HOTUBA YA MHESHIMIWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA HOSPITALI YA CHUO KIKUU CHA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI MUHIMBILI, KAMPASI YA MLOGANZILA, TAREHE 24 APRILI 2014

Mheshimiwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini;
Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam,
Professa Ephata Kaaya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili.
Viongozi na Watendaji wa Serikali,
Viongozi na Wanajumuia wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;



Shukrani
Awali ya yote, napenda kukushukuru Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kunialika kuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya kisasa ya kufundishia na kutolea huduma katika eneo hili la Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Afya Sayansi Shirikishi Muhimbili, Mloganzila. Leo ni siku ya aina yake katika historia ya Chuo Kikuu cha Muhimbili na taifa kwa jumla. Kitendo hiki cha leo kinaashiria kuanza rasmi kwa kazi ya ujenzi wa Kampasi mpya ya Mloganzila ya MUHAS na ni kubwa katika uboreshaji wa huduma ya afya nchini. Shughuli hii kufanyika leo kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wetu ni jambo stahiki kabisa. Ujenzi huu ni moja ya kielelezo thabiti cha juhudi na mafanikio ya Serikali yetu, katika kuwapatia Watanzania huduma bora zaidi za afya.


Hali ya Sekta ya Afya Wakati Tunaungana
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Utoaji wa huduma bora za afya ni wajibu wa msingi wa Serikali yetu na uhai wa taifa letu. Wakati tulipoungana tarehe 26 Aprili, 1964, hali ya huduma ya afya ilikuwa duni na afya ya wananchi wetu haikuwa ya kuridhisha. Kulikuwa na hospitali chache mno, halikadhalika, vituo vya afya na zahanati zilikuwa chache sana. Iliwalazimu wananchi kutembea umbali mrefu sana kutafuta huduma za afya. Katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba vilikuwa haba na duni. Wataalamu wa fani mbalimbali za afya walikuwa wachache sana. Watu walikuwa wanakufa siku si zao kwa maradhi yanayoweza kuzuilika na kutibika. Umri wa wastani wa kuishi ulikuwa miaka 35. Kwa ajili hiyo, Serikali zetu zilitangaza maradhi kuwa moja ya maadui watatu wakubwa, wengine wakiwemo umaskini na ujinga. 


Katika kipindi cha miaka 50 ya muungano, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimepambana na adui maradhi kwa nguvu kubwa. Tumetoa kipaumbele cha juu katika kupanua na kuboresha huduma za afya. Hii imejidhihirisha kwa sera na mikakati mbalimbali ya afya inayotekelezwa, ukubwa wa bajeti za afya zinazotengwa, idadi ya miradi inayotekelezwa na matokeo mazuri yanayopatikana kutokana na juhudi hizo za Serikali. 


Mafanikio ya Miaka 50 ya Muungano katika Sekta ya Afya


Ndugu Wananchi;
Jitihada zilizofanyika katika miaka 50 iliyopita zimewezesha kuongezeka kwa zahanati, vituo vya afya na hospitali, vifaa vya uchunguzi, vifaa tiba na wataalamu wa kada mbalimbali za afya. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya Watanzania wanaopata huduma bora za afya katika ngazi zote imeongezeka sana na ushindi dhidi ya maradhi mengi unaonekana. Uwezo wetu wa kupambana magonjwa yanayoua watu wengi nchini umefikia mahali pazuri, na ule wa kuchunguza na kutibu maradhi yanayotulazimu kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi unaendelea kuimarika. Kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa watoto na akina mama wajawazito yamepungua kwa asilimia 50, na kule Zanzibar maambukizi ya malaria ni asilimia 0.3. Maambukizi ya UKIMWI yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 1986 hadi kufikia asilimia 5.1 hivi sasa. 


Tunaendelea kuimarisha vituo vya kutoa huduma ya afya kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na taifa kwa majengo, vifaa tiba, vifaa vya uchunguzi na wataalamu. Katika ngazi ya taifa kwa mfano, tumepiga hatua ya kutia moyo kwa maradhi ya moyo, figo, saratani, mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu. Kwa upande wa maradhi ya moyo tumejenga kituo cha tiba na mafunzo ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye vitanda 100. Kituo hiki kinawezesha wagonjwa wa moyo wengi kupata matibabu hapa hapa nchini badala ya kupelekwa nje. Katika kipindi cha mwaka mmoja cha ufanyaji kazi wake, kituo hiki kimeweza kufanyia upasuaji wagonjwa 347, kuwawekea mashine za kuongeza nguvu kwenye moyo (pacemaker) wagonjwa 3 na mwaka huu wameanza uwekaji wa vyuma vidogo (stent) katika mishipa ya damu ya moyo ambayo imebana. Haya ni mafanikio makubwa na ya kutia moyo.
Kwa upande wa figo, hivi sasa tunatoa huduma za magonjwa ya figo katika Hospitali ya Muhimbili, Hospitali ya Kanda, Mbeya na Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Pale Chuo kikuu cha Dodoma pia tunajenga kituo kikubwa kitakachobobea kwenye maradhi ya figo. Lengo letu ni kwamba, kitakapokamilika chuo hiki kiweze kufanya matibabu ya kubadilisha figo (kidney transplant). 


Aidha, tumeboresha taasisi ya saratani ya Ocean Road kwa mejengo, vifaa na wataalamu. Tumeongeza maradufu uwezo wa taasisi hiyo kulaza wagonjwa kutoka wagonjwa 120 mwaka 2011 hadi wagonjwa 290 hivi sasa. Halikadhalika, tumenunua mashine mpya kwa ajili ya uchunguzi na tumeongeza wataalamu waliobobea wa magonjwa ya saratani. Vilevile, tunakamilisha ujenzi wa jengo la Taasisi ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu. Litakapokamilika tutaliwekea vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba ili kuongeza uwezo wetu wa kukabiliana na maradhi haya.
Ujenzi wa Hospitali ya Kufundishia ya Kampasi ya Mlonganzila


Ndugu Wananchi;

Jiwe la msingi tunaloweka leo, ni mwendelezo wa juhudi hizi za Serikali za kupambana na adui maradhi. Hospitali hii itakuwa na vitanda 600, itakuwa na vifaa tiba vya kisasa kabisa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mishipa ya fahamu. Ujenzi wa Hospitali ya Kampasi hii utasaidia sana kupunguza msongamano kwenye hospitali ya rufaa ya Taifa ya Muhimbili na za rufaa zilizopo nchini, ambazo hutoa huduma za utaalamu wa juu. Aidha, itasaidia kupunguza ulazima wa kupeleka wagonjwa nchi za nje kwa ajili ya matibabu. Matibabu nje ya nchi ni gharama kubwa kwa Serikali, lakini pia fursa zenyewe ni chache na wengi wengi hawapati nafasi ya kupelekwa nje kwa matibabu. Hivyo ujenzi wa hospitali hii ya Chuo Kikuu cha Muhimbili ni ishara ya wazi ya dhamira ya serikali katika kukabiliana na tatizo hili.

Hatua Zilizochukuliwa na Serikali Katika Ujenzi wa Kampasi na Hospitali ya Kufundishia


Ndugu Wananchi;

Baada ya Chuo Kikuu cha Muhimbili kutafuta eneo la kupanua huduma zake, mwaka 2006 nilifanya uamuzi wa kuwapatia eneo hili lenye ukubwa wa ekari 3,800 kwa ajili ya kujenga Kampasi mpya na hospitali ya kisasa ya kufundishia na kutolea huduma. Tulianza kutafuta fedha za ujenzi wa hospitali ya kufundishia, tukafanikiwa kupata mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini wenye thamani ya dola za Marekani milioni 76.5. Mkopo huo ungetosheleza kujenga jengo la hospitali hiyo pamoja na vifaa vya kisasa vya kutosheleza mahitaji ya hospitali.
Ujenzi haukuweza kuanza kwa wakati kutokana na mgogoro wa ardhi uliokuwepo katika eneo hili. Matokeo ya ucheleweshaji huo umepandisha gharama za ujenzi kwa dola za Marekani milioni 18. Maana yake ni kuwa fedha za mkopo tulizopata hazitoshi tena kukamilisha jengo hilo na kununulia vifaa kama ilivyokusudiwa. Viongozi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili waliponijia nilikubali bila kusita kwamba Serikali itaongeza hizo dola milioni 18 zinazohitajika. Niwahakikishie kuwa tutatoa fedha hizo ili ujenzi ukamilika kwa kiwango kilichotarajiwa.


Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ni mategeneo ya Serikali kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kampasi hii, Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili kitakuwa na uwezo wa kuongeza udahili wa wanafunzi wa fani mbalimbali za afya kutoka takribani wanafunzi 3,000 na kufikia wanafunzi 15,000. Hii itapunguza kwa kaisi kikubwa, kama si kumaliza kabisa uhaba mkubwa wa wataalam wa fani za afya ulioko nchini kwa sasa. Aidha, ni mategemeo yangu pia kuwa wakati ujenzi utakapokamilika idadi ya wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu itaongezeka kwa kiasi kikubwa na hivyo kuongeza idadi ya wataalamu waliobobea wa fani mbalimbali za afya.


Hitimisho
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;


Kwa kumalizia, napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa kutupatia mkopo wa ujenzi na vifaa vya hospitali hii. Mkopo uliotolewa ni mkopo wenye riba nafuu ambao kama usingepatikana ingebidi tutumie fedha iliyopangwa kwa ajili ya miradi mingine kwenye ujenzi wa hospitali hii. Napenda kuwashukuru wananchi wa maeneo ya Kwembe na Mloganzila kwa kutoa ushirikiano katika mradi huu. Mradi huu ni moja ya kielelezo cha mafanikio ya Muungano wetu wa Miaka 50, tuutunze utakapokamilika ili utufae kwa miaka 50 mingine. Nawatakieni kila la heri katika kusherehekea miaka 50 ya Muungano wetu.
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.