazo Serikali mbili kwa hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha Serikali hii ina madaraka gani. Wanagombania madaraka.

Kama suala ni mafuta au mengine tuzungumze. Inategemea mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo yatakuja kuwatenganisha wananchi. Kama kwa mfano, kuna watu wanafikiri kuimarisha Muungano ni kuwa na serikali tatu, unaimarishaje?

Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.

Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote.

Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi?

Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa.

Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa pande zote mbili. 

Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake unavunja Muungan

Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.