Matokeo mabovu --pengine-- kuliko yote ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato
cha Nne kuwahi kutokea katika historia ya taifa la Tanzania yamezua
balaa la aina yake baada ya wanafunzi wawili kujiua kwa kujipiga vitanzi
hadi kufa.
Taarifa zilizothibitishwa leo na jeshi la Polisi
zimeeleza kuwa wanafunzi waliojiua kutokana na matokeo hayo ni wa jijini
Dar es Salaam na mwingine kutoka mkoa wa Tabora.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, amesema leo kuwa mhitimu
aliyejiua mkoani humo ni Michael Fidelis (19) mkazi wa Mtaa wa Mwinyi,
Kata ya Chemichemi aliyemaliza katika Shule ya Sekondari ya Kanyenye
mjini Tabora.
Kamanda Rutta amesema kuwa Fidelis amejiua kwa
kujinyonga hadi kufa baada ya kwenda kuangalia matokeo juzi Jumatatu
(Februari 18, 2012), saa 11:00 jioni. Baadaye akakutwa amejinyonga
chumbani kwake kwa kutumia kamba ya manila, kisa ikiwa ni kupada
divisheni ziro.
Taarifa kutoka kwa rafiki wa kijana huyo ambaye
maziko yake yalifanyika juzi, zilisema awali alipigiwa simu na kaka yake
aishiye Mbeya kumwambia kwamba matokeo yametoka.
Walisema
wakiwa kwenye intaneti, kijana huyo ambaye ni wa kwanza kuzaliwa kwa
mamake, alionekana amenyong’onyea, “Aliporudi nyumbani alinyong’onyea
zaidi. Hakusema chochote. Kumbe alipotoka hapo alikwenda kujinyonga,”
alisema mmoja wa watu waliokuwa naye.
Sehemu ya ujumbe alioacha marehemu Fidelis ulisomeka hivi: “Nisamehe sana mama, usitafute mchawi... nakupenda sana. Uamuzi niliouchukua ni sababu ya matokeo mabaya, nakutakia maisha mema.”
Matokeo
ya shule ya Kanyenye yanaonyesha kuwa wahitimu 85 walipata sifuri na
hakuna aliyefaulu kwa daraja la kwanza wala la pili.
Kwa mujibu
wa ndugu zake, kijana huyo alikuwa akiishi na ndugu zake nyumba tofauti
na mama yake ambaye alishaachana na baba yake mzazi na kuolewa na mume
mwingine. Ilielezwa kuwa alikuwa na kawaida ya kula usiku nyumbani kwa
mama yake. Lakini usiku huo hakuonekana na ilipofika saa 3 usiku
walikwenda na kukuta amejifungia ndani wakavunja mlango na kukuta
amekufa.
Jijini Dar es Salaam, aliyejiua kwa kujipiga kitanzi
baada ya kufeli ni aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Debrabant
iliyopo Mbagala, wilayani Temeke, Barnabas Venant (18).
Kamanda
wa Engelbert Kiondo wa mkoa wa kipolisi Temeke, amesema leo kuwa Vicent
alikuwa akiishi Nzasa na amejinyonga kwa manila akiwa ndani ya stoo ya
nyumba yao juzi saa 10:00 jioni baada ya kuambulia daraja la nne (Div
IV), kinyume kabisa na matarajio yake.
Post a Comment