Imeandikwa na Happiness Katabazi
HATIMAYE upande wa Jjamhuri
katika kesi ya uchochezi na kuiba malighafi zenye thamani ya Sh. milioni
59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda
Issa Ponda na wenzake 48, umetangaza rasmi kuifunga kesi yake.
Hayo
yalisemwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka mbele ya
Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es
Salaam, muda mfupi baada ya shahidi wa 17 wa upande wa Jamhuru D/C F8586
Ismail wa kituo cha Polisi Chang’ombe kumaliza kutoa ushahidi wake
ambapo jana jumla ya mashahidi watatu kwa mpigo walitoa ushahidi wao.
Wakili
Kweka alieleza kuwa hadi kufikia jana upande wa Jamhuri ulikuwa
umeleta mashahidi 17 na vielelezo 13 ambavyo vilipokelewa mahakamani
kama vielelezo vimetosheleza upande wa Jamhuri kufikia uamuzi huo wa
kuifunga kesi yao.
Baada ya wakili Kweka kutoa maelezo hayo
wakili wa Ponda, Juma Nassor aliiomba mahakama iwapatie muda hadi Machi 4
ili waweze kwenda kujiandaa na kufanya utafiti utakaowawezesha
kuwasilisha maombi ya kuwaona wateja wao wote 49 hawana kesi ya kujibu.
Hata
hivyo, Hakimu Nongwa alisema jukumu la kupanga tarehe ya kuja kufanya
majumuisho ya mawakili wa pande hizo mbili katika kesi hiyo ya kuwaona
washitakiwa wanakesi ya kujibu au la ni vyema ikaachiwa mahakama. Hakimu
huyo akatoa amri kuwa majumuisho hayo yatafanyika Februali 27, 2013,
saa mbili asubuhi na kuutaka upande wa utetezi kuwa wa kwanza
kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo.
Kabla ya Hakimu
Nongwa kukubali ombi la upande wa Jamhuri majira ya saa nane mchana, la
kuifunga kesi yake, alisikiliza ushahidi wa mashahidi watatu wa
waliokuwa wameletwa na upande wa Jamhuri ambao ni shahidi wa 15 ambaye
ni F3929 D/C Constebo Eliaeli (35), shahidi wa 16 ambaye ni Stationi
Sajenti Amos wa kituo cha Polisi Kati na Shahidi wa 17 ambaye ni askari
mpelelezi Na. F8586 D/C Ismail.
Kwa upande wake shahidi wa 17,
D/C Ismail aeleza mahakama kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa kazi na
Mkuu wake wa kazi na saa 2-9 alasiri alikuwa katika kituo cha Polisi
Kijinyoma alipewa jukumu la kuwahoji washitakiwa ambao walikamatwa
katika kiwanja cha Chang’ombe Marskas wakikabiliwa na makosa ya kuingia
kwa jinai katika kiwanja hicho .
Ismail alidai kuwa yeye
alimhoji mshitakiwa aitwaye Fiswaa ambaye alimweleza kuwa kati ya
tarehe, mwezi na saa isiyofahamika akiwa nyumbani kwake Mlandazi Mkoani
Pwani, akiwa anasikiliza Redio Iman, alisikia tangazo lilokuwa
likiwataka waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kuongeza nguvu ya kujenga
msikiti katika kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya waislamu
na si BAKWATA, lakini kilikuwa kimevamiwa.
Shahidi huyo alidai
kuwa, mshitakiwa huyo alimweleza kuwa aliitikia wito huo na kufunga
safari toka nyumbani kwake Mlandizi na kwenda hadi kwenye kiwanja hicho
kilichopo Dar es Salaam, na kuungana na wenzake ambapo kiongozi wao
aliyekuwa akiwaongoza walipokuwa kwenye kiwanja hicho ni mshitakiwa wa
kwanza ambaye ni Sheikh Ponda.
“Sululu, mapanga vilitumika kama
vifaa vya kujengea msikiti wa muda katika kiwanja hicho na ndipo usiku
wa kuamkia Oktoba 17 mwaka jana, tukiwa tumekaa kwenye kiwanja hicho
nikasikia sauti ikisema kuwa panda kwenye gari, panda kwenye gari na
sikuwa na kumbukumbuku yoyote...,’ alidai Ismail kuelezwa na Fiswaa.
Maelezo ya mshitakiwa huyo yalipokelewa kama kilelezo cha 13 na
hakikupingwa na mawakili wa utetezi.
Kwa upande wake shahidi wake
Shahidi wa 16, Station Sajenti Amos, alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana
alipewa jukumu la kumhoji mshitakiwa Hussein Ally ambaye mshitakiwa
huyo alimweleza kuwa alipokea maelekezo kutoka kwa Masheikh wake wa
Msikiti wa Kinyerezi yakimtaka afike katika kiwanja cha Markas na
alienda akakutana na wenzake ambapo walianza kufanya usafi ili waweze
kujenga msikiti na walikuwa wakiongozwa na Sheikh Ponda kufanya ujenzi
na usafi katika kiwanja hicho ambacho tayari mashahidi wengine kutoka
BAKWATA walishasema kiwanja hicho ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd,
na siyo BAKWATA tena. Maelezo ya mshitakiwa hayo yalipokelewa kama
kielelezo cha 12.
Aidha, shahidi wa 15 , D/C Constebo
Elieli alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa jukumu na mkubwa wake
wa kazi la kuandika maelezo ya mshitakiwa Mohamed Ramadhan ambaye
alimweleza kuwa siku hiyo yeye alikwenda kusali katika eneo la kiwanja
hicho akitoa Oysterbay Dar es Salaam. Elieli alieleza kuwa mshitakiwa
huyo alimweleza kuwa alifikia uamuzi wa kwenda kusali swala ya alfajiri
hapo Chang’ombe Markas kwa sababu alikuwa anauguliwa na ndugu yake
anayeishi Keko. Yeye mshitakiwa hakutaka kwenda kuswali Msikiti ya Keko
kwa sababu hali ya usalama ilikuwa mbaya na hivyo akaamua kwenda kusali
katika eneo hilo la Markas.
“Mshitakiwa huyo akanieleza eti baada
ya kusali hapo alfajiri ya Oktoba 17 mwaka jana, ndiyo ghafla
alishitukia anakamatwa na mapolisi. Nilipomhoji kama analifahamu
vuguvugu la Waislamu kudai haki zao, mshitakiwa huyo alikubali
kulifahamu vuguvugu hilo na kwamba yeye pale kwenye lile eneo
alipokamatiwa alikuwa katika kutetea na kudai haki yao ya kurejeshewa
kiwanja kile ambacho ni mali ya Waislamu na si BAKWATA,” alidai Elieli.
Hata hivyo, mahakama ilikataa kuyapokea maelezo hayo kama kielelezo kwa
sababu yana dosari nyingi za kisheria.
Awali Oktoba 18 mwaka
jana, ilidaiwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo na wakili Kweka mbele
ya Hakimu Nongwa kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano
likiwemo kosa la kula njama,wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.
milioni 59 na uchochezi ambalo linamkabili Ponda na mshitakiwa wa tano,
Sheikh Mkadam Swalehe ambao wanaendelea kuzuiliwa gerezani kwa sababu
Mkurugenzi wa Mashitaka, DPP, Dk Eliezer Feleshi bado hawajaondolea hati
ya kuwafungia dhamana.
Post a Comment