Serikali inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa hivi karibuni
kumezuka kundi la Watu wadanganyifu ambao wamekuwa wakitumia majina ya
viongozi waandamizi wa serikali na Taasisi nyeti ikiwemo Usalama wa
Taifa kujipatia fedha kwa madai ya kutumwa na viongozi hao.
Watu
hao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa simu (SMS) kwa maofisa mbalimbali
wa wizara, mashirika ya umma na Idara za Serikali zinazojitegemea
kuomba pesa ili wawafanye mipango ya kupandishwa vyeo.
Utapeli
huo umekuwepo nchini kwa kipindi kirefu sasa, ambapo watu huwapigia
simu viongozi wa Taasisi za fedha, Mifuko ya Taasisi za Jamii na watu
binafisi wakiomba fedha kwa madai ya kutumwa na viongozi waandamizi
Serikalini wakati si kweli.
Watu hao wamekuwa
wakiwatapeli maofisa mbalimbali kuwa wanaweza kuwafanyia mipango ya
kupandishwa vyeo endapo watawapatia kiasi cha fedha jambo ambalo halipo
katika taratibu za utumishi wa umma.
Utumishi wa
umma unazo taratibu zake za kuwapandisha vyeo watumishi wake kulingana
na sifa za kada zao na wala haiwezekani kwa viongozi waandamizi
kuwachangisha fedha kwa ajili ya kuwapandisha vyeo. Serikali inawataka
wananchi kuwapuuza matapeli hao na watoe taarifa katika vyombo vya dola
na usalama mara wapatapo ujumbe wa aina hiyo ili hatua zichukuliwe
dhidi yao.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI (MAELEZO)
DAR ES SALAAM.
12.02.2013
Post a Comment