MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI
BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO), MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU
(MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2014/2015
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka
huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefikisha umri wa nusu karne tangu
ilipozaliwa tarehe 26 Aprili, 1964. Kama anavyosema Waziri Mkuu Mh.
Mizengo Pinda katika hotuba yake ya tarehe 7 Mei, 2014 'Kuhusu Mapitio
na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya
Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2014/2015': "Miaka 50
kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi." Waziri Mkuu ametumia takwimu
za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinazoonyesha kwamba asilimia
90.6 ya Watanzania wote "wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi
wanayoifahamu ni
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania." Kwa maneno
ya Waziri Mkuu, "sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa
kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu."
Mheshimiwa Spika,
Kama
ilivyo kwa Watanzania wengine wengi, na mimi pia nimezaliwa ndani ya
Muungano. Ninaamini kwamba ukweli huu unawahusu pia waheshimiwa wabunge
wengi waliomo ndani ya Bunge hili tukufu. Na sisi pia tunaomba kutendewa
haki kuhusu Muungano huu. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, haki
tunayoomba
kutendewa ni moja tu: kuambiwa ukweli juu ya Muungano huu na historia
yake, hali yake ya sasa na mwelekeo wake wa baadaye. Haki tunayoomba
kutendewa ni kwa watawala kuacha propaganda na uongo juu ya Muungano na
kutuambia ukweli wote juu ya Muungano huu.
Bob
Marley, aliyekuwa mwanamuziki mpigania uhuru wa watu weusi maarufu
kutoka Jamaica, aliwahi kusema katika wimbo wake 'Get Up, Stand UP,
Stand Up For Your Rights' ('Amkeni, Simameni, Simameni kwa Haki Zenu')
kwamba: "You can fool some people some time, but you cannot fool all the
people all the time", yaani, unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa
muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote! Baada
ya nusu karne ya uongo na propaganda kuhusu Muungano huu,
Watanzania wa kizazi hiki cha Muungano wanataka ukweli.
Na
Watanzania hawa hawataulinda, wala kuuimarisha au kuudumisha Muungano
huu endapo wataendelea kudanganywa au kufichwa ukweli juu ya mambo mengi
yanayouhusu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, sisi kizazi cha Muungano
tunahitaji kutendewa haki: acheni propaganda na uongo kuhusu Muungano
huu ndipo muweze kutuambia tuulinde, tuuimarishe na tuudumishe!
SHEREHE ZA MUUNGANO NA 'WAASISI' WA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Sherehe
za Miaka 50 ya Muungano ni mahali pazuri pa kuanzia kudai ukweli juu ya
Muungano huu. Mtu yeyote anayetembea sasa katika Barabara ya Nyerere
kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere hadi
katikati ya jiji la Dar es Salaam; au Barabara ya Ali Hassan Mwinyi
kuanzia Morocco hadi katikati ya jiji, ataona kila mlingoti wa taa za
barabarani umepambwa kwa picha za Waasisi rasmi wa
Muungano,
yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume,
wakiwa katika matukio mbali mbali ya siku za mwanzo za Muungano. Picha
hizo za Waasisi hao pia zimepambwa karibu kila mahali katika barabara za
katikati ya Eneo Kuu la Kibiashara (CBD) la Jiji la Dar es Salaam.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, barabara zote kuu za
Mji wa Zanzibar, ikiwamo ile inayotoka Mji Mkongwe kupitia Ikulu ya
Zanzibar hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, hakuna
picha hata moja ya Waasisi wa Muungano katika matukio yanayoonyeshwa
kwenye picha zilizoko Dar es Salaam. Badala yake, barabara hizo
zimepambwa kwa picha za Marais wa Zanzibar toka Mapinduzi ya mwaka 1964
hadi wa sasa. Ni ndani ya eneo la wageni maarufu (VIP) pekee ndio kuna
picha moja ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Hii ni katika wiki
ambayo Muungano huu umeadhimisha miaka hamsini tangu kuzaliwa kwake!
Kwa
jinsi ambavyo tangu mwaka huu uanze Watanzania tumepigwa propaganda za
kila aina juu ya Muungano na TBC na vyombo vingine vya habari vya
serikali na vya binafsi, kukosekana kwa dalili yoyote ya sherehe za
Muungano kwa upande wa Zanzibar wakati wa kilele cha sherehe hizo
kunatilia shaka juu ya uimara wa misingi ya Muungano wenyewe. Hii ndio
kusema kwamba pengine kuna ukweli katika hitimisho la Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwamba Tanganyika ndiyo imevaa koti la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Na pengine ndio maana Muungano huu haujawahi kuungwa mkono
Zanzibar kwa kiasi ambacho wanaopenda kutuaminisha vinginevyo wamekuwa
wakidai. Aidha, pengine ndio maana hata picha za kuchanganya udongo
zinazoonyeshwa na TBC kila kukicha zinamwonyesha Mwalimu Nyerere
akichanganya udongo peke yake, wakati Sheikh Karume haonekani kabisa!
Mheshimiwa Spika,
Kuna
jambo lingine linalofikirisha sana kuhusu picha hizi za Sherehe za
Miaka Hamsini ya Muungano zilizopamba mitaa ya Dar es Salaam. Baadhi ya
picha hizo zinawaonyesha watu wengine ambao wamefutwa kabisa katika
historia rasmi wanayofundishwa watoto wetu mashuleni na vyuoni.
Hivyo,
kwa mfano, katika picha maarufu ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume
wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano wapo pia, kwa upande wa
Tanganyika, Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa
upande wa Zanzibar wanaoonekana kwenye picha hiyo ni Abdallah Kassim
Hanga,
Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo. Aidha, kuna picha inayowaonyesha
Mwalimu Nyerere, Sheikh Karume na Kassim Hanga wakitabasamu kwa furaha
kubwa.
Katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni,
Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia kilichochapishwa mwaka
2010, Harith Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo Oscar Kambona, Abdallah
Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida walitoa mchango
mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, na
baadaye kufanikisha Muungano na Tanganyika wa Aprili 26 ya mwaka huo.
Katika kitabu chake The Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar:
Miaka 30 ya Dhoruba, Rais wa Pili wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe ameeleza kwamba ni Kambona, Bhoke
Munanka na Job Lusinde ndio waliompelekea Sheikh Karume nakala za Hati
ya Makubaliano ya Muungano kabla ya Hati hizo kusainiwa tarehe 22
Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Swali
kuu ambalo sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa
ukweli kabisa ni 'waasisi' hawa wengine wa Muungano, akina Abdallah
Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla Akida kwa upande wa
Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde kwa upande wa
Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia rasmi
ya Muungano na waasisi wake? Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye
Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala
alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa
mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona
alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi
wakati wa Mapinduzi
ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa Muungano; Bhoke Munanka
alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya masuala ya
usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
Katika
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo
akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi
katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi
Ussi na Jaha Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu
inayoitwa Kama, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha
Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi
wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja.
Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa walishtakiwa katika mahakama
gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka kuambiwa ukweli
kwanini mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa muda wote
wa nusu karne ya Muungano huu.
Kuhusu Oscar
Kambona, inafahamika kwamba katika miaka ya mwisho ya ukoloni na miaka
ya mwanzo ya uhuru, 'mwasisi' huyu wa Muungano alikuwa mtu wa karibu
sana wa Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa 'Best Man' wa
Kambona wakati wa harusi yake iliyofanyika London, Uingereza mwaka 1960.
Inafahamika, hata hivyo, kwamba mwaka 1967 Oscar Kambona alikosana na
Mwalimu Nyerere na akalazimika kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza
alikoishi hadi aliporudi nyumbani wakati wa kurudishwa tena kwa mfumo wa
vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
Tuliosoma
miaka ya sabini na ya themanini tulifundishwa mashuleni na kuimbishwa
nyimbo zilizotuaminisha kwamba Oscar Kambona alikuwa msaliti aliyetaka
kuipindua Serikali yetu tukufu. Hata hivyo, hatukuwahi kuambiwa kama
alishtakiwa katika mahakama yoyote ya hapa nchini na, kama ni hivyo,
kama alipatikana na hatia yoyote na kuadhibiwa na mahakama. Tunachojua
ni kwamba aliporudi nyumbani mwaka 1992, Mzee Kambona hakukamatwa wala
kushtakiwa kwa kosa lolote lile.
Sisi tuliozaliwa ndani ya
Muungano huu tunataka tutendewe haki kwa kuambiwa ukweli juu ya tuhuma
za usaliti dhidi ya Mzee Oscar Kambona ambaye sasa anaandikiwa vitabu
kuwa ni mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kuzaliwa kwa
Muungano huu.
KUTOLEWA KWA NYARAKA ZA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika
maoni yake wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha 2012/2013, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kwamba Serikali iweke wazi
"nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya
Muungano wetu na
'mapito' yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea
yanayouhusu. Hii ni muhimu zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba mataifa ya
magharibi kama vile Marekani na Uingereza
yalikwishatoa
hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za
Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika
katika kuzaliwa kwa Muungano."
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni ilifafanua kwamba "kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika
mamlaka mbali mbali za Serikali kutasaidia kuthibitisha au kukanusha
taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za
kidiplomasia na
kijasusi za nchi hizo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ulitokana na njama za kibeberu za kudhibiti ushawishi wa siasa za
kimapinduzi za Chama cha Umma na viongozi wake ndani ya Baraza la
Mapinduzi Zanzibar la wakati huo. Aidha, nyaraka hizo zitatoa mwanga juu
ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama hicho ambao bila uwepo
wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano
inabaki pungufu."
Aidha, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni ilisisitiza juu ya haja ya taifa letu kuambiwa ukweli
juu ya Muungano huu: "... Miaka karibu hamsini ya Muungano ni umri wa
kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake
na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho." Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni ilirudia wito wake huo wakati wa kuwasilisha maoni yake
juu ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka jana.
Mheshimiwa Spika,
Mjadala
juu ya nyaraka za Muungano huu ulichukua picha mpya wakati wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba walipohoji uwepo wa Hati ya Makubaliano ya
Muungano na uhalali wa Muungano wenyewe wakati wa mjadala juu ya Sura ya
Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Baada ya wajumbe walio wachache
wa Kamati Namba Nne kuonyesha ushahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar haijawahi kuwa na nakala ya Hati hiyo, na kwamba haijawahi
kupelekwa na kusajiliwa katika Sekretarieti
ya Umoja wa Mataifa, Serikali hii ya CCM ililazimika kutoa kile ilichokiita nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano.
Hatuhitaji
kuzungumzia tofauti kubwa ya sahihi ya Sheikh Karume iliyoko kwenye
Hati hiyo na sahihi ya Sheikh Karume iliyoko katika Sheria mbali mbali
alizosaini kama Rais wa Zanzibar na wakati mwingine
kama kaimu
Rais wa Jamhuri ya Muungano. Cha muhimu ni kwamba mgogoro juu ya Hati
ya Makubaliano ya Muungano unathibitisha ukweli kwamba matokeo ya
utamaduni huu wa kufichaficha nyaraka muhimu za nchi ni kwa wananchi
kukosa imani na serikali iliyoko madarakani, kwa kuwa
wananchi wanajenga hisia kwamba nyaraka hizo zinafichwa kwa sababu zina ushahidi wa maovu yaliyofanywa na serikali hiyo.
Kwa
sababu hizi zote, kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa nyaraka za Muungano huu
hadharani ili Watanzania waweze kuelewa historia halisi ya Muungano
badala kuendelea kulishwa propaganda na TBC na kwenye majukwaa ya
kisiasa ya CCM na Serikali yake! Vinginevyo, chochote kitakachosemwa na
TBC na watawala katika majukwa yao ya kisiasa kuhusu Muungano huu
hakitaaminika tena na wananchi wa Tanzania.
KIELELEZO CHA UMOJA NA MSHIKAMANO AU UNYONYAJI WA KIKOLONI?
Mheshimiwa Spika,
Katika
hotuba ya Waziri Mkuu Bunge lako tukufu limeambiwa kwamba "Muungano huu
ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni kielelezo
kamili cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi...." Ni
kweli kwamba Muungano huu ni wa kipekee kwa sababu haujawahi kuigwa na
nchi nyingine zozote katika Afrika. Na kama Muungano huu ungekuwa wa
'kupigiwa mfano duniani kote', kama inavyodaiwa na Waziri Mkuu, basi
kungekuwa na angalau nchi moja iliyoomba kujiunga katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Angalau kungekuwa na nchi zilizoiga mfano wa
Muungano huu kwingineko Afrika na duniani kote.
Kwa
kuwa hakuna nchi hata moja iliyowahi kuomba kujiunga nasi, na kwa kuwa
hakuna nchi nyingine zilizoiga mfano wa Muungano huu, pengine huu ni
muda muafaka wa kuhoji ukweli wa kauli kwamba Muungano huu 'ni kielelezo
cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi' wa Tanganyika na
Zanzibar. Mzee Pius Msekwa, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Spika Emeritus
wa Bunge hili tukufu, aliwahi kusema katika mada yake Hali ya Muungano
kwa semina iliyofanyika Tanga miaka 20 iliyopita kwamba, muundo wa sasa
wa Muungano huu umepelekea wengi kuamini kwamba Muungano huu ni kiini
macho tu.
Hii ni kwa sababu, chini ya Muungano
huu, Zanzibar ilikabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya
nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu
za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika; na kisha Tanganyika
ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Spika Emeritus Msekwa
aliongeza kwamba kwa jinsi mambo yalivyo sasa, Zanzibar inaonekana kama
vile ni 'invited guest' (mgeni mwalikwa) katika Muungano huu.
Naye
msomi mashuhuri wa Kiafrika, Profesa Ali A. Mazrui katika Makala yake
'Imperialism after the Empire: Lessons from Uganda and Tanzania', yaani
'Ubeberu Baada ya Himaya: Funzo Kutoka Uganda na Tanzania',
iliyochapishwa katika gazeti la Kenya, The Sunday Nation, la Mei 22,
1994, alisema kwa sababu ya Muungano, Zanzibar imepoteza kila kitu chake
muhimu, wakati Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania, huku
ikiwa na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo yake ya
Taifa, wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa Mataifa.
Kama
tunavyoonyesha katika Maoni haya, gharama ya kuyapuuza maneno haya ya
watu hawa wazito imekuwa kubwa kweli kweli, hasa kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Ushahidi
wa nyaraka ambazo zimewasilishwa kwenye Bunge lako tukufu na Serikali
hii ya CCM unaonyesha kwamba Muungano huu ni kielelezo cha unyonyaji na
ukandamizaji mkubwa ambao nchi ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi
kubwa ya Tanganyika. Ni mfano wa jinsi ambavyo nchi
moja kubwa
ya Kiafrika inaweza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya Kiafrika kuwa
koloni lake. Kwa sababu maneno haya yanaweza kupotoshwa na wale ambao
wamefaidika na uhusiano huu wa kikoloni kati ya
Tanganyika na Zanzibar naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo.
Kwa
miaka mingi Zanzibar imelalamika kwamba inapunjwa katika mgawanyo wa
mapato yanayotokana na fedha zinazotolewa na nchi wafadhili na taasisi
za kimataifa kwa Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu ya malalamiko hayo,
mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na
Utawala iliiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba: "Utaratibu wa mgawanyo
wa mapato yanayotokana na fedha zinazotoka kwa wafadhili ni vyema
ukaangaliwa upya kwa Serikali zote mbili yaani SMZ na SMT."
Aidha,
Kamati ilishauri kwamba "Serikali itolee uamuzi mapendekezo ya Tume ya
Pamoja ya Fedha yaliyowasilishwa Serikalini tangu mwaka 2006 na
kuwasilishwa tena mwaka 2010 kuhusu utaratibu wa mgao wa fedha za
Serikali zote mbili."
Serikali hii ya CCM imejibu maagizo haya ya Kamati kama ifuatavyo:
"Serikali
zetu mbili bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na
Tume ya Pamoja ya Fedha. Aidha, kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotoka kwa
wafadhili, upo utaratibu wa mgawanyo wake ambapo, kwa upande wa misaada
na mikopo ya kibajeti isiyokuwa na masharti maalum, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ... hupata gawio la asilimia 4.5."
Mheshimiwa Spika,
Kauli
hii ya Serikali ni ya uongo. Katika maelezo yake mbele ya Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano, aliitaarifu Kamati kwamba "Kwa mwaka wa fedha 2013/14, hadi
kufikia mwezi Machi, 2014 SMZ imepata Gawio la Misaada ya Kibajeti
(General Budget Support - GBS) shilingi 27,190,502,190.97/= kati ya
shilingi 32,627,535,000/= zilizoidhinishwa na Bunge." Hii ndio kusema
kwamba kati ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu kama gawio la
misaada na mikopo ya kibajeti kwa Zanzibar, ni asilimia 83 ndizo
zilizolipwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, hili sio tatizo, kwani kwa mwelekeo wa takwimu
hizi, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, gawio lililoidhinishwa
na Bunge lako tukufu linaweza kuwa limelipwa lote.
Tatizo
kubwa na la msingi ni kwamba gawio lililoidhinishwa na Bunge hili tukufu
sio gawio halali kwa Zanzibar. Hii kwa sababu, kwa mujibu wa Maelezo ya
Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (MB.) Akiwasilisha
Mapendekezo ya Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2014/15
kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya tarehe 30
Aprili, 2014, mapato halisi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
yanayotokana na misaada na mikopo nafuu ya nje ilikuwa shilingi bilioni
1,163 au trilioni 1.163.
Kama Zanzibar
ingepatiwa asilimia 4.5 ya mapato hayo, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa
utaratibu uliowekwa na Serikali hii ya CCM, basi kwa mwaka jana peke
yake, gawio halali la Zanzibar la misaada na
mikopo ya
kibajeti lingekuwa shilingi bilioni 52.335. Badala ya kupatiwa shilingi
bilioni 52.335 ambazo ni fedha zake halali, Zanzibar iliidhinishiwa
shilingi bilioni 32.627 au asilimia 52 ya fedha zake halali. Fedha hizo
ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote za misaada na mikopo ya kibajeti
kwa Jamhuri ya Muungano. Fedha zilizobaki, yaani shilingi trilioni 1.130
au asilimia 97.2 ya fedha zote za misaada ya kibajeti zimetumika na
zitatumika Tanganyika. Kwa ushahidi huu wa nyaraka za Serikali hii ya
CCM, kwa sababu ya Muungano huu, kwa mwaka jana peke yake Zanzibar
iliibiwa shilingi bilioni 25.145 au asilimia
48 ya fedha zake halali za gawio la misaada na mikopo ya kibajeti.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mapendekezo yaliyoletwa kwenye Bunge lako tukufu na Serikali hii ya
CCM, Zanzibar itaibiwa fedha nyingi zaidi kwa mwaka huu wa fedha
2014/15. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, kwa mwaka huu wa fedha, "fedha
zitakazokwenda SMZ zinajumuisha shilingi 21,639,608,000.00 mgao wa
misaada ya kibajeti...." Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Maelezo ya
Waziri wa Fedha, 'misaada na mikopo ya kibajeti' kwa mwaka huu wa fedha
itakuwa shilingi bilioni 992.170. Hii ina maana kwamba kwa mwaka huu wa
fedha, Zanzibar itapata asilimia 2.18 tu ya fedha za misaada na mikopo
ya kibajeti. Hii inaonyesha pia kwamba, kwa mwaka huu, fedha za misaada
na mikopo ya kibajeti ambazo zitabaki na kutumika Tanganyika ni shilingi
bilioni 970.531 au asilimia 97.82 ya fedha hizo.
Kama
Serikali hii ya CCM ingeheshimu utaratibu wake wa asilimia 4.5 ya fedha
hizo kwa Zanzibar, gawio halali la Zanzibar kutokana na fedha za
misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka ujao wa fedha lingekuwa shilingi
bilioni 44.647! Kwa maana hiyo, Serikali hii ya CCM inapendekeza
kuilipa Zanzibar asilimia 48.47 ya fedha zake halali. Endapo Bunge lako
tukufu litapitisha mapendekezo haya kama inavyoombwa na Serikali hii ya
CCM, Zanzibar itaibiwa shilingi bilioni 23 au asilimia 51.53 ya fedha
zake halali kwa mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge
lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa Wazanzibari, kwa nini fedha
halali za Zanzibar kutokana na misaada na mikopo ya
kibajeti
inayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano hazijalipwa kwa mwaka jana wa
fedha. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya
CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa
Wazanzibari, kwa nini inapendekeza kuipatia Zanzibar pungufu ya fedha
zake halali kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka huu wa
fedha.
Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilete mbele ya Bunge lako tukufu
takwimu za fedha zote zilizopokelewa na Serikali kama misaada na mikopo
ya kibajeti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na sehemu ya fedha hizo
zilizolipwa kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho. Takwimu
hizo ni muhimu ili Watanzania, na hasa Wazanzibari, waweze kufahamu kama
Zanzibar imekuwa ikipata sehemu yake halali ya mapato ya Jamhuri ya
Muungano yanayotokana na misaada na mikopo ya kibajeti. Mwisho, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Bunge lako tukufu kuunda Kamati
Teule ya Bunge hili itakayochunguza mgawanyo wa mapato yanayotokana na
misaada na mikopo ya kibajeti kati ya Tanganyika na Zanzibar ili kupata
ukweli juu ya uhalali wa malipo ya mapato hayo kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO ISIYOKUWA YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Misaada
na mikopo ya kibajeti sio eneo pekee ambapo Zanzibar inanyonywa na
Tanganyika kwa sababu ya Muungano huu. Ukweli ni kwamba hali ni mbaya
zaidi kuhusiana na fedha za misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti.
Hapa pia takwimu za Serikali hii ya CCM zinatisha na kusikitisha. Hivyo,
kwa mfano, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, kwa mwaka wa fedha
2013/14 fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha
misaada na mikopo ya Basket Fund na misaada na mikopo ya miradi zilikuwa
shilingi trilioni 2.692 au bilioni 2,692. Fedha hizi zote zilitumika
kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika. Hapa Zanzibar haikupata
kitu chochote!
Maelezo ya Waziri wa Fedha
yanaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2014/15, misaada na mikopo
isiyokuwa ya kibajeti kutoka nje inatazamiwa kuwa shilingi bilioni
2,019.43 au trilioni 2.019. Hizi zote ni fedha zitakazotumika kwa ajili
ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika. Hapa pia Zanzibar haitapata kitu
chochote. Ni muhimu kwa Bunge lako tukufu kukumbuka kwamba, kwa sababu
ya Muungano huu,
Zanzibar imenyang'anywa mamlaka ya kuomba
mikopo au misaada kutoka nje bila kwanza kupata kibali cha Wizara ya
Fedha ya Jamhuri ya Muungano, aka Wizara ya Fedha ya Tanganyika. Sisi
tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka kujua unyonyaji na wizi huu wa
fedha za Wazanzibari utakomeshwa lini. Aidha, sisi tulio kizazi cha
Muungano huu tunataka kuambiwa kama mgawanyo wa aina hii wa mapato
yanayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano ndio kielelezo cha umoja,
mshikamano na upendo
miongoni mwa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar ulioletwa na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Sio
tu kwamba Zanzibar haipati stahili yake ya mapato yanayopatikana kwa
jina la Jamhuri ya Muungano kutoka vyanzo vya nje, bali pia fedha
zinazopatikana kutokana na mambo ya Muungano zinatumika kwa mambo yasiyo
ya Muungano ya Tanganyika. Moja ya matokeo ya mjadala wa katiba
wa
mwaka 1983/84 uliopelekea 'kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar' na kung'olewa madarakani kwa Alhaj Aboud Jumbe ni kuingizwa
kwa Sura ya Saba inayohusu 'Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya
Muungano' katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Kufuatia
kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1984, ibara mpya ya 133 ya Katiba iliweka
masharti kwamba "Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza 'Akaunti ya
Pamoja ya Fedha ... ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na
Serikali mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha ...
kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya
Muungano."
Aidha, ibara ya 134 iliweka masharti
ya kuwa na Tume ya Pamoja ya Fedha yenye majukumu ya "kuchambua mapato
na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya
Muungano na kutoa mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu mchango na mgawo
wa kila mojawapo ya
Serikali hizo." Majukumu mengine ya Tume
hiyo ni "kuchunguza ... mfumo wa shughuli za fedha kwa Jamhuri ya
Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali
mbili."
Mheshimiwa Spika,
Kwa
miaka thelathini tangu kupitishwa kwa Mabadiliko ya Tano ya Katiba,
masuala ya Tume ya Pamoja ya Fedha na Akaunti ya Pamoja ya Fedha
yamekuwa mojawapo ya kile kinachoitwa 'Kero za Muungano' ambayo ufumbuzi
wake umeshindikana. Kwa mfano, licha ya Katiba kuelekeza kuundwa kwa
Tume ya Pamoja ya Fedha, sheria ya kuunda Tume hiyo, yaani Sheria ya
Tume ya Pamoja ya Fedha, ilipitishwa miaka kumi na mbili baadaye, yaani
mwaka 1996.
Baada ya hapo Tume yenyewe iliundwa
rasmi mwaka 2003, yaani miaka saba baada ya kutungwa kwa sheria na
miaka 19 tokea Katiba iweke masharti ya kuundwa kwa Tume hiyo. Kwa
upande wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha, leo ni mwaka wa thelathini tangu
Katiba kuelekeza Akaunti hiyo kufunguliwa na bado haijafunguliwa.
Kutokana na kushindikana kufunguliwa huko, kwa miaka yote hii, bajeti ya
Muungano imekuwa ndio bajeti ya Tanganyika, kinyume na maelekezo ya
Katiba.
Mwaka 2006 Tume ya Pamoja ya Fedha
iliajiri wataalamu waelekezi kutoka kampuni kimataifa ya uhasibu ya
PriceWaterhouseCoopers kuangalia suala la gharama na mgawanyo wa fedha
za Muungano. Wataalamu hao walifanya uchambuzi halisi wa mambo yapi ni
ya Muungano na yapi ni ya Tanganyika
na yapi ni ya Zanzibar na
gharama za uendeshaji wa kila moja. Baada ya orodha kupatikana,
watafiti hao walitafuta matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa
muda wa kiasi cha miaka 10 iliyopita.
Watafiti
wa PriceWaterhouseCoopers walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya
mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Muungano halisi. Mwishowe,
wakalinganisha iwapo mapato hayo yanakidhi matumizi ya Muungano au yana
upungufu. Taarifa ya uchambuzi wa PriceWaterhouseCoopers ilitolewa kama
Mapendekezo ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato na Kuchangia
Gharama za Muungano ya mwezi Agosti 2006.
Taarifa
ya Tume ya Pamoja ya Fedha inaonyesha hali ya kusikitisha kuhusu mapato
na matumizi ya fedha za Muungano, hasa kwa upande wa Tanganyika. Ili
kupata picha kamili ya hali halisi ilivyo, tunaomba
kunukuu sehemu ya Taarifa hiyo in extenso, kwenye ukurasa wake wa 18:
"Uchambuzi
unaonyesha kuwa mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi
matumizi ya Muungano na kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu zinaonyesha
kuwa kiasi kidogo cha mapato hayo kimekuwa kinagharimia matumizi ya
Muungano. Kwa mfano, uwiano huu ulikuwa ni (shilingi
bilioni
360.679 kati ya (shilingi bilioni 1,030.513) sawa na asilimia 35 mwaka
1999/2000, (shilingi bilioni 468.450) kati ya (shilingi bilioni
1,801.733) sawa na asilimia 26 mwaka 2002/03, na (shilingi bilioni
636.078) kati ya (shilingi bilioni 2,271.710) sawa na asilimia 28 mwaka
2003/04.
"Uchambuzi unaonyesha kuwa kiasi
kikubwa cha ziada ya mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika kugharimia
mambo yasiyo ya Muungano. Viwango hivi kwa mwaka 1999/2000 vilikuwa ni
(shilingi bilioni 39.822) sawa na asilimia 5.9 kwa (Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar) na (bilioni 631.714) sawa na asilimia 94.1 kwa
Tanzania Bara. Viwango hivi vilibadilika kwa kiasi kikubwa kwa mwaka wa
fedha 2003/04 ambapo kwa (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kilishuka hadi
(shilingi bilioni 37.053) sawa na asilimia 2.3, na (shilingi bilioni
1,588.494) sawa na asilimia 97.7 kwa (Serikali ya Muungano wa
Tanzania)."
Takwimu za utafiti wa
PriceWaterhouseCoopers zinaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2003/2004
pekee, matumizi halisi kwa vifungu vya Muungano yalikuwa shilingi
bilioni 537.258 ambayo ni asilimia 20 tu ya bajeti yote ya Serikali ya
Muungano kwa mwaka huo. Mapato halisi ya vyanzo vya mapato vinavyotokana
na mambo ya Muungano kwa mwaka huo yalikuwa ni shilingi bilioni
1,030.826, au takriban shilingi trilioni 1.030. Kwa maana nyingine,
mapato na matumizi ya fedha zinazotokana na
vyanzo vya mambo
ya Muungano yaliacha ziada ya shilingi bilioni 493.567 kwa mwaka huo
mmoja. Ziada hii ni nje ya mapato yaliyotokana na misaada na mikopo
kutoka nje, na ilitumika kwa shughuli za
maendeleo za Tanganyika zisizo za Muungano.
Kwa
sababu Tanganyika imekuwa inafaidika sana na utaratibu huu, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano - ambayo kiuhalisia ni Serikali ya Tanganyika
iliyovaa joho la Muungano - imekataa kutekeleza mapendekezo ya Tume ya
Pamoja ya Fedha kwamba uwekwe utaratibu utakaowezesha kutenganisha
mapato na matumizi ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Miaka nane tangu
mapendekezo hayo yatolewe mwaka 2006, "Serikali zetu mbili", kwa maneno
ya Mh. Samia Suluhu Hassan, "bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo
yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha."
Mheshimiwa Spika,
Kero
nyingine kubwa ya Muungano huu na ambayo ina umri karibu sawa na
Muungano wenyewe inahusu hisa za Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki kabla ya Bodi hiyo kuvunjwa mwaka 1965 na
Benki Kuu ya Tanzania kuanzishwa. Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri
Suluhu
Hassan, hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ni
mojawapo ya "kero zilizobaki katika orodha ya mambo ya kutafutiwa
ufumbuzi...." Kufuatana na maelezo hayo, "masuala ya Bodi
ya
Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu yapo katika
ngazi ya Mawaziri wa Fedha wa (Serikali ya Jamhuri ya Muungano) na
(Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kwa hatua za majadiliano."
Alipohojiwa
juu ya hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki mwezi Januari 2013, Waziri huyo huyo aliiambia Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala kwamba: "Katika Kikao
cha Kamati
ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano
kilichofanyika tarehe 14 Januari 2013 imeelezwa kwamba Mawaziri wa Fedha
wa SMT na SMZ wamepatiwa nyaraka maalum zenye taarifa za siri na
wamekubaliana kujadili suala hili mwezi Februari, 2013 baada ya
kuzipitia nyaraka hizo." Kwa vile bado mawaziri wanajadiliana, kama
tulivyosema mwaka jana, "sio tu kwamba Wazanzibari hawajui ni kiasi gani
cha fedha zao zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kufuatia
kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, bali pia hawana
uhakika watazirudishiwa lini!"
Mheshimiwa Spika,
Kwa
vile fedha za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu zilichukuliwa na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano baada ya masuala ya fedha, sarafu na Benki Kuu
kufanywa kuwa mambo ya Muungano mwaka 1965, sisi tuliozaliwa ndani ya
Muungano tuna haki ya kuambiwa ukweli kwanini Serikali hii ya CCM
imeshindwa kurudisha fedha hizo kwa Wazanzibari kwa takriban miaka
hamsini tangu fedha hizo zinyakuliwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
aka Serikali ya Tanganyika? Tunahitaji kuelezwa Serikali hii
ya CCM inahitaji muda wa miaka mingapi mingine ili iweze kurudisha fedha za watu na
kuwaepusha Watanganyika na laana ya wizi wa fedha za Wazanzibari?
Kwa
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar au Wazanzibari wenyewe katika umoja wao, wana haki ya kutumia
njia yoyote ile watakayoona inafaa, ikiwamo kufungua kesi za madai
katika mahakama za ndani au mahakama za kimataifa, kudai fedha zake
zote
halali ambazo zimeibiwa na Tanganyika kwa kutumia kivuli cha Muungano
katika kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
vyovyote vile, takwimu hizi zinaonyesha kwamba, kwa sababu ya Muungano
huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji.
Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya
'himaya' ya Tanganyika na 'koloni' lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni
huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na
uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya
makoloni yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao
wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii
na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati
ya Tanganyika na Zanzibar tangu kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26
Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe
20 Aprili, 1968, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo wakati akihojiwa na
gazeti la The Observer la London, Uingereza: "If the mass of the people
of Zanzibar should, without external manipulation, and
for
some reason of their own, decide that the Union was prejudicial to their
existence, I could not bomb them into submission.... The Union would
have ceased to exist when the consent of its constituent members was
withdrawn." Yaani, "endapo umma wa wananchi wa Zanzibar wataamua, bila
kurubuniwa kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe, kwamba Muungano
unaathiri kuendelea kuwepo kwao, sitaweza kuwalazimisha kwa kuwapiga
mabomu.... Muungano hautaendelea kuwepo pale ridhaa ya washirika wake
itakapoondelewa."
Miaka 45 baada ya kauli hiyo
ya Mwalimu Nyerere, Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar, alisema yafuatayo katika Maoni aliyoyatoa kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba tarehe 13 Januari, 2013: "Mfumo (wa Muungano)
uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari.
Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati umefika tushone
koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi."
Nalo
Baraza la Wawakilishi Zanzibar, katika maoni yake kwa Tume ya tarehe 5
Februari, 2013, limetaka 'kuwa na Muungano wa dhati', yaani "...
Muungano wa kweli, hata kama ni kwa maeneo machache, kwa dhati ya
wanasiasa na Watanzania kwa ujumla." Kwa mujibu wa Baraza hilo, Muungano
'wa dhati' na 'wa kweli' ni ule ambao kuna "... Mamlaka ya Zanzibar
huru na Mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Muungano, (na) Mamlaka ya
Muungano iwekwe wazi - maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na
utendaji wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake."
Aidha,
Baraza la Wawakilishi limependekeza kwamba "rasilmali za Muungano ziwe
ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilmali hizo ndio zitumike
katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano. Ugawaji wa rasilmali ufanywe
kwa uwiyano maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na
pande mbili za Muungano."
Hata
kama baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar baadaye
waliyakana maneno yao haya walipofika mbele ya wakubwa wao wa Tanganyika
wakati wa vikao vya Bunge Maalum hapa Dodoma, haya sio maneno ya
kupuuza hata kidogo kwa sababu yanathibitisha kwamba hata wale
Watanzania wachache, kama wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
ambao wamefaidika kwa kupata nafasi za uongozi kwa sababu ya Muungano,
hawauoni Muungano huu kama kielelezo cha umoja, mshikamano
na upendo wao. Kuyapuuza maneno haya ni kujenga misingi imara na hakika ya Muungano huu kuvunjika.
NCHI MOJA AU NCHI MBILI?
Mheshimiwa Spika,
Kuna
propaganda na uongo mwingine juu ya Muungano huu ambayo imeenezwa sana
katika kipindi hiki cha nusu karne ya uhai wake. Propaganda hii inahusu
kile kilichozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano, yaani Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Baada ya jina la Jamhuri hiyo
kubadilishwa kuwa Tanzania tarehe 28 Oktoba, 1964, ilizaliwa dhana
kwamba Makubaliano ya Muungano yaliua nchi za Tanganyika na Zanzibar na
kuanzisha 'nchi moja' ya Tanzania. Dhana hii
imetumika, katika
miaka hamsini ya Muungano huu, kuhalalisha ukiukwaji wa matakwa ya
Makubaliano ya Muungano kwa kutumia dhana nyingine ya 'kuimarisha
Muungano.' Dhana hizi mbili ndio msingi wa nyongeza zote za mambo ya
Muungano, na ndio sababu kubwa ya kuporomoka kwa uhuru na mamlaka ya
Zanzibar katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika,
Dhana
kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano iliua nchi mbili na kuzaa nchi
moja ya Tanzania ni dhana potofu na isiyokuwa na msingi wowote katika
Hati yenyewe. Kwanza, Hati ya Makubaliano ya Muungano ilitamka wazi
kwamba sheria zilizokuwepo Tanganyika na Zanzibar kabla ya Muungano
zitaendelea kutumika 'katika nchi zao' hadi hapo zitakaporekebishwa ili
kutilia nguvu Muungano na Hati za Muungano; au sheria mpya
zitakapotungwa na mamlaka husika au kutolewa kwa amri ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano kwa ajili ya utekelezaji wa Mambo ya Muungano kwa upande wa
Zanzibar.
Pili, vifungu mbali mbali vya Katiba
zilizofuatia Makubaliano ya Muungano ziliweka wazi kwamba Tanganyika na
Zanzibar hazikuuawa na Makubaliano ya Muungano. Hivyo basi, hata baada
ya mabadiliko ya jina kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba na
sheria mbali mbali
ziliendelea kutumia jina la Tanganyika na
Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya Kuongeza Muda wa Kuitisha Bunge la
Katiba, 1965, iliyosainiwa na Rais Nyerere tarehe 24 Machi, 1965,
inataja, katika vifungu vyote
vitatu, 'Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.'
Aidha,
Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya Tanzania ya tarehe 11 Julai,
1965, ilitangaza kwamba 'Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano'; kwamba
eneo lake ni "... eneo lote la Tanganyika na Zanzibar ..." na kwamba
chama kimoja cha siasa "... kwa Tanganyika kitakuwa Tanganyika African
National Union (TANU)...." Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda
haikuwahi kutamka kuwa Tanzania ni nchi moja. Badala yake, ibara ya
27(1) ya Katiba hiyo iliyokuwa inahusu sifa za kuchaguliwa kuwa mbunge
ilitamka wazi kwamba: "Raia yeyote wa Tanganyika ambaye amefikisha umri
wa miaka ishirini na moja na ni mwanachama (wa TANU) atakuwa na sifa ya
kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo...."
Kwa
upande wake, licha ya kuanza kutumia jina la Tanzania Bara na Tanzania
Visiwani kwa mara ya kwanza, Toleo la Kwanza la Katiba ya sasa ya
Muungano lilitamka kwamba Tanzania ni 'Jamhuri ya Muungano.' Hapa pia
hapakuwa na tamko la 'nchi moja.'
Mheshimiwa Spika,
Maneno
ya ibara ya 1 ya Katiba ya sasa ya Muungano kwamba "Tanzania ni nchi
moja na ni Jamhuri ya Muungano" yaliingia katika kamusi ya kikatiba na
kisiasa ya nchi hii kufuatia 'kuchafuka kwa hali ya
kisiasa ya
Zanzibar' na kung'olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe. Kufuatia hali
hiyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa
ambayo, pamoja na mengine, yalitangaza kuwa
"Tanzania ni nchi
moja na ni Jamhuri ya Muungano." Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa
Wazanzibari, Marekebisho hayo ya Katiba yaliondoa pia maneno 'Tanzania
Visiwani' na kuweka 'Tanzania Zanzibar' badala yake. Maneno 'Tanzania
Bara' yalibaki kama yalivyowekwa mwaka 1977.
Kwa
maana hiyo, dhana ya Tanzania kama nchi moja haijatokana na Makubaliano
ya Muungano bali ilitokana na siasa za Muungano, yaani mvutano kati ya
viongozi wa Tanganyika wakiwa wamevalia joho la Jamhuri ya Muungano na
viongozi wa Zanzibar waliotaka uhuru zaidi kwa nchi yao. Pili, dhana
hiyo haina umri mkubwa sana kuliko inavyodhaniwa, kwani iliingia kwenye
Katiba mwaka 1984, miaka
thelathini iliyopita, na miaka ishirini baada ya Muungano.
MUUNGANO USIO WA USAWA
Mheshimiwa Spika,
Tangu
mwanzo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa Muungano wa usawa.
Huu ni Muungano ulioipa Tanganyika - ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya
Muungano - mamlaka ya kuingilia uhuru na mamlaka ya Zanzibar. Hii
inathibitishwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano
yenyewe.
Kwanza, kwa kutamka kwamba katika kipindi cha mpito "Katiba ya Jamhuri
ya Muungano itakuwa ni Katiba ya Tanganyika...", ni wazi kwamba Mshirika
wa Muungano aliyekuwa na nguvu katika Muungano huu ni Tanganyika.
Pili,
kwa kuweka orodha ya mambo 11 ya Muungano, ni wazi kwamba Zanzibar
ilinyang'anywa mamlaka juu ya masuala hayo na mamlaka hayo yalihamishiwa
kwa Tanganyika ikiwa imevaa koti la Jamhuri ya Muungano. Kwa maana
hiyo, Zanzibar ilinyang'anywa mamlaka yake juu ya masuala ya nchi za
nje, ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia, uhamiaji,
biashara ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya
Makubaliano ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba "Bunge na Serikali
(ya Jamhuri ya Muungano) litakuwa na mamlaka kamili kwenye mambo hayo
kwa Jamhuri ya Muungano na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa ajili ya
mambo mengine yote ya na kwa ajili ya Tanganyika."
Tatu,
kwa kutangaza kwamba rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa
Mwalimu Nyerere na Makamu wa kwanza wa Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume;
na kwa kutangaza kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa ndiye msaidizi
mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa majukumu yake
ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi kwamba Hati ya Makubaliano ya
Muungano ilithibitisha nafasi ya chini (subordinate position) ya
Zanzibar katika Muungano.
Nne, kwa kuzifanya
alama za utaifa (national emblems) za Tanganyika kuwa ndio alama za
taifa za Jamhuri ya Muungano, kuna-emphasize superior position ya
Tanganyika ndani ya Muungano na subaltern position ya Zanzibar katika
Muungano huu. Ukweli huo huo unahusu masuala ya kuzifanya taasisi na
watumishi wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio taasisi na watumishi wa
Jamhuri ya Muungano.
Tano, hata kwa kuangalia
watu ambao wamewahi kupata fursa ya kuongoza Jamhuri ya Muungano, ni
wazi kwamba Watanganyika ndio wamekuwa mabwana na Wazanzibari wamefanywa
watwana katika masuala ya haki za kiutawala.
Hivyo,
kwa mfano, katika kipindi cha miaka hamsini ya Muungano huu, ni
Mzanzibari mmoja tu ndiye aliyepata fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano, kwa miaka kumi kati ya miaka hamsini hiyo. Kwa utaratibu huo
huo, tokea mwaka 1964, Zanzibar haijawahi kutoa Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi au Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Zote
hizi ni taasisi za Muungano. Aidha, Zanzibar imewahi kutoa Waziri Mkuu
mmoja tu, tena kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, na Jaji Mkuu mmoja
tu katika kipindi hicho cha nusu karne ya Muungano huu. Vile vile,
katika Diplomatic Corps, kwa sasa kuna Wazanzibari wawili tu ambao ni
mabalozi wa Tanzania nchi za nje kati ya mabalozi
32 wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.
Mheshimiwa Spika,
Hata
Bunge lako tukufu lina rekodi mbaya katika masuala haya. Hivyo, kwa
mfano, katika miaka yote ya Muungano, hakuna Mzanzibari ambaye amewahi
kushikilia nafasi ya Spika au Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano. Aidha, licha ya Kanuni za Bunge lako tukufu kuruhusu kufanyika
kwa vikao vya Kamati zake za Kudumu nje ya Dodoma, yaani Dar es Salaam
na/au Zanzibar; na licha ya Kanuni kuruhusu Mikutano ya Bunge kufanyika
nje ya Dodoma ikiwa 'itaelekezwa vinginevyo', hakuna
Kamati
hata moja ya Bunge hili tukufu ambayo imewahi kufanya vikao vyake
Zanzibar na haijawahi kutokea Bunge hili likaelekezwa kufanya Mikutano
yake nje ya Tanganyika!
KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Baada
ya nusu karne ya Muungano wa aina hii, wananchi wa Tanganyika na, hasa
wa, Zanzibar hawako tayari kuendelea na utaratibu huu wa kinyonyaji na
kikandamizaji. Wananchi wanataka mabadiliko ya msingi ya muundo wa
Muungano na uendeshaji wake. Wananchi wanataka kusikilizwa juu ya
Muungano. Wananchi wanataka kufanya maamuzi kuhusu kama wanataka
kuendelea na Muungano na, kama jibu ni ndiyo, muundo wa Muungano huo.
Wakati
wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba katika
Bunge Maalum, Kamati nyingi zilishindwa kufanya maamuzi kwa sababu ya
kukosa uungwaji mkono wa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Kamati kutoka
Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar. Kama hali ni
hiyo katika Bunge Maalum licha ya Bunge hilo kujazwa wajumbe wengi wa
CCM kutoka kundi la 201, hali ni mbaya zaidi nje ya Bunge Maalum na nje
ya Bunge lako tukufu. Nje ya mabunge haya,
watu wengi, hasa
Wazanzibari ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa Muungano huu
katika nusu karne ya maisha yake, wananchi wengi hawataki tayari
kuendelea na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Katika
mazingira haya, namna muafaka ya kutoka katika constitutional impasse
inayokuja mbele yetu, ni kuwauliza wananchi wa Tanganyika na Zanzibar -
kwa kutumia kura ya maoni - kama bado wanataka kuendelea na Muungano
huu. Na kama jibu lao litakuwa ni ndiyo, basi wananchi waamue, katika
kura hiyo, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Miaka hamsini ya
watawala kuamua masuala haya muhimu peke yao inatosha. Huu ni wakati
muafaka kwa wananchi kufanya maamuzi haya makubwa kwa maisha yao na kwa
nchi zao mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawataka wabunge wa
Bunge lako tukufu wawe kwenye upande sahihi wa historia, yaani upande wa
wananchi katika jambo hili.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Katika
kuhitimisha maoni haya, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama vyetu vitatu vinavyounda Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni kwa kufanya maamuzi ya kuendeleza ushirikiano
ulioanzia ndani ya Bunge Maalum, kwenye Bunge lako tukufu.
Wananchi
wetu wanataka mabadiliko ya msingi ya utawala wa nchi zetu mbili na
usimamizi wa rasilmali zake. Kama ilivyokuwa kwa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) ndani ya Bunge Maalum, ndivyo wananchi wanavyotutazamia
kuendesha shughuli zetu ndani ya Bunge hili tukufu.
Historia itatuhukumu vikali endapo tutashindwa kukamata fursa hii ya kihistoria katika nchi zetu mbili.
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
------------------------------ ----------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
Post a Comment