Na Hudugu Ng'amilo.
Bunge Maalumu la
Katiba linaahirishwa leo baada ya kukutana kwa siku 67 bila kupitisha hata
ibara moja kati ya 240 zilizomo katika Rasimu ya Katiba.
Badala yake Bunge
hilo likiongozwa na Samuel Sitta "Mzee wa Kasi na Viwango"
linaahirishwa hadi Agosti, mwaka huu likiendelea kujadili Sura ya Kwanza na ya
Sita zenye jumla ya Ibara 19, zinazohusu masuala yanayojenga msingi wa aina ya
Muungano unaopendekezwa.
Tume ya Mabadiliko
ya Katiba katika rasimu iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wake,
Jaji Joseph Warioba ilipendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu,
pendekezo ambalo limeligawa Bunge hilo vipande viwili.
Kutokana na
mgawanyiko huo, kauli zenye utata, kejeli, matusi, dhihaka na ubaguzi ni mambo
yaliyoshika hatamu katika mjadala wa sura hizo mbili, huku viongozi wa Bunge;
Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan wakilaumiwa kwa kushindwa kudhibiti
hali hiyo.
Mwanzoni mwa wiki
hii, Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiah Oluoch alimshutumu Sitta kwamba ameshindwa
kudhibiti nidhamu katika Bunge na kwamba ndiye chanzo cha kuondoka kwa wajumbe
wapatao 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
"Mwenendo wa
Bunge Maalumu ulikuwa na dalili zote za kuonyesha kungetokea matatizo ndani
yake kutokana na mipasho ambayo ilikuwa ikitokea kwa wajumbe pamoja na lugha
ambazo siyo za staha wakati wa kutengeneza kanuni," alisema Oluoch na
kuongeza:
"Kwanza
matumizi ya lugha zisizo na staha, mwenyekiti anaruhusu wajumbe kuchangia hoja
kwa kupeana mipasho bila kujali hoja iliyopo mezani kinyume na kanuni,"
alisema Olouch.
Hata hivyo, Suluhu
alisema amekuwa akiendesha Bunge hilo kwa umakini mkubwa na kwamba kila
anaposikia lugha chafu amekuwa akiwabana wajumbe kwa kuwaamuru kufuta kauli au
kuomba radhi kwa matamshi. "Sipendezwi na lugha chafu, kwa hiyo mojawapo
ya mambo ambayo huwa najitahidi kusikiliza kwa makini kila michango inapotolewa
na wajumbe bungeni ni kubaini kama wametumia lugha zisizostahili, kisha
kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni zetu," alisema Suluhu.
Alikiri kwamba wapo
baadhi ya wajumbe ambao wamekuwa wakigoma au kukataa kuomba radhi na kwamba
masuala yao hupelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo ina mamlaka ya kuchukua
hatua zaidi kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo.
Matakwa ya Kanuni
Sehemu ya Tano ya
Kanuni za Bunge Maalumu inatoa mwongozo wa mambo yanayokatazwa na yale
yanayopaswa kufuatwa wakati wa mjadala.
Kanuni ya 46
imeorodhesha mambo yasiyoruhusiwa ambayo ni pamoja na kusema uongo, kutoa
taarifa zisizokuwa za kweli, kuzungumza jambo lolote ambalo halipo kwenye
mjadala na kutumia majina ya marais na waasisi wa Taifa kwa dhihaka.Pia inazuia
matumizi ya lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au inayodhalilisha watu
wengine, kuzomea, kupiga kelele za aina yoyote zinazoweza kuvuruga mjadala au mwenendo
bora wa shughuli za Bunge hilo.
Licha ya makatazo
hayo, wajumbe wamekuwa wakikiuka kanuni bila kuchukuliwa hatua na hali hiyo
imekuwa chanzo cha mivutano, zomeazomea, kelele na mambo mengine hadi kundi la
Ukawa kususia kikao wakieleza kutokuridhishwa na mwenendo wa Bunge.
Kuufyata na
kuufyatua
Baadhi ya kauli
tata zilizojitokeza ni pamoja na ile iliyotolewa na Asha Bakari Makame kwa
mjumbe mwenzake, Ismail Jussa kuwa anafanana na watu wenye mabusha nyuma ambao
ndiyo huufyata.
Makame ambaye pia
ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), alikwenda mbali zaidi
na kumwambia Jussa kuwa ana matatizo ya kiafya na si mwanamume kamili, kwani
ameshindwa kuoa na hana watoto wakati ana umri mkubwa.
"Huyu Jussa
anasema kwamba tumeufyata, hapa tuwekane sawa, maana ya kuufyata ni mtu kuwa na
mabusha pale yanapokuwa nyuma ndiyo kuufyata kwa hiyo yeye ndiyo ameufyata, ana
busha huyu," alisema Bakari.
Naye Profesa
Ibrahim Lipumba alichafua hali ya hewa pale alipowafananisha wajumbe wa Bunge
Maalumu na kundi la mauaji nchini Rwanda, Intarahamwe.
"Tumechoka
kusikiliza matusi. "Tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka
ubaguzi hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Intarahamwe linalohamasisha ubaguzi
ndani ya Tanzania hili hatulikubali. Tunawaachia, watu wote tunaotaka Katiba ya
wananchi tunawaachia Intarahamwe mwendelee na Bunge lenu."
Mjumbe mwingine ni
Mwanakhamis Kassim Said aliyesema: "Mimi nilikuwa namwomba baba yangu
mdogo Seif (Maalim Seif Sharif Hamad) awarejeshe watu wake humu (bungeni) kwa
sababu mpira unachezwa huku ndani. Hatutakii mema humu, tena ana choyo na
husuda. Namwomba baba mdogo atuache, alichokitaka amekipata, king'ora
anazunguka saa 24 Dar es Salaam, Unguja. Mheshimiwa Mwenyekiti Baba mdogo kila
mara yuko kwenye pipa (ndege) mara Uingereza, mara Canada mara wapi? Hicho
ndicho anachokitaka amekipata."
Mjumbe mwingine,
Mohamed Seif Khatibu alisema: "Nimejifunza kuwa baadhi ya wanasiasa wa
upinzani ni vinyonga. Lakini Maalim Seif ni kinyonga, wakipita kwenye mvua
wanakuwa na rangi ya mvua, kwenye jua wanakuwa na rangi ya jua, baharini
wanakuwa na rangi ya bahari."
Tuhuma za rushwa
Mjumbe Ezekiah
Wenje alisema baadhi ya mawaziri wamewahonga wajumbe wa kundi la 201 ili waunge
mkono msimamo wao, lakini alipotakiwa kufuta kauli hiyo alikataa na suala lake
kufikishwa kwenye kamati ya kanuni.Kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa
waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku, wengine walikwenda
kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa
bahasha."
Kuingia msituni
Kapteni John Komba
alitangaza kuingia msituni iwapo Bunge Maalumu la Katiba litapitisha muundo wa
serikali tatu, huku akimshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba na timu yake ni waasi kama Adamu na Eva waliomuasi Mungu
kutokana na kile walichokifanya cha kupendekeza serikali tatu. Mwingine katika
orodha ni Bernard Membe aliyesema, Tume ya Mzee Warioba itakuja kukumbukwa kwa
kuratibu mauaji ya Muungano na Bunge nalo litakuja kulaaniwa kwa kubariki
mauaji hayo.
Watoto wa shetani
Mjumbe Paul Makonda
alisema: "Shetani alikuja duniani kuiharibu dunia, kuiangamiza na
kuteketeza kila kilichostahili kuungana... watoto wake ni Mheshimiwa Jussa,
watoto wake ni Mheshimiwa Mbowe, watoto wake ni Mheshimiwa Lipumba... Hawa ni
watoto wa shetani".
Mwingine: Waride
Bakari Jabu alisema: "Chiku Abwao mimi namshangaa sana anayesema bora
Muungano uvunjike lakini Tanganyika iwepo. Tunafahamu asili yake mwenyewe ni
Mkongo mumewe ndiye Mtanganyika, namwambia Muungano huu utakuwepo na utaendelea
kuwapo."
Mjumbe Tundu Lissu
alisema: "Tanganyika haikuuawa na makubaliano ya Muungano, bali iliuawa
kwa amri za Nyerere.... Mwalimu Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote ya kikatiba ya
kutunga amri na kuua Tanganyika."
Imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema,
Sharon Sauwa na Beatrice Moses
CHANZO MWANANCHI
chanzo cha habari hii na mtandao wa www.mjengwablog.com
Post a Comment