KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Serikali imesusia maadhimisho ya 15 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Hali hiyo imejidhihirisha jana baada ya MTANZANIA kutembelea yaliyokuwa makazi ya Mwalimu Nyerere, Msasani Dar es Salaam na kutokuta chochote kilichokuwa kikifanyika kama sehemu ya maadhimisho hayo.

Licha ya kutokuta dalili yoyote ya maadhimisho hayo, nyumbani hapo kulikuwa na watoto waliokuwa wakifanya usafi.

Waandishi wetu walipotaka kuonana na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, ili kujua kilichokuwa kikiendelea, mmoja wa walinzi wa makazi hayo alisema hakuwapo wakati huo bali alikuwa amekwenda kanisani kusali.

“Mbona hatukuwa na taarifa za ujio wa mgeni yeyote na wala hakukuwa na taarifa za kufanyika kwa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere hapa nyumbani?
“Lakini pia mama ni mgonjwa na ameshindwa hata kwenda Butiama kwa ajili ya maadhimisho ya kifo cha Mwalimu,” 
alisema mlinzi huyo.

KIJIJINI BUTIAMA

Kijijini Butiama ambako kulitarajiwa kuwa na maadhimisho ya kifo hicho, nako hakukuwa na chochote kilichofanywa na Serikali.

Kutokana na hali hiyo, hakuna kiongozi yeyote wa Serikali kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa aliyefika nyumbani kwa Mwalimu kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.

Katika kuonyesha kuwa haridhishwi na jinsi Serikali inavyomuenzi Mwalimu Nyerere, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema anakusudia kwenda mahakamani kukishtaki Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake kwa kile alichosema wameshindwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

Kwa mujibu wa Butiku, CCM na Serikali yake wametupa maadili ya Mwalimu Nyerere yakiwamo yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba.

Butiku aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Nyerere yaliyofanyika kijijini Butiama bila Serikali kushiriki.

“Katika kipindi cha miaka 23 niliyofanya kazi na Mwalimu, alikuwa akichukizwa na suala la kutofuata maadili ya uongozi kama inavyofanywa leo na viongozi wa CCM.

“Sijawahi kuzungumza jambo hili, lakini leo kupitia kumbukumbu ya maadhimisho ya kifo chake ambapo ni mwaka wa 15 tangu atutoke, nitaangalia namna ya kuwafungulia mashtaka CCM na Serikali.

“Kwa hili wala sitanii, mashtaka haya lazima yatafunguliwa kupitia wanasheria wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa hatukubaliani na namna anavyoenziwa,” alisema.

Butiku ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, alisema Mwalimu Nyerere alikuwa muumini mkubwa wa maadili na alikuwa akisisitiza uwapo wa usawa kwa watu wote tofauti na ilivyo sasa.

LUKUVI AZUNGUMZA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipoulizwa na MTANZANIA kuhusu Serikali kutoadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere, alijibu kwa kifupi: “Wewe mwandishi, swali lako limepitwa na wakati, hebu kafanye mambo mengine, kwa sasa niko kwenye mkutano mwingine.”

Pamoja na kutoadhimisha kifo cha Mwalimu Nyerere, jana kulikuwa na sherehe za kitaifa za kuzima mwenge wa uhuru zilizofanyika mjini Tabora.

Katika sherehe hizo viongozi wengi wa kitaifa wa chama na Serikali walikuwapo wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Habari hii imeandikwa na Asifiwe George, Shaban Matutu (Dar) na Shomari Binda (Butiama).

Mtanzania: Butiku kuishtaki CCM

Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.