Na Deodatus Balile
Siri nzito zimeanza kuvuja jinsi Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mzee
Madeni Kipande (58), anavyofanya unyanyasaji kwa wafanyakazi wa Bandari
hiyo, hasa wanawake, vyanzo vimeifahamisha JAMHURI.
Pia,
wafanyakazi waliozungumza na JAMHURI (majina yanahifadhiwa kwa sababu za
wazi), wamesema katika viambaza vya Bandari hiyo sasa wanamuona Kipande
kama aliyekuwa kiongozi wa taifa la Uganda dikteta Idi Amin Dada.
“Chini
kwa chini wafanyakazi wamembatiza jina IDI AMIN, na wengi wanarejea
filamu ya ‘Last Kingo of Scotland’ inayoigiza udikteta aliokuwa akifanya
Idi Amin, wanasema Kipande naye amejielekeza katika mlengo
huo. Sasa Gawile [Kaimu Mkurugenzi wa Utumishi] amekuwa kama Kapteni
Yamungu ambaye Idi Amin alikuwa anamwelekeza amkamate na kumuua nani kwa
muda gani.
“Kipande amesema kwenye mkutano wa uongozi kuwa
yeyote ambaye anapingana naye atamng’oa. Taarifa tulizonazo amesema
yeyote asiyekubaliana na afanyacho yeye [Kipande] bila kujali hoja
anayotoa aandikiwe barua ya kuondolewa kazini. Anasema itakayolipa fidia
ni Serikali na si Bandari hivyo hajali,” kilisema chanzo chetu.
Katika
mkondo huo, mwishoni mwa mwezi uliopita Kipande alianzisha mchakato wa
kumsimamisha kazi Meneja wa Bandari ya Tanga, Hassan Kyomile. Habari za
uhakika zilizoifikia JAMHURI, zimesema Kipande aliagiza Kyomile
asimamishwe kazi kwa maelezo kwamba mwandishi wa habari hizi [Balile] ni
Mhaya na Kyomile aliyeomba kazi ya Ukurugenzi Mkuu TPA ni Mhaya, hivyo
anaamini Kyomile ndiye anayevujisha siri za TPA kwa JAMHURI.
Kipande
alimshusha cheo Kyomile mwezi Machi, mwaka huu kutoka Ukurugenzi wa
Ununuzi na kumfanya Meneja wa Bandari ya Tanga, lakini kadiri joto la
habari nzito zinazohusu madudu yake Bandari kupitia gazeti hili JAMHURI
linaloanzia wanapoishia wengine linavyozidi, sasa anapanga kumsimamisha
kazi. Ikumbukwe, Kyomile alijaza fomu kuomba nafasi ya Ukurugenzi Mkuu
wa TPA mwaka jana, nafasi ambayo Kipande anaamini yeye kama Kaimu
Mkurugenzi ndiye anayestahili kuijaza na hivyo ni kosa ‘nafasi yake’
kuombwa na mtu yeyote.
Aliagiza nafasi ya Kyomile na Franciscas
Muindi ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko wa TPA zitangazwe na kujazwa mara
moja kwa kuwa walikuwa wameomba kazi ya Ukurugenzi Mkuu anayoikaimu.
Nakala ya barua ya maelekezo yake, ambayo JAMHURI inayo, ilipingwa
vikali na Bodi ya Wakurugenzi waliomwambia si kosa mtu yeyote ndani ya
TPA kuomba nafasi yoyote ya kazi ilimradhi awe na sifa. Hata hivyo, hadi
Jumapili (Mei 4), Kyomile alikuwa hajakabidhiwa barua ya kusimamishwa
kazi, ambayo JAMHURI imehakikishiwa na vyanzo vyake kuwa imeandikwa siku
10 zilizopita.
Kwa upande wake Mama Muindi, aliyejaza fomu ya
kuwania nafasi hiyo mwaka jana, Kipande amemsimamisha kazi kwa tuhuma
kuwa anavujisha siri (madudu ya) za TPA kwenye vyombo vya habari. Hata
hivyo, hadi leo si TPA wala Kipande waliojitokeza kukanusha kwa
vielelezo tuhuma nyingi zinazohusiana na utendaji mbovu wa kiongozi
huyo, ikiwamo kuhatarisha usalama wa Bandari kwa kutokuwapo CCTV camera
na mita za kupima mafuta yanayoingia nchini kutofanya kazi kwa miaka
mitatu sasa.
Orodha ya wafanyakazi aliowaonea Kipande ambayo sasa
inachunguzwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ni
pamoja na Vulfrida Teye. Huyu kwa cheo chake ni Meneja wa Masuala ya
Bodi ya Wakurugenzi.
Mama huyu alisimamishwa kazi na Kipande
Agosti 2013 kwa tuhuma za kuondoa kipengele cha kununua vipuri vya SPM
na mtu aliyewauzia Bandari Boya. Hajahojiwa na wala kurudishwa kazini.
Tuhuma zake zinaelezwa kuwa za uonevu kwani yeye si aliyekuwa na mamlaka
ya kuihitimisha mkataba husika. Anaendelea kupokea mshahara na
marupurupu mengine bila kufanya kazi hadi sasa na wala hajahojiwa na
vyombo stahiki.
Mfanyakazi mwingine Ndugu Msemo, aliyekuwa Afisa
Ununuzi, naye alisimamishwa kazi Agosti 2013 kwa tuhuma sawa na za Teye.
Anaendelea kulipwa mshahara, na Kipande ameshindwa kuthibitisha tuhuma
dhidi yake, lakini anaapa kuwa milele hatarudishwa kazini wakati yeye
akiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu au Mkurugenzi Mkuu, ikiwa atabarikiwa kupewa
nafasi hiyo. Msemo hajahojiwa na uongozi kwa tuhuma hizi.
Isaac
Godson amehamishiwa Kigoma. Huyu ni Afisa Ununuzi Mwandamizi ambaye kwa
cheo chake hakustahili kuhamia kwenye bandari ndogo kama Kigoma.
Erasto
Lugenge ni Mwanasheria Mwandamizi wa TPA, ambaye Kipande ameagiza
asimamishwe kazi, lakini hajui ni tuhuma zipi amwandikie kama mashtaka
ya kusimamishwa kwake kazi. Bado analipwa mshahara na marupurupu bila
kuwa kazini.
Mwingine ni Mama Nyirabu, alisimamishwa mwaka 2012,
Eng. Mhayaya alikuwa Mhandisi Mwandamizi na Marcelina Kisanko Mhando.
Huyu alisimamishwa kazi Desemba, 2012 lakini baada ya JAMHURI kuchapisha
tuhuma hewa alizosimamishwa nazo na jinsi Kipande alivyokuwa anakiuka
maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kumrejesha kazini, kwa shinikizo
amemrejesha kazini. Lakini pamoja na kwamba ni Meneja Mifumo wa TEHAMA,
mpango unasukwa kumhamishia mikoani. Awali Kipande alikuwa ameapa kuwa
huyu asingerejea kazini wakati wa uhai wake.
Eng. Johnson
Mutalemwa alikuwa Meneja wa Bandari Mwanza aliyesimamishwa kazi tangu
mwaka 2013, lakini hadi leo kama wengine analipwa mshahara na mashitaka
yake hayapo -- ni hewa. Kilichobainika ni chuki binafsi za Kipande dhidi
ya kabila la watu kama Mutalemwa.
Mwingine ni Kulwa Masaga, huyu
alikuwa Karani wa ICT, amesimamishwa muda mrefu, lakini hatimaye baada
ya shinikizo la gazeti JAMHURI, Aprili mwaka huu amemrejesha kazini.
Joseph
Singano alikuwa Mkuu wa Ulinzi Bandari ya Mwanza, lakini taarifa
ilizopata JAMHURI, zinaonesha barua ya kusimamishwa kazi ya Singano,
inaonesha kuwa alizembea kusimamia ushuru wa mizigo Bandari Mwanza,
wakati hilo ni suala la uhasibu kitu kisichokuwa sehemu ya kazi yake.
Lucas Magomola wa Mwanza na Kassimu Mori wote wamesimamishwa miaka
miwili iliyopita.
Cha kushangaza ni maelezo ya mdomo aliyotoa
Kipande wakati anawasimamisha watumishi hawa wa Bandari ya Mwanza kuwa
Mwanza ilikuwa wanajiendesha kwa hasara, hivyo ikamlazimu awasimamishe
kazi lakini anaendelea kuwalipa mishahara kwa miaka miwili sasa.
Hajawafungulia mashtaka wala nini.
Waliohamishwa kwa tuhuma hewa
Henry
Arika, aliyekuwa Meneja Biashara wa Bandari ya Dar es Salaam,
alihamishiwa Makao Makuu na kuambiwa kuripoti Idara ya Utawala tangu
April 2013 hadi leo hii. Analipwa mshahara na marupurupu yake bila
kufanya kazi kwa mwaka mmoja sasa, kwa sababu Kipande hamtaki.
Sasa
anajulikana kama “freelance manager”. Alituhumiwa kupokea rushwa
kutoka kwa Mohammed Enterprises kiasi cha sh milioni 100 baada ya kuwa
ameruhusu kuondolewa makontena bandarini yaliyokuwa yameweka msongamano
mkubwa na kupunguza nafasi ya kushushia mizigo.
Arika aliruhusu
makontena 70 baada ya kushauriana na Kaimu Meneja wa Bandari wakati huo,
Mama Mosha, na hivyo kukubaliana kuruhusu makontena 70 ya sukari kati
ya 100, ili 30 yabaki kama dhamana iwapo Mohammed Enterprises
wangeshindwa kulipa.
“Huu ni utaratibu wa kibiashara uliozoeleka,
na lengo ni kusaidia wateja waendelee na biashara zao, na wakati huo
huo TPA isipate hasara. Hata Kipande anafanya hivyo hivyo kwa sasa.
SUMATRA walichunguza sakata hili na kubaini kuwa Arika hakuwa na kosa,
ila Kipande ameapa kuwa hampangii kazi ataendelea kuripoti kwa
Mkurugenzi wa Utumishi na kurejea nyumbani kila siku.
“Hana meza,
kiti wala ofisi. Anaripoti na kuondoka. Ni udhalilishaji wa hali ya juu
kwa mtu aliyekuwa Meneja leo anatendewa kama kinyangarika. Inauma
sana,” alisema mtoa habari wetu.
Kakusa, aliyekuwa Meneja wa
Bandari Mtwara, alihamishiwa Bandari ya Kyela. Baadaye uamuzi
ukabatilishwa na Bodi, kwa kuwa cheo chake kilikuwa kikubwa, na hii
ingelikuwa kama kumshusha cheo. Alikaa bila kazi yoyote tangu April
2013 na kuwajibika kuripoti makao makuu hadi alipostaafu mwishoni mwa
mwaka jana. Alituhumiwa na Kipande bila ushahidi kuwa alikuwa anauza
kinyemela ardhi ya TPA Mtwara kwa wawekezaji.
Aliyekuwa Mkuu wa
Bandari ya Kigoma, Nandi, naye yalimkuta. Alihamishiwa makao makuu bila
kazi yoyote na kuwajibika kuripoti Utumishi hadi alipostaafu mwanzoni
mwa mwaka huu. Alituhumiwa na Kipande kuwa alikuwa anakula rushwa
kutoka kwa kampuni ya MUAPI iliyokuwa ina zabuni ya kuendesha Bandari ya
Kigoma wakati huo, na sasa haipo tena.
Beatrice Jairo
alihamishiwa Bandari Ndogo ya Nansio, Ukerewe nje ya Ikama. Alikuwa
Afisa Mawasiliano Makao Makuu na hivi sasa kasimamishwa kazi bila
mshahara eti alitoroka kazini (abscond). Alichukua ruhusa ya dharura, na
alipoomba kuongeza ikacheleweshwa, na Kipande akasema ni mtoro kazini.
Levina
Msia alihamishiwa Bandari Ndogo ya Kasanga nje ya Ikama. Alikuwa Afisa
Mawasiliano Mwandamizi Makao Makuu na hivi sasa kasimamishwa kazi bila
mshahara eti alitoroka kazini (abscond), kwa kuwa alikuja Dar es Salaam
kwa rufaa kutibiwa Muhimbili. Kipande anasema kwa nini hakupelekwa
Mbeya.
Francisca Muindi, Mkurugenzi wa Masoko; anachukiwa na
Kipande kwa kutaka kuchukua “nafasi yake” ya CEO kwa vile aliiomba kazi
hiyo ilipotangazwa. Kipande amemsimamisha kazi Aprili mwaka huu na
anafanya uchunguzi wa tuhuma kuwa ana hujuma alizofanya kwa TPA bila
kuzitaja.
Makatibu Muhtasi, Ms Rabia Mahfudhi , Zuhura Maganga,
Mwantumu Ngoda na Michael Mganga anawahamisha ofisi moja hadi nyingine
kila habari zinapochapishwa kwenye gazeti lolote, akiwatuhumu bila
ushahidi kuwa ndiyo wanaovujisha siri za ofisi.
Wanawake waliokumbana na manyanyaso ya Kipande
Wanawake
walioorodheshwa hapa chini, wamepata kunyanyaswa na Kipande kwa nyakati
tofauti, ila kutokana na ufinyu wa nafasi leo tunaorodhesha majina yao
tu na nafasi zao. Apolonia Mosha (Meneja Bandari Msaidizi, Dar es
Salaam), Francisca Muindi (Mkurugenzi wa Masoko), Kokutulage Kazaura
(Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria), Adelaide Lukaija (Meneja
Ununuzi) – huyu kaomba kustaafu mapema, Janet Ngowi (Meneja TEHAMA),
Vulfrida Teye (Meneja wa Mambo ya Bodi), Marcelina Kisanko (Mhando) na
Winnie Mulindwa ambaye alistaafu kama Meneja Bandari Msaidizi, Dar es
Salaam (Utekelezaji).
Ajira za upendeleo
Kama kuna
mgogoro unaofuka moshi ndani ya Bandari basi ni huu unaotokana na ajira
za Mhandisi Alois Matei, ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu (Maendeleo ya
Miundombinu) na Mhandisi William Shilla, ambaye ni Mkurugenzi wa
Uhandisi. Taarifa zilizopo bandarini ni kuwa wahandisi hawa wawili
waliajiriwa na Kipande kupitia mlango wa nyuma. Hawakushiriki mchakato
wa usaili bali waliletwa na kupewa barua za ajira. JAMHURI bado
inakamilisha orodha ya wafanyakazi wa aina hii walioajiriwa katika
Kurugenzi ya Sheria bila kufuata mkondo sahihi pia.
Wanawake wasio watumishi wa Bandari aliowadhalilisha
Ukiacha
wafanyakazi wa Bandari, Kipande amekuwa hana staha hata kwa wafanyakazi
wanaofika ofisini kwake bila kuwa watumishi wa Bandari. Prediganda
Assenga, ambaye ni Meneja Biashara wa TICTS, alionja joto ya jiwe la
Kipande.
Mwaka juzi Prediganda alifika ofisini kwa Kipande
akifuatana na bosi wake mpya, yaani Mtendaji Mkuu wa TICTS, kwa minajili
ya utambulisho, yakamkuta. “Mara tu alipomuona, Kipande alitamka kwa
jazba na hasira mbele ya Mtendaji Mkuu wa TICTS kuwa Prediganda aondoke
ofisini kwake, kwa kuwa anafahamu ni mwizi mkubwa na alimtaka huyo bosi
wake aliyefuatana naye, amfukuze kazi mara moja pamoja na mameneja wote
weusi hapo TICTS. Mama huyu ni mwaminifu haijapata kutokea. Kila
aliyekuwapo alishangaa Kipande kwa nini alifyatuka hivyo.
“Mgeni
huyo alimsihi Kipande kumruhusu Prediganda afanye utambulisho, naye
alikubali kwa sharti kuwa asioongee lolote. Isingelikuwa busara za
Mtendaji Mkuu wa TICTS, bila shaka pangelichimbika,” kilisema chanzo
chetu.
Pia Kipande alimdhalilisha Rukia Shamte ambaye ni Mtendaji
Mkuu wa “Central Corridor Transit Transport Facilitation Agency”. Mara
kadhaa amekuwa akimdhalilisha mbele ya watu kila mara. Kipande
anamtuhumu kiongozi huyo wa kike, tena mwenye sifa na uzoefu uliotukuka
katika sekta ya usafirishaji hapa nchini na hata nje ya nchi; kuwa ni
“mdandiaji wa mambo” yasiyomhusu.
Fikra hizi potofu zilijengwa na
Kipande kwa sababu hakutaka kuthamini mchango wa Rukia na wala kupata
ushauri wake. Ilifikia hatua Kipande kumtuhumu Rukia kwa maandishi
kwamba anamwamuru kazi wakati si bosi wake!
Je, unafahamu hatua
wanazotaka kuchukua wafanyakazi baada ya ahadi aliyowapa Waziri
Mwakyembe, kutokana na ushauri potofu na wa uongo wa Kipande kuwa
wangelipwa bonasi? Usiikose JAMHURI, wiki ijayo.
Kipande, Mwakyembe watumia milioni 360
Katika
hatua nyingine, habari za uhakika kutoka TPA zinasema Kipande,
Mwakyembe na wabunge kadhaa wametumia dola 200,000 (Sh milioni 364) kwa
wiki moja katika ziara ya kufungua ofisi ya biashara ya TPA mjini
Lubumbashi, DRC.
Ziara hii, Kipande ameifanya wakati siku za
nyuma alikuwa akipinga ziara za kuitangaza TPA akidai ni wizi. Nakala za
maandishi ya Kipande kwenda Idara ya Masoko siku za nyuma, zilikuwa
zikielekeza kuwa kwenda kuitangaza Bandari Zambia au kufungua ofisi ni
kupoteza mapato na wizi wa wazi.
“Bandari ya Dar es Salaam Zambia
wanaifahamu tangu enzi za Mwalimu Nyerere, hivyo hakuna sababu ya
kukutana na wafanyabiashara kuitangaza,” aliandika Kipande katika moja
ya madokezo kupinga mipango ya kuhamaisha watumiaji wa bandari.
Wabunge
wawili, ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu, Zainabu Madabida na
Peter Serukamba, walishiriki ziara hiyo iliyoteketeza mamilioni ya
shilingi. Zipo tuhuma pia kuwa baadhi ya wajumbe katika safari hiyo
wamelipwa posho mara mbili. Wamelipwa kwenye vituo vyao vya kazi, na
Bandari imewalipia pia.
Chanzo cha habari na mtandao wa www.wavuti.com
Post a Comment