Meneja
huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na jukumu la kupanga bei za mafuta za kila
mwezi, alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili; Ijumaa na Jumamosi
iliyopita kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa
nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme vijijini
(Rea) na fedha za mfuko wa barabara.
Jeshi
la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa meneja huyo
alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo
Vituka wilayani Temeke.
Nyumbani
kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na waombolezaji waliokuwa kwenye vikundi na
kikao cha maandalizi ya mazishi kilifanyika ndani ya nyumba ya marehemu iliyopo
Yombo Vituka na baadaye kuhamia nyumba ya jirani.
Kamati
ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge,
ilikutana na maofisa wa Ewura, akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta
kilichostahili kutozwa kodi.
Gashaza
alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura kwenye kamati hiyo ya Bunge
akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo, takwimu za Ewura ziliashiria
kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini
Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu za mamlaka ya mapato.
Habari
hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es Salaam juzi majira ya saa tatu usiku,
Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo
karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawaeleza
kuwa anahisi kutishiwa maisha yake.
Baadaye
walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.
Inadaiwa
kuwa marehemu aliomba akalale hotelini kwa sababu hakuona kama ana amani kulala
nyumbani kwake na ilipofika asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’ ndani ya chumba
alicholala hotelini humo.
Nyumbani
kwa marehemu waombolezaji walikusanyika katika makundi, lakini baada ya kukaa
katika kikao cha familia walitoka na kauli moja kuwa hawatasema chochote na
kwamba jukumu hilo libaki mikononi kwa polisi.
Kamanda wa polisi wa
Kanda ya Dar es Salaam, Seleiman Kova hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo
akidai kuwa anayetakiwa kulizungumzia ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke,
Engbert Kiondo.
Alipotafutwa,
Kamanda Kiondo alisema kulingana na taarifa zilizopo Gashaza aliitwa bungeni
Mei 14 na akarejea Dar es Salaam Mei 17. Alisema aliporejea, Gashaza aliaga
nyumbani kwake kuwa hajisikii vizuri na kuelekea Hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo
Yombo ambako alichukua chumba Namba 113.
Kamanda
Kiondo alisema akiwa hotelini, Gashaza alimpigia simu rafiki yake mmoja
anayejulikana kwa moja la Silipwango akimweleza kuwa yupo hotelini hapo
kujipumzisha kwa sababu bungeni aliulizwa mambo ambayo hayakumpendeza na kwamba
alihitaji kupumzika.
Rafiki
huyo, kwa mujibu wa Kiondo, alimpigia simu mkewe anayeitwa Judith akamweleza
alivyoelezwa na mumewe na baadaye kwa pamoja wakamfuata hotelini ambako baada
ya kuzungumza nao kwa muda mfupi, aliwaomba wamuache apumzike na ndipo
walipoondoka.
Asubuhi,
Silipwango alipigiwa simu na mkewe kumueleza kuwa Gashaza hakurudi nyumbani na
akaamua kupitia kwenye hoteli waliyomuacha na alipofika akakuta watu wamejaa.
Alipouliza akaelezwa kuwa kuna mtu amejinyonga chumbani.
Kamanda
Kiondo alisema Gashaza alijinyonga kwa kutumia tai aliyoifunga kwenye bomba la
maji ambalo pia lilikatika na hivyo kuukuta mwili wake ukiwa sakafuni.
Kilichojiri
kamati ya bajeti
“Kisheria
kodi ya mafuta ni Sh263 kwa lita inakwenda mfuko mkuu Hazina na Sh50 inakwenda
kwa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), lakini takwimu za mafuta yaliyouzwa
inayostahili kutozwa kodi kati ya TRA na Ewura zinatofautiana,” alisema mmoja
wa wajumbe.
“Kwa
hiyo Kamati ya Bajeti iliwaita wote (Ewura na TRA) na kwa kweli wajumbe wa
kamati tulikuwa wakali sana, hatutaki mchezo tulitaka kujua nani anasema
ukweli,” alidokeza mjumbe huyo.
“Uko
ugomvi mkubwa tu kati ya TRA na Ewura kuhusu nani hasa mwenye takwimu halisi,”
alisema mjumbe huyo na kudokeza kuwa meneja huyo alisema kila kitu kwa uwazi.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa baada ya vuta nikuvute ndani ya
kamati hiyo, iliamuliwa watendaji wa vyombo hivyo viwili wakafanye ulinganisho
na kupeleka jibu kwa kamati hiyo. Ewura waliwasilisha takwimu zao Jumamosi.
“Tension
(mvutano) ni kubwa kwa sababu kuna watu wizarani hawazitaki takwimu za Ewura na
wanataka za TRA ambazo sisi kama wajumbe tunaziona hazina uhalisia kunaweza kukawa
na ufisadi,” alisisitiza mjumbe mwingine.
Chenge
azungumza
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alipoulizwa jana, alikiri kufanyika
kwa kikao kilichomuhusisha meneja huyo na kwamba taarifa alizotoa zilionekana
tofauti na zile za TRA.
“TRA
ni chombo cha Serikali na Ewura ni chombo cha Serikali, kwanini wawe na takwimu
zinazotofautiana? Hilo tu ndio tumewaagiza wakae pamoja watuambie zipi ni
takwimu halisi,” alisema Chenge.
Alipoelezwa
kuwa mmoja kati ya maofisa wa Ewura waliofika mbele ya kamati yake amejinyonga,
Chenge alionyesha kushtushwa na kuhoji kama taarifa hizo zina ukweli.
“Una
uhakika kwamba amejinyonga? lini? Kama ni kweli basi ni jambo la kusikitisha
sana, lakini hiyo sasa ni kazi ya polisi. Mimi nisingependa sana kuzungumza,
tuwaachie wao wachunguze sababu za kifo chake,” alisema Chenge.
Serikali
inaelezwa kuwa katika hali mbaya kifedha na kamati hiyo ya Bajeti imekuwa
ikifanya kila linalowezekana kuinusuru kwa kukutana karibu kila siku na Hazina
na wadau wengine wanaochangia fedha katika mfuko wake.
Kwa
bajeti ya mwaka 2013/2014 iliyopitishwa na Bunge, Serikali imejikuta ikiwa na
upungufu wa Sh1.8 trilioni hali ambayo kamati ya bajeti inatafuta kila njia
ikiwamo kushauri vyanzo vipya vya mapato ili kunusuru bajeti ya mwaka huu wa
2014/2015.
Bajeti
ambazo zinaelezwa kuiumiza kichwa Serikali ni ya Maji, Miundombinu na Nishati
na Madini ambazo zinaelezwa kupata mgawo kidogo mwaka jana na kuzifanya
zishindwe kutekeleza miradi mbalimbali.
Mkurugenzi
wa Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alisema alipata taarifa jana saa 3:00
asubuhi.
Alithibitisha
kuwa marehemu alikuwa Dodoma kikazi kwenye vikao na kamati ya Bunge tangu
Alhamisi iliyopita.
Baada
ya kumaliza kazi ndiyo ndiyo jana (juzi) alichelewa sana kurudi ndipo alipoamua
kujipumzisha kwenye nyumba ya wageni (iliyopo karibu na nyumbani kwake) ambako
alikutwa amefariki,” alisema Samwel.
Alisema
marehemu alikuwa mwadilifu, mchapa kazi na asiye na tatizo lolote kazini na
kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa.
Post a Comment