Dodoma. Meno ya tembo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya vielelezo mahakamani yalitoweka katika Kituo cha Polisi cha Kilwa mkoani Lindi.
Polisi akilinda sehemu ya shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa Dar es Salaam hivi karibuni. Picha ya Maktaba |
Tukio hilo limenukuliwa katika Ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikisema meno makubwa 108 ya
tembo na kilo 20 za meno mengine ya tembo yaliyokuwa yamehifadhiwa kama
kielelezo cha kesi za uhujumu uchumi, yamebainika kutoweka kinyemela.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni juzi,
imebainisha kuwa meno mengine makubwa ya tembo yaliyokuwa na uzito wa
kilo 498.3 yamebadilishwa kinyemela na meno madogo, hivyo kusababisha
hasara ya kilo 203.66 za meno ya tembo ambazo thamani yake
haikufahamika.
CAG Ludovick Utouh katika ripoti hiyo ya mwaka
ulioishia Juni 30, 2013, amebainisha kuwa kumbukumbu katika Pori Tengefu
la Miguruwe zilionyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Juni 5 hadi
Juni 8, 2012 meno makubwa 108 yalikuwa miongoni mwa vielelezo kituoni
hapo.
Kati ya meno hayo 108 yaliyokamatwa katika matukio
ya ujangili, 74 yalitoweka katika kituo cha polisi wakati 34
yalibadilishwa na meno madogo, tofauti na yale yaliyokuwa yamekamatwa
yakihusishwa na kesi ya ujangili Na. 3/2009 na kesi nyingine ya uhujumu
uchumi Na. 2/2010 ambazo zilikuwa zikiendelea mahakamani mkoani Lindi.
Pia ilibainika kuwa kilo 20 za meno ya tembo
ambayo yalikamatwa na kuhifadhiwa kama kielelezo cha majalada
KLM/IR/184/2009, KLM/IR/235/2009 na KLM/IR/567/2010 yalitoweka.
Gari la ujangili latoweka
Ukaguzi huo pia ulibaini kuwa gari lililokamatwa
likiwa kielelezo baada ya kukutwa na kilo 26 za meno ya tembo yenye
thamani ya Sh135 milioni liliondolewa kinyemela katika Kituo cha Polisi
Kilwa.
CAG katika ukaguzi huo alibaini upungufu katika
usimamizi wa meno ya tembo na nyara nyingine za taifa katika chumba cha
meno hayo Dar es Salaam na vituo vya mikoani.
CAG katika taarifa yake hiyo amesema kutokana na
kukosekana kwa kumbukumbu sahihi, meno ya tembo yanaweza kuibwa au
kupotea bila menejimenti kuwa na taarifa yoyote, hivyo ameishauri
Serikali kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa kutosha katika usimamizi wa
nyara za Serikali nchi nzima.
Chanzo cha habari na gazeti la kila siku www.mwananchi.co.uk
Chanzo cha habari na gazeti la kila siku www.mwananchi.co.uk
Post a Comment