Benki ya
kuhudumia Wananchi wa Kawaida Nchini {
NMB } imekabidhi mchango wa Vikalio 100 kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu
katika Skuli za Sekondari za Donge na Kitope zilizomo ndani ya Wilaya ya
Kasakazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Msaada huo
wa Vikalio wenye gharama ya shilingi za Kitanzania Milioni Kumi utasaidia
kupunguza uhaba wa madeski kwa Skuli hizo za Donge na Kitope ambapo kila Skuli
imefanikiwa kupata madeski 50.
Meneja wa
Tawi la NBC Zanzibar Bwana Bakari Khamis Moh’d alikabidhi msaada huo kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi
pamoja na Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis hafla iliyofanyika
hapo katika skuli ya Sekondari Kitope.
Meneja huyo
wa Tawi la Benki ya NMB Bwana Bakari aliiomba Jamii kuendelea kuiunga mkono
Benki hiyo ili kusaidia kuipa nguvu za kiutendaji itakaoongeza kasi ya kusaidia
harakati za Kijamii Nchini.
Alisema Benki
hiyo tokea kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1997 imekuwa ikijitahidi kuunga mkono
maendeleo ya Wananchi hasa katika miradi iliyomo ndani ya Sekta ya Elimu.
Akitoa
shukrani zake mara baada ya kupokea msaada huo wa vikalio Mbunge wa Jimbo la
Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziomba
Benki nyengine Nchini kuiga mfano wa Benki ya NMB katika kusaidia maendeleo ya
Wananchi.
Balozi Seif
alisema taasisi za Kifedha ndani na nje ya nchi zimekuwa na mfumo maalum
unaosaidia kuunga mkono juhudi za jamii katika maeneo tofauti ya kiuchumi na
ustawi wa jamii.
Alisema
Wananchi hawanabudi kushirikiana na kuzipa nguvu taasisi hiyo ili ziweze
kutekeleza malengo zilizojipangia.
“ Ukweli
halisi NMB ni Benki ya wanyonge. Ni Benki yetu inayolenga kuhudumia wananachi
wa kipato cha chini. Huyu ndie rafiki yetu na tunapaswa kumuunga mkono “.
Alisema Balozi Seif.
Naye Mbunge
wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis
alisema Benki ya NMB imeonyesha umahiri mkubwa katika kutekeleza ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ambayo
imejipangia kuimarisha Sekta ya Elimu iliyo muhimili pekee wa maendeleo ya kiuchumi kwa
Taifa lolote Duniani.
Akisoma
risala ya Walimu na wazazi wa Skuli za Donge na Kitope Mwalimu Mkuu wa Skuli ya
Sekondari ya Kitope Mwalimu Suleiman
Juma Makame ameupongeza Uongozi wa Benki hiyo pamoja na ule wa Jimbo la
Kitope kwa juhudi zao zilizojikita zaidi katika kuimarisha Sekta ya Elimu.
Hata Hivyo
Mwalimu Suleiman alisema zipo changa moto zinazoendelea kuzikabili skuli hiyo
akatolea mfano wa Skuli yake ya Kitope inayokabiliwa na uhaba wa Vifaa vya
Maabara pamoja na uwezekwaji wa jengo moja la Skuli hiyo.
Akitoa salamu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar Afisa Elimu wa Wilaya ya
Kaskazini “B “ Mwalimu Ussi Machano alieleza kwamba mchango wa Mbunge wa Jimbo
la Kitope Balozi Seif katika Sekta ya Elimu umekuwa mfano wa kuigwa na Viongozi
wengine hapa Nchini.
Mwalimu Ussi Machano alisema kwamba mchango huo kwa
kiasi kikubwa umeipunguzia mzigo mkubwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
katika ukamilishaji wa Majengo mbali
mbali ya Skuli yanayoanzishwa na wananchi wenyewe kwa mpango wa kujitolea.
Huu ni
mkupuo wa Pili kwa Benki hiyo ya NMB kusaidia vikalio kwa Skuli za Donge na
Kitope.
Othman
Khamis Ame
Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Kitope waliohudhuria halfa ya kupatiwa vikalio vya skuli za Donge na Kitoe iliyofanyika katika Skuli ya Sekondari ya Kitope |
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akipokea Madeski 50 kwa ajili ya skuli ya Sekondari ya Kitope kutoka kwa Meneja wa Tawi la Benki ya NMB Bwana Bakari Khamis Mohd. |
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya NMB mara baada ya hafla ya makabidhiano ya madeski kwa ajili ya skuli za Donge na Kitope. |
Post a Comment