Digitali yavunja ndoa za watu uswahilini
. Fumanizi zaongezeka mitaani
.Vijana wengi wakosa bongo flavour na maiigizo
. 40% ya wakazi wa jiji hawatizami Televisheni majumbani
.Wasanii wa kizazi kipya wakosa promo
   “Tangu mfumo wa digitali kuanza katika jiji la Dar es Salaam mahusiano ya wachumba na ndoa nyingi zinaendelea kuvunjika hasa sehemu za uswahilini kwa sababu wachache wenye ving’amuzi wanatumia kama nyenzo ya kupata wanawake hasa kwenye vipindi vinavyopendwa sana na watazamaji wakinamama,” anasema Alban Marcus.

Akizungumza na Clouds Television jijini Dar es Salaam, Bw Marcus ambaye ni Mkurugenzi wa (Citizen Public Watch) anasema huku uswahilini mafumanizi yameongezeka kwa kasi ya ajabu baada ya wenye ving’amuzi kutumia upenyo huo kutembea na wachumba na wake za watu.
Bw Marcus anasema kwamba mfumo wa digitali nchini Tanzania uliharakishwa bila ya kutolewa elimu ya kutosha Kwa wananchi wote Ili waelewe nini maana ya analogia na mfumo mpya wa digitali na manufaa yake kwa watumiaji wa televisheni hapa nchini.

Anasema kutokana na msukumo wa wafanyabiashara ambao wanawaza na kufikiri kibiashara zaidi na kutomdhamini mlaji ambaye ndio mtanzania wa hali ya chini mfumo huu mpya umewaweka pembeni watu wenye kipato cha chini hapa Tanzania.

Katika mfumo wa digitali Serikali ilifanya haraka kuzima bila ya kuwadhamini kwanza wananchi wake hasa wenye vipato vya kati na vya chini na hali ya kiuchumi kwa ujumla kabla ya kuwashirikisha kwa lazima katika mfumo mpya wa teknolojia.

Bw Marcus alisisitiza kwamba mfumo wa digitali ulipaswa uende sambamba na elimu ya teknolojia mpya kwa wananchi lakini cha kushangaza zaidi ni kwamba hata makampuni ya kusambaza ving’amuzi vilikuwa bado havijajipanga kwa mfumo mpya wa matangazo.

“Uhuru na haki ya kupata habari na matangazo upo kitanzini wananchi sasa wanalazimika kununua na kulipia taarifa ya habari na matangazo kwani tunarudi kwenye ujima?

“Kwa hakika mfumo huu hauwezi kuharakisha maendeleo maana upatikanaji wa habari na elimu ya uraia unasambaa kwa urahisi na haraka zaidi kwa njia ya televisheni hata kwenye kuunda mabaraza ya katiba mfumo rahisi wa mawasiliano ni huu wa televisheni,” alisema Marcus 

Wakati wa kuzima mtambo wa digitali ilikuwa ni kipindi cha mwisho wa mwaka kwamba watu wengi wenye hata kipato cha kati walikuwa wanajiandaa na karo za watoto wao mashuleni kwahiyo serikali ilikuwa inatakiwa kutizama hali za kiuchumi za wananchi wake kwa wakati husika.

Ilikuwa Desemba 31, mwaka jana ilikuwa mwisho wa mimi Mtanzania wa kawaida kutizama kipindi cha michezo cha sports bar kinachorushwa na Clouds TV ambacho ni mmoja wa vipindi bora na vinavyonisisimua sana,” anasema Said Khamis Mkazi wa jiji la Dar es Salaam.

Tanzania ilingia rasmi katika mfumo wa kurushia matangazo ya televisheni kwa njia ya dijitali kutoka katika mfumo wa analogia tangu mwaka katika mkoa mmoja pekee wa Dar es Salaam na kuacha maelfu ya wakazi wa jiji wenye kipato cha chini bila matangazo ya televisheni anasema khamis.

Huo ulikuwa ni usiku wa kuamkia Januari mosi mwaka huu, ambapo mitambo ya analojia ilizimwa na mamlaka husika kwa mkoa huu na kuungana na nchi nyingine duniani zilizotangulia kwenye mfumo wa digitali ili kwa kile kinachoelezwa kutoa picha na sauti nzuri.

Kuja kwa mfumo wa dijitali kulitokana na agizo lililotolewa na Tume ya Kimataifa ya Mawasiliano (ITU) kwa nchi zote duniani kuhamia kwenye mfumo huo ifikapo Julai, 2015.

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa ya kwanza kutekeleza agizo hilo mapema badala ya kusubiri hadi tarehe ya mwisho iliyowekwa na ITU.

Katika kufanikisha hilo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa vibali kwa kampuni tatu kufanya kazi ya usambazaji wa mfumo wa dijitali, ambazo ni Star Media Tanzania Limited (Startimes) yenye ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Star Communications and Technology ya China, Ting ya Agape Associates na Basic Transmissions ya Kampuni za IPP Media pamoja na Sahara Communications.

Kwa kuanzia, TCRA imechagua mikoa saba ambapo imeanza na Mkoa wa Dar es Salaam, huku Dodoma na Tanga ikitarajiwa kuanza Januari 31, Mwanza Februari 28, Moshi na Arusha Machi 31 na Mbeya ni Aprili 30 mwaka huu.

Wakati mikoa mingine ikiendelea kutumia mfumo wa analojia, imeahidiwa ndani ya miezi nane mwaka huu, teknolojia ya dijitali itakuwa imeenea kote.

Lakini siku chache baada ya kuanza kwa mfumo huu mpya jijini Dar es Salaam, tafiti zilizofanywa na TCRA zinaonesha asilimia 90 ya wakazi wake wanatumia mfumo huu.

Mbali ya hilo kumekuwa na malalamiko kwa wakazi wengi wa jiji kuhusu ubora wa huduma za baadhi ya ving’amuzi kuwa havikidhi kiwango kinachotakiwa kulingana na fedha wanazozitoa.

Aidha, wakazi hao wanadai kuwa ving’amuzi hivyo vimekuwa na matatizo ya sauti pamoja na picha hasa kwa wale waliolipia vituo vichache huku wakilalamikia bei za ving’amuzi na vifurushi vyake kuwa kubwa tofauti na vipato vya wengi.

Wakazi hao wanasema kuna mafundi wachache wa kuunganisha ving’amuzi, hivyo ambao pia hawapatikani kiurahisi huku wakisema lugha iliyotumika kutoa maelezo ya jinsi kuunganisha si ya taifa hivyo ni vigumu kwa watu wengi kuelewa.
Wakizungumza na kituo hiki kwa wakati tofauti, wakazi hao wanasema wamekuwa wakipewa namba za watu wa huduma kwa wateja, lakini imekuwa vigumu kuwapata pindi wanapohitaji msaada.
Anitha George, mkazi wa Banana jijini Dar es Salaam anasema mfumo wa dijitali umeleta usumbufu mkubwa sana kwani imekuwa shida kupata matangazo ya televisheni kama zamani.

“Muda mwingi matangazo hayaonekani vizuri huku ukitokea ujumbe wa ‘hakuna huduma’, wakati mwingine matangazo yakiwa yanaendelea picha zikiganda na ikitokea picha ikionekana vizuri basi sauti haitasikika,” anasema Anitha.

Naye Mary Jacob mkazi wa Buguruni, alisema bei za ving’amuzi bado ni tatizo kwa Watanzania walio wengi na kutoa pendekezo kwa serikali kupanga bei stahiki itakayowalinda watu wa hali zote.
“Hizi bei zao hata hazijawalenga wanyonge, kama mtu anashindwa kununua antena ya sh 3,000 (si za ving’amuzi) ataweza kununua king’amuzi cha sh 48,000 kinachohitaji vitu kibao?

“Mimi nadhani serikali ingesimamia hili ili bei iwe hata sh 7,000 watu wanaweza kumudu,” anasema Mary.
Naye Issa Hamad anaeleza kwamba: “Jamani sidhani kama Watanzania wote ni wasomi…nashangaa hivyo vinavyotumika kuelekezea jinsi ya kuunganisha ving’amuzi (menu) vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza.”
Baadhi ya wakazi hao waliitupia lawama serikali kwa kuharakisha kuingia kwenye dijitali wakati mfumo huo ukiwa haujaenea kwenye miji yote nchini na kushangazwa na kila kituo cha televisheni kutangaza king’amuzi chake.

Ving`amuzi vimesaidia kupunguza wimbi la uvivu wa kukesha Tiviini kuangalia maigizo, bongo flavor, wabongo wengi hasa wa uswazi hawawezi kumiliki sh 30000 au 50000 za kununulia ving`amuzi hii ni sawa na kusema Serikali imefanikiwa kupunguza watazama Tv sugu kwa asilimia zaidi ya 40% na haya ndio maendeleo tuyatakayo! Ambokile Msonda

Mwisho.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.