Augustino Ramadhani |
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyosimamia uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa wa vyama vingi vya siasa wa mwaka 1995, Jaji Augustino Ramadhani, amesema kwamba uchaguzi huo katika jiji la Dar es Salaam ulihujumiwa.
Jaji Ramadhani alibainisha hayo katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuulizwa kile ambacho hatakisahau katika kipindi chake cha utumishi alipokuwa NEC.
“Kitu ambacho sitakisahau nilipokuwa makamu mwenyekiti wa NEC ni ule uchaguzi wa kwanza wa Multipartism (vyama vingi) Dar es Salaam, mwaka 1995,” alisema.
Jaji Ramadhan alisema wote waliokuwa katika tume hiyo hawatausahau uchaguzi huo kutokana na
kwenda kinyume cha walivyokuwa wamepanga.
“Tuliamka asubuhi na mapema kwenye kama saa kumi na mbili, tukaenda kwenye vituo vyetu tukapiga kura na baada ya kupiga kura tukakutana na kugawana majimbo kwa ajili ya kwenda kuyasimamia,” alisema Jaji Ramadhani.
Alisema jimbo lake lilikuwa Ukonga, huku viongozi wengine wa tume wakienda katika sehemu nyingine za majimbo saba ya mkoa wa Dar es Salaam. Alisema mpaka alipofika Ukonga hadi saa nane mchana Magereza Shule ya Msingi palipokuwa na vituo saba, alikuta hata kituo kimoja hakijafunguliwa kufanya kazi kutokana na kutowasili kwa vifaa.
“Nilikuta wengine kwenye vituo hivyo wana wino, wengine wana kalamu, wengine wana mihuri na hakuna hata kituo kimoja kati ya vituo saba kimefunguliwa pamoja na kwamba pale si shamba,” alisema Jaji Ramadhani.
Alisema baada ya kukuta hali ikiwa hivyo, waliwasiliana na kukubaliana kukutana kwenye ofisi ya tume na kuichambua hali hiyo na baadaye kugundua kuwa ilikuwa hivyo hivyo karibu jiji lote la Dar es Salaam.
“Tukakubaliana pale pale tufute uchaguzi wa Dar es Salaam, tulikaa pale mpaka saa nane za usiku huku tukinywa kahawa na biskuti tu, hata kule kuagizia lunch box hatukuagizia,” alisema.
Alisema walikubaliana wakapumzike ili wakutane tena kesho yake saa mbili ambapo walikubaliana kuufuta uchaguzi kwa majimbo yote ya Dar es Saalam.Alisema baada ya kuufuta uchaguzi huo, kazi yao ilibakia kuwa ni kuita mabalozi wa nchi mbalimbali ili kupata msaada wa kugharimia uchaguzi wa marudio kwa jiji la Dar es Salaam.
“Tukamuita Balozi wa Denmark ambaye yeye alitusaidia sana wakati wa maandalizi ya uchaguzi, akasema hana pesa, tukamuita Balozi wa Uingereza aliyetusaidia kupiga mashine ballot papers (karatasi za kura), ambaye alikubali kutoa msaada.
Alisema, Balozi wa Uingereza alitoa fedha za kuchapa karatasi za kura za udiwani, ubunge na rais.
“Nikasema alhamdulillahi sasa ikabaki sisi na serikali yetu tugombane kupata fedha za mambo mengine ndipo tukarudia ule uchaguzi, lakini siku ile kabisa sitaisahau na naamini ilikuwa ni hujuma,” alisema Jaji Ramadhani, ambaye hata hivyo, hakudokeza mtu au kikundi chochote walichohisi kufanya hujuma hiyo wala lengo lao.
Alisema hajui ni nani alifanya hivyo kwa sababu mwenzake aliyekuwa kwenye jimbo lililokuwa likijumuisha maeneo ya Magomeni, Kinondoni mpaka Ubungo, alikwenda ofisi ya mkuu wa wilaya ambapo napo alikuta hakuna kinachofanyika.
Alisema baada ya kuamua kuuvunja ule uchaguzi, siku ya pili walikwenda kwa DC Magomeni pembeni wakakuta kuna karatasi za kura, si moja na kushangaa kwani siku ya uchaguzi karatasi hizo hazikuwapo.
Alisema hajui aliyehujumu na sababu zake na kuwa waliwaita wasimamizi wote wa uchaguzi na wakahojiana nao, lakini hakuna majibu ya maana waliyowapa.
“Wengine walisema ooh gari sijui ilikwenda ikapata pancha na yuko mmoja mwanamama alisema Jumamosi alikuwa kwenye harusi ya mtoto wake, kwa hiyo Jumapili akaamka na uchovu wa harusi, hatukuwa na la kufanya,” alisimulia Jaji Ramadhani.
Alisema baada ya kuamua kurudia uchaguzi huo mkoani Dar es Salaam baada ya wiki mbili, walitumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo ndilo lililotoa magari na walipeleka vifaa na kufanikiwa kwa sababu Jeshi lina nidhamu.
Post a Comment