Asasi zaidi ya 500 zaunga mkono rasimu ya pili ya Jaji Warioba
KAULI
ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa ufunguzi wa Bunge la Katiba na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William
Lukuvi kwamba muundo wa serikali tatu utatoa mwanya kwa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) kuchukua nchi ni vitisho dhidi ya maoni ya wananchi wanaotaka
serikali tatu.
Akizungumza
na Makangale Satellite blog Tanzania hivi karibuni jijini Dar es Salaam muda
mfupi baada ya mkutano wa waandishi wa habari uliondaliwa na Asasi za Kiraia
kuhusu mwenendo wa mchakato wa kutunga katiba Mpya, Mkurugenzi Mtendaji wa
Youths Partnership Countywide (YPC), Israel Ilunde amesema kwamba kauli ya Rais
Kikwete wakati wa uzinduzi wa Bunge la Katiba ni kutisha wananchi dhidi ya
maoni yao kuhusu serikali tatu.
“kimsingi
baada ya Rais kutoa maoni yake kwamba serikali tatu itatoa nafasi kwa jeshi
kuchukua nchi ni kutisha wananchi wa Tanzania dhidi ya maoni yao ambayo yapo
kwenye rasimu ya pili iliyowasilishwa na jaji warioba,” amesema
Ilunde
amesema kwamba si kweli kwamba muundo wa serikali tatu italifanya jeshi la
wananchi wa Tanzania kuchukua madaraka bali ilikuwa mbinu ya Rais kikwete
kutisha na kuwatia hofu wananchi ambao wanataka serikali tatu.
Aliongeza
kwamba Waziri Lukuvi aliongeza chumvi kwenye mkutano na baadhi ya viongozi wa
dini kwamba serikali tatu itakuwa rahisi kwa JWTZ kuchukua nchi wakati kimsingi
ni upotoshaji mkubwa.
“viongozi
wakuu wa serikali wamewatisha wajumbe wa bunge maalum la katiba na wananchi kwa
ujumla kuhusu swala la serikali tatu ni kinyume kabisa na katiba ya mwaka
1977,” alisisitiza
Kwa
upande wake, Mratibu wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo
Olengurumwa amesema kwamba Bunge la katiba linatumia mamlaka yake vibaya kwa
kutaka kuhodhi kila kitu.
“Tume
ya Jaji warioba imefanya kazi nzuri ya kuandika rasimu na bunge maalum ya
katiba na kuijadili na kuibariki tu rasimu ili iende kwa wananchi na si
kubadilisha rasimu yenye maoni ya wananchi,” amesema
Amesema
kwamba bunge la katiba halina mamlaka ya kisheria kubadili rasimu ya pili
iliyotengenezwa na Tume ya warioba kwa sababu ni kinyume na matakwa ya
kisheria.
Awali,
Mwenyekiti wa Umoja wa AZAKI wa kutetea Rasimu ya wananchi, Irinei Kiria
amesema kwamba asasi za kiraia zaidi ya 500 wanaunga mkono rasimu ya pili ya
katiba mpya kwa kuwa imekidhi mahitaji ya watanzania.
“kwamba
hatujafurahishwa na mijadala ndani ya bunge maalum la kutunga katiba mijadala
ambayo imepoteza utaifa na badala yake imejikita kwenye kutoheshiminiana,
ubabe, ubaguzi, vijembe na vitisho,” aliongeza
Amesema asasi za kiraia wamehuzunishwa na
tabia ya kudhihaki na kudharau rasimu ya pili pamoja na Tume ya Mabadiliko ya
katiba pamoja na Mwenyekiti wake.
Mwisho
Post a Comment