Hoja hii ya
Muungano, imekuwa na umuhimu wa kipekee na hii ndiyo sababu katika ufunguzi wa
Bunge hilo, Rais Jakaya Kikwete alitumia zaidi ya saa moja kuizungumzia.
Salum Rashid |
Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wakati akiwasilisha Rasimu
ya Pili bungeni, pia alitumia zaidi ya saa moja kuzungumzia mambo yanayohusu
muungano.
Kutokana na mvutano
huu, gazeti hili limefanya mahojiano maalumu na aliyekuwa Katibu wa Baraza la
Mapinduzi mwaka 1964, Salum Rashid ili kupata ufafanuzi wake juu ya jambo hilo
hasa baada ya Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa kueleza anayojua
kuhusu suala hilo.
Swali: Salum Rashid
(72) wewe ndiye ulikuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi mwaka 1964. Je,
unauzungumzia vipi Muungano?
Jibu: Muungano ni
jambo bora, tumekuwa nao kwa miaka 50 sasa lakini una changamoto nyingi ambazo
baadhi tangu ulipoanza tuliziona.
Swali: Ni
changamoto zipi hizo ambazo tangu mwanzo, zilionekana?
Jibu: Kuna mengi,
lakini kikubwa ilikuwa ni usiri wa jambo hili, kwani mimi kama Katibu wa Baraza
la Mapinduzi sikujua ila hili la Zanzibar kumezwa tangu wakati huo lilionekana.
Swali: Je, kidogo
una ufahamu ilipo Hati ya Muungano? Kuna ambao wanasema ipo Umoja wa Mataifa,
wewe unasemaje kwani ulikuwa kiongozi wa Serikali wakati huo?
Jibu:
Ninachokumbuka ni kwamba hati haikupelekwa Umoja wa Mataifa (UN), bali
kilichopelekwa ni taarifa ya ya kuungana Tanganyika na Zanzibar.
Swali: Katika Bunge
linaloendelea sasa kuna mijadala mingi imeibuka kuhusiana na hati ya sheria ya
Zanzibar kuridhia Muungano je, una taarifa gani juu ya hati hii?
Jibu: Hati ya
Sheria ya Zanzibar Presidential Decree kukubali Muungano, hiyo haipo na wala
wasihangaike kuitafuta.
Swali: Kuna hati ya
sheria namba 22 ya mwaka 1964, ilisainiwa kwa upande wa Tanganyika na Rais wa
Tanganyika wakati huo, Hayati Julius Nyerere, Katibu wa Bunge Pius Msekwa na
Spika wa Bunge hilo, Adam Sapi Mkwawa, Aprili 25 mwaka 1964. Je, kwa upande wa
Zanzibar hamkupata hati hii?
Jibu: Mimi
kama Katibu wa Baraza sijawahi kuiona hiyo Sheria (Presidential Decree) ambayo
ilipaswa kusainiwa na Rais wa Zanzibar hayati Abeid Karume na mimi.
Mimi ndiye nilikuwa
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Baraza halikuwahi kuridhia Muungano,
kilichofanyika ni kupewa taarifa tu .
Alifafanua kuwa
ilipaswa sheria hiyo, kupelekwa rasmi katika Baraza la Mapinduzi na Baraza la
Mawaziri lakini haikuwahi kufanyika hivyo.
Swali: Je, unadhani
ni kwa nini sheria hii haijasainiwa na wewe?
Jibu: Unajua haya
mambo yalikuwa siri sana na kuna mambo mengi yanapotoshwa kuhusu muungano..
Swali: Je, hujawahi
kuona Hati ya Muungano na wewe ulikuwa kiongozi mkubwa wa serikali wakati huo?
Jibu: Mimi niliona
ile draft (rasimu) ya kwanza ya muungano na nilipoiona nikiwa na hayati Karume
nilimshauri vitu vingi na tulirekebisha na baadaye ilirudi Dar es Salaam.
Swali: Je, baada ya
kukamilika uliwahi kuiona tena?
Jibu: Hapana,
sijaiona nilikuwapo Zanzibar wakati huo, lakini jambo hili baadaye lilifanywa
siri kubwa sana, Nyerere hakutaka mtu yeyote ajue na upande wetu Zanzibar
hatukupata ushauri wa kisheria hata Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alikuwa hana
taarifa, lakini Tanganyika walikuwa na ushauri wa kisheria.
Swali: Sasa baada
ya Miaka 50 ya Muungano, nini maoni yako?
Jibu: Mimi nawataka
wajumbe waachane na haya mambo ya hati kwani yamepita na kwa kuwa sote
tunautaka Muungano ni muhimu tu kuuboresha.
Swali: Je, unadhani
muundo upi unafaa?
Jibu: Mimi ni
muumini wa Muungano wa Mkataba, lakini kutokana na mapendekezo mazuri ya Tume
ya Jaji Warioba naamini muundo wa Serikali tatu ndiyo mwafaka.
Swali: Lakini kuna
hofu ya muungano wa Serikali tatu utavunja Muungano wewe huoni hofu hiyo
itatimia.
Jibu: Hakuna sababu
ya kuwa na hofu yoyote ya kuvunjika Muungano, kama ambavyo inaelezwa na baadhi
ya wanasiasa kwani Muungano wetu siyo wa wanasiasa au Serikali, ni watu. Hapa
Zanzibar kuna watu kutoka maeneo mbalimbali ya bara na huko bara wapo
Wazanzibar sasa muungano huu hauwezi kuvunjika kirahisi.
Hao wanadhani
Tanganyika itakuja kuwa na nguvu zaidi na hivyo kuja kuathiri Muungano hilo
haliwezi kutokea kutokana na Muundo uliopendekezwa na Tume ya Warioba.
Swali: Chama Cha
Mapinduzi (CCM), wamekuwa wakipendekeza serikali mbili nini maoni yako.
Jibu: Binafsi najua
hasa huku Zanzibar watu hawataki serikali mbili na kama ikilazimishwa na
mwakani ni uchaguzi CCM inaweza kupata shida sana kwani asilimia 60 wa
Wazanzibariwanataka serikali tatu.
Chanzo cha habari na gazeti la kila siku la mwananachi 13/04/2014
Post a Comment