HOTUBA YA
MHESHIMIWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
WAKATI WA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA HOSPITALI YA CHUO KIKUU CHA AFYA
NA SAYANSI SHIRIKISHI MUHIMBILI, KAMPASI YA MLOGANZILA, TAREHE 24 APRILI 2014
Mheshimiwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini;
Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam,
Professa Ephata Kaaya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi
Shirikishi, Muhimbili.
Viongozi na Watendaji wa Serikali,
Viongozi na Wanajumuia wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Shukrani
Awali ya yote, napenda kukushukuru Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa
kunialika kuja kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya kisasa ya
kufundishia na kutolea huduma katika eneo hili la Kampasi mpya ya Chuo Kikuu
cha Afya Sayansi Shirikishi Muhimbili, Mloganzila. Leo ni siku ya aina yake
katika historia ya Chuo Kikuu cha Muhimbili na taifa kwa jumla. Kitendo hiki
cha leo kinaashiria kuanza rasmi kwa kazi ya ujenzi wa Kampasi mpya ya
Mloganzila ya MUHAS na ni kubwa katika uboreshaji wa huduma ya afya nchini.
Shughuli hii kufanyika leo kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano
wetu ni jambo stahiki kabisa. Ujenzi huu ni moja ya kielelezo thabiti cha
juhudi na mafanikio ya Serikali yetu, katika kuwapatia Watanzania huduma bora
zaidi za afya.
Hali ya Sekta ya Afya Wakati Tunaungana
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Utoaji wa huduma bora za afya ni wajibu wa msingi wa Serikali
yetu na uhai wa taifa letu. Wakati tulipoungana tarehe 26 Aprili, 1964, hali ya
huduma ya afya ilikuwa duni na afya ya wananchi wetu haikuwa ya kuridhisha.
Kulikuwa na hospitali chache mno, halikadhalika, vituo vya afya na zahanati
zilikuwa chache sana. Iliwalazimu wananchi kutembea umbali mrefu sana kutafuta
huduma za afya. Katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya vifaa vya
uchunguzi na vifaa tiba vilikuwa haba na duni. Wataalamu wa fani mbalimbali za
afya walikuwa wachache sana. Watu walikuwa wanakufa siku si zao kwa maradhi
yanayoweza kuzuilika na kutibika. Umri wa wastani wa kuishi ulikuwa miaka 35.
Kwa ajili hiyo, Serikali zetu zilitangaza maradhi kuwa moja ya maadui watatu
wakubwa, wengine wakiwemo umaskini na ujinga.
Katika kipindi cha miaka 50 ya muungano, Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar zimepambana na adui maradhi kwa nguvu kubwa. Tumetoa
kipaumbele cha juu katika kupanua na kuboresha huduma za afya. Hii
imejidhihirisha kwa sera na mikakati mbalimbali ya afya inayotekelezwa, ukubwa
wa bajeti za afya zinazotengwa, idadi ya miradi inayotekelezwa na matokeo
mazuri yanayopatikana kutokana na juhudi hizo za Serikali.
Mafanikio ya Miaka 50 ya Muungano katika Sekta ya Afya
Ndugu
Wananchi;
Jitihada zilizofanyika katika miaka 50 iliyopita zimewezesha kuongezeka kwa
zahanati, vituo vya afya na hospitali, vifaa vya uchunguzi, vifaa tiba na
wataalamu wa kada mbalimbali za afya. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya
Watanzania wanaopata huduma bora za afya katika ngazi zote imeongezeka sana na
ushindi dhidi ya maradhi mengi unaonekana. Uwezo wetu wa kupambana magonjwa
yanayoua watu wengi nchini umefikia mahali pazuri, na ule wa kuchunguza na
kutibu maradhi yanayotulazimu kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi unaendelea
kuimarika. Kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa watoto na akina mama
wajawazito yamepungua kwa asilimia 50, na kule Zanzibar maambukizi ya malaria
ni asilimia 0.3. Maambukizi ya UKIMWI yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 1986
hadi kufikia asilimia 5.1 hivi sasa.
Tunaendelea kuimarisha vituo vya kutoa huduma ya afya kuanzia zahanati, vituo
vya afya, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na taifa kwa majengo, vifaa tiba,
vifaa vya uchunguzi na wataalamu. Katika ngazi ya taifa kwa mfano, tumepiga
hatua ya kutia moyo kwa maradhi ya moyo, figo, saratani, mifupa, ubongo na
mishipa ya fahamu. Kwa upande wa maradhi ya moyo tumejenga kituo cha tiba na
mafunzo ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye vitanda
100. Kituo hiki kinawezesha wagonjwa wa moyo wengi kupata matibabu hapa hapa
nchini badala ya kupelekwa nje. Katika kipindi cha mwaka mmoja cha ufanyaji
kazi wake, kituo hiki kimeweza kufanyia upasuaji wagonjwa 347, kuwawekea
mashine za kuongeza nguvu kwenye moyo (pacemaker) wagonjwa 3 na mwaka huu
wameanza uwekaji wa vyuma vidogo (stent) katika mishipa ya damu ya moyo ambayo
imebana. Haya ni mafanikio makubwa na ya kutia moyo.
Kwa upande wa figo, hivi sasa tunatoa huduma za magonjwa ya figo katika
Hospitali ya Muhimbili, Hospitali ya Kanda, Mbeya na Shule ya Tiba ya Chuo
Kikuu cha Dodoma. Pale Chuo kikuu cha Dodoma pia tunajenga kituo kikubwa
kitakachobobea kwenye maradhi ya figo. Lengo letu ni kwamba, kitakapokamilika
chuo hiki kiweze kufanya matibabu ya kubadilisha figo (kidney
transplant).
Aidha, tumeboresha taasisi ya saratani ya Ocean Road kwa mejengo, vifaa na
wataalamu. Tumeongeza maradufu uwezo wa taasisi hiyo kulaza wagonjwa kutoka
wagonjwa 120 mwaka 2011 hadi wagonjwa 290 hivi sasa. Halikadhalika, tumenunua
mashine mpya kwa ajili ya uchunguzi na tumeongeza wataalamu waliobobea wa
magonjwa ya saratani. Vilevile, tunakamilisha ujenzi wa jengo la Taasisi ya
Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu. Litakapokamilika tutaliwekea vifaa vya
kisasa vya uchunguzi na tiba ili kuongeza uwezo wetu wa kukabiliana na maradhi
haya.
Ujenzi wa Hospitali ya Kufundishia ya Kampasi ya Mlonganzila
Ndugu
Wananchi;
Jiwe la msingi
tunaloweka leo, ni mwendelezo wa juhudi hizi za Serikali za kupambana na adui
maradhi. Hospitali hii itakuwa na vitanda 600, itakuwa na vifaa tiba vya kisasa
kabisa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya
mishipa ya fahamu. Ujenzi wa Hospitali ya Kampasi hii utasaidia sana kupunguza
msongamano kwenye hospitali ya rufaa ya Taifa ya Muhimbili na za rufaa zilizopo
nchini, ambazo hutoa huduma za utaalamu wa juu. Aidha, itasaidia kupunguza
ulazima wa kupeleka wagonjwa nchi za nje kwa ajili ya matibabu. Matibabu nje ya
nchi ni gharama kubwa kwa Serikali, lakini pia fursa zenyewe ni chache na wengi
wengi hawapati nafasi ya kupelekwa nje kwa matibabu. Hivyo ujenzi wa hospitali
hii ya Chuo Kikuu cha Muhimbili ni ishara ya wazi ya dhamira ya serikali katika
kukabiliana na tatizo hili.
Hatua
Zilizochukuliwa na Serikali Katika Ujenzi wa Kampasi na Hospitali ya
Kufundishia
Ndugu Wananchi;
Baada ya Chuo Kikuu cha Muhimbili kutafuta eneo la kupanua
huduma zake, mwaka 2006 nilifanya uamuzi wa kuwapatia eneo hili lenye ukubwa wa
ekari 3,800 kwa ajili ya kujenga Kampasi mpya na hospitali ya kisasa ya
kufundishia na kutolea huduma. Tulianza kutafuta fedha za ujenzi wa hospitali
ya kufundishia, tukafanikiwa kupata mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya
Jamhuri ya Korea Kusini wenye thamani ya dola za Marekani milioni 76.5. Mkopo
huo ungetosheleza kujenga jengo la hospitali hiyo pamoja na vifaa vya kisasa
vya kutosheleza mahitaji ya hospitali.
Ujenzi haukuweza kuanza kwa wakati kutokana na mgogoro wa ardhi uliokuwepo
katika eneo hili. Matokeo ya ucheleweshaji huo umepandisha gharama za ujenzi
kwa dola za Marekani milioni 18. Maana yake ni kuwa fedha za mkopo tulizopata
hazitoshi tena kukamilisha jengo hilo na kununulia vifaa kama ilivyokusudiwa.
Viongozi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili waliponijia nilikubali bila kusita kwamba
Serikali itaongeza hizo dola milioni 18 zinazohitajika. Niwahakikishie kuwa
tutatoa fedha hizo ili ujenzi ukamilika kwa kiwango kilichotarajiwa.
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Ni mategeneo ya Serikali kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa
Kampasi hii, Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili kitakuwa na
uwezo wa kuongeza udahili wa wanafunzi wa fani mbalimbali za afya kutoka
takribani wanafunzi 3,000 na kufikia wanafunzi 15,000. Hii itapunguza kwa kaisi
kikubwa, kama si kumaliza kabisa uhaba mkubwa wa wataalam wa fani za afya
ulioko nchini kwa sasa. Aidha, ni mategemeo yangu pia kuwa wakati ujenzi
utakapokamilika idadi ya wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu itaongezeka
kwa kiasi kikubwa na hivyo kuongeza idadi ya wataalamu waliobobea wa fani
mbalimbali za afya.
Hitimisho
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kwa kumalizia, napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa
kutupatia mkopo wa ujenzi na vifaa vya hospitali hii. Mkopo uliotolewa ni mkopo
wenye riba nafuu ambao kama usingepatikana ingebidi tutumie fedha iliyopangwa
kwa ajili ya miradi mingine kwenye ujenzi wa hospitali hii. Napenda kuwashukuru
wananchi wa maeneo ya Kwembe na Mloganzila kwa kutoa ushirikiano katika mradi
huu. Mradi huu ni moja ya kielelezo cha mafanikio ya Muungano wetu wa Miaka 50,
tuutunze utakapokamilika ili utufae kwa miaka 50 mingine. Nawatakieni kila la
heri katika kusherehekea miaka 50 ya Muungano wetu.