Dodoma. Mbunge machachari wa Mwibara, Alphaxard
Kangi Lugola, amedai kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo
yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii.
Lugola ambaye katika Bunge lililopita aliwaongoza
wabunge wenzake kuichachafya Serikali hadi mawaziri wanne kujiuzulu
nyadhifa zao, jana aligeuka tena mwiba kwa Serikali ya CCM.
“Hakuna lolote humu ni blabla tu… Mheshimiwa Zambi wewe ulikuwa ‘backbencher’ (kiti cha nyuma) kama mimi ulikuwa unapiga muziki kama kasuku juu ya wizara hii, leo unashirikiana na waziri wako unakuja na vitu ambavyo havina majibu, maana yake nini?”.PICHA|MAKTABA |
Akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika, Lugola alisema anashangaa Waziri mwenye dhamana, Christopher
Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blabla.
Pia alimgeukia naibu wa wizara hiyo, Godfrey Zambi
na kumwambia kuwa amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma
bungeni akipaza sauti, lakini baada ya kupata madaraka amewageuka na
kushirikiana na waziri.
Akichangia kwa hisia kali, Lugola alihoji
inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za
umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki ofisini
kama Waziri.
“Waziri huyuhuyu ndiye anayezindua mbegu aina ya
Chutoni ambayo haioti, bado ni Waziri. Waziri huyu huyu analipa ruzuku
mbegu ya pamba isiyoota bado ni Waziri,” alisema Lugola.
Lugola alihoji kama Mchina aliyekuwa akijenga
daraja la Kilombero alijiua kwa sababu tu ya kuhofia kupigwa risasi
atakaporudi kwao, hata Waziri Chizza alipaswa awe ameiacha kazi hiyo.
“Simshauri waziri ajiue, lakini kwa vitendo vyote
hivi waziri huyu angekuwa ameacha wizara hii na kupumzika na kufanya
kazi nyingine mbadala,” alisema Lugola huku akipigiwa makofi.
Lugola alikumbushia Chizza alikuwa ni miongoni mwa
mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo na kusema mambo yanayofanywa na
wizara hiyo yatakigharimu Chama Cha Mapinduzi.
Mbunge huyo alibainisha kuwa, katika hotuba yake
mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Serikali iko kwenye
mchakato wa kuanzisha mfuko wa kinga ya pamba ili kuwasaidia wakulima.
Hata hivyo, alisema katika hotuba ya Waziri Mkuu
juzi, hakuna sehemu aliyozungumzia mfuko huo wala Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika katika hotuba yake ya mwaka huu, naye hajazungumzia
mfuko huo.
“Hivi nchi hii tunaiendesha kwa usanii mpaka lini?
Usanii juu ya usanii… Hatuwezi kuwadanganya wananchi kwa kiwango hiki.
Itakuwaje mimi mbunge niunge mkono bajeti ya namna hii?” alihoji.
Alimgeukia Zambi na kumweleza kuwa aliwahi kumtahadharisha kuwa
atakapokuja na bajeti yake ahakikishe anampa majibu ya asilimia 20 ya
malipo waliyoahidiwa wakulima waliotumia mbegu ya chutoni.
“Uniambie asilimia 20 ya malipo ya wakulima ambayo
waliahidiwa kwamba wakitumia chutoni walipwe kama sehemu ya malipo yao,
lakini hili halimo kwenye bajeti,” alisema na kuongeza:
“Hakuna lolote humu ni blabla tu… Mheshimiwa Zambi
wewe ulikuwa ‘backbencher’ (kiti cha nyuma) kama mimi ulikuwa unapiga
muziki kama kasuku juu ya wizara hii, leo unashirikiana na waziri wako
unakuja na vitu ambavyo havina majibu, maana yake nini?”
Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema
wakati Zambi akiwa mbunge, alikuwa msitari wa mbele kupinga matumizi ya
mbolea ya minjingu na kumtaka aeleze kama bado ana msimamo huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Magharibi, John
Shibuda (Chadema), aliwashukia wakuu wa mikoa ya Simiyu na Geita kuwa ni
chanzo cha tatizo kwa wakulima wa pamba.
Mbali na hilo, amemtaka Balozi wa Uingereza nchini
ajitokeze kueleza misaada inayotolewa na nchi yake inavyotumiwa kwenye
sekta ya pamba kwani imekuwa ni sehemu ya ubabaishaji kwa kuendeshwa
semina zisizo na maana.
Shibuda alitoa kauli hiyo jana alipokuwa
akichangia maoni kwenye hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2014/15.
Aliwatuhumu wakuu hao kuwa walimpeleka Waziri Mkuu
katika kampuni ya Kiotoni wakamdanganya kuwa mbegu hizo ni nzuri,
lakini kumbe hazikuwa zimefanyiwa utafiti wa kina na kuwasababishia
hasara kubwa wakulima.
Shibuda alisema mbegu za kiotoni zina udhalimu
mkubwa na hazina tija yoyote kwa wakulima lakini kila siku wakuu wa
mikoa na wilaya wanazipigia debe licha ya kuwa wanatambua kwamba
wakulima wanaumizwa.
Magdalena Sakaya aliifananisha Serikali kuwa ni
sawa na sikio la kufa kwa kuwa kila wakati imeshindwa kuwa na majibu ya
ukombozi kwa wakulima wa Tanzania ambao ndio wapigakura wao.
Mbunge wa Kasulu, Moses Machali (NCCR-Mageuzi)
aliwapongeza wabunge wa CCM wanaoonyesha ujasiri wa kuisema Serikali yao
kuwa inaendesha mambo kisanii na hivyo kushindwa kuwaletea wananchi
maendeleo.
“Serikali imekuwa ikidanganya katika kutatua
matatizo ya wananchi ndiyo maana tunaona ni Serikali ya maigizo… Ukisoma
hotuba ya bajeti hapa haijibu matatizo ya wananchi,” alisema.
Wakati wabunge hao wakiiponda bajeti hiyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni imeitaka Serikali, kueleza ni lini na vipi wakulima
walioathirika na mbegu feki watafidiwa.
Msemaji wa Kambi hiyo wa Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika, Rose Kamili, alisema tayari wakulima wameshapata hasara na
bado wako wanaoendelea kuathirika na tatizo la mbegu kutoota.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema, Habel Chidawali na Fidelis Butahe
Chanzo cha habari hii na gazeti la kila siku la mwananchi
Chanzo cha habari hii na gazeti la kila siku la mwananchi
Post a Comment