SIKU moja baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kutangaza majina ya
wagombea, baadhi ya vigogo walioachwa kwenye uteuzi huo wameeleza ya
moyoni, huku Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe akisema anaamini
ametoswa kwa sababu alitia saini ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
Katika
Bunge la 10 lililoketi Aprili mwaka huu, baadhi ya Wabunge wa CCM
akiwamo Filikunjombe, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugola, waliunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na
Pinda iliyokuwa imeanzishwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe wa CHADEMA.
Wabunge
hao wa chama tawala, waliungana na wenzao wa upinzani kutaka kupiga
kura za kutokuwa na imani na Pinda kutokana na kile kilichoelezwa kuwa
ameshindwa kuisimamia Serikali kwa kuwawajibisha mawaziri wazembe.
Hata hivyo, mpango huo haukufanikiwa baada ya Spika wa Bunge Anne Makinda kueleza kuwa haukufuata taratibu zinazotakiwa.
Filikunjombe
Filikunjombe
alipotakiwa jana kuzungumzia kuenguliwa kwake kwenye kinyang'anyiro cha
uchaguzi wa ndani ya chama, alisema anaamini yeye na wenzake hao wa
CCM, wametoswa kwa sababu ya kushiriki mpango wa kumng'oa Waziri Mkuu
Pinda.
Hata hivyo,
alisema amelazimika kukubali hali hiyo na kupokea matokeo, kwa kuwa
hatua yake ya kusaini kitabu hicho ilitokana na nia njema kutaka Waziri
Mkuu ajiuzulu ili mambo fulani muhimu katika jamii
yafanyike. Filikunjombe alibainisha kuwa alisaini kitabu hicho cha
kutokuwa na imani na Pinda akiwa na akili timamu na alikuwa anajua
kinachoweza kutokea kutokana na hatua yake hiyo.
"Nimesaini
kitabu kile kwa nia njema, nikiwa na akili timamu na sijutii uamuzi
wangu huo, ila siwezi kuwasemea Kigwangalla (Khamis mbunge wa Nzega) na
Bashe (Hussein). Lakini sisi watatu (yeye, Lugola, Mkono) tumeenguliwa
kwa sababu hiyo (ya kutokuwa na imani na Pinda)." Aliendelea: "Nashangaa
leo naonekana adui wa chama wakati nilikuwa nakinusuru na kusema kweli
adui wa CCM ni Wabunge wa chama hicho ambao hawakusaini kitabu hicho cha
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, " alisema Filikunjombe.
Mkono
Mbunge wa Musomo Vijijini, Nimrod Mkono alisema kutoswa kwake ni uamuzi wa watu aliowaita wenye chama.
"Walikata
jina langu nikakata rufaa, likarudishwa Dodoma, lakini walipokutana
wakaona sifai. Wakaamua kunifukuza sasa hapo mimi nifanye nini?" alihoji
Mkono.
Mkono alisema
huu ni utaratibu wa chama chao cha CCM ambao umewapa baadhi ya watu
haki ya kuwafukuza wengine bila kuwapa fursa ya kujitetea, "Kama
ilivyotokea kwangu wamekaa na kuona Mkono hafai, fukuza basi wakafanya
hivyo na hiyo haijalishi kama nilisaini kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
au la. Suala la msingi ni kuwa Mkono amefukuzwa na atarudi kama
ilivyokuwa kwa mwana mpotevu." alisema bila kufafanua.
Kigwangalla
Mbunge
wa Nzega, Dkt. Hamis Kigwangalla alisema anaheshimu uamuzi wa vikao
vilivyokaa na kufikia uamuzi uliochukuliwa na kwamba, ataendelea kuwa
mwanachama na kukitumikia chama pamoja na wananchi kwa nguvu zote bila
kinyongo, “Nitaendelea kuheshimu vikao vya chama changu na kuwa
mwanachama hai ingawa sijajua wametumia vigezo gani kuteua majina hayo,”
alisema Dkt. Kigwangalla.
Bashe
Kwa
upande wake Bashe alisema kilichotokea ni uamuzi wa chama na vikao
halali vilivyokaa na kuchukua uamuazi huo, “Sijui kwa nini jina langu
halikupitishwa, lakini nitaendela kuwa mwanachama na kuwatumikia
wananchi wenzangu wa Nzega,” alisema Bashe. Katika kuhakikisha hilo,
Bashe alisema leo anakwenda Nzega kupeleka mifuko ya saruji tani 18 kwa
ajili ya ujenzi wa ofisi za kata za chama hicho wilayani humo.
Kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitaka makada waliotoswa na
wenye kinyongo wawasilishe malalamiko yao CCM kwa maandishi badala ya
kulalamika nje ya utaratibu."Wathibitishe kwa maandishi nasi chama
tutajua la kufanya, kwani wabunge hao hawakuingia katika vikao
vilivyotoa maamuzi sasa nashangaa kusikia katika vikao tuliwajadili na
hoja iliyowaondoa ni hiyo," alisema Nape.
Maoni ya wasomi
Wakizungumzia
uteuzi huo wasomi na wanasiasa walitoa maoni tofauti huku baadhi
wakisema chama kinatakiwa kuwa na sera na mtizamo wa kuliletea maendeleo
taifa bila kujali kama chama kinaongozwa na wazee au vijana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson Bana
alisema uamuzi huo wa CCM umeonyesha kuwa, ndani ya chama hicho hakuna
aliye juu kuliko mwenzake, “Wapo waliosema wakitoswa patachimbika,
lakini wametoswa na hapajachimbika, uamuzi wa kuwatosa watu wa aina hii
utarejesha nidhamu ndani ya chama hicho licha ya kuwa kazi bado ni
kubwa,” alisema Dk Bana.
Profesa Gaudence Mpangala alisema
vijana kupewa nafasi kubwa ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM,
hakuna maana kuwa sera na mtizamo wa chama hicho utabadilika, “Kuwa na
wanachama au wagombea wenye umri wa wastani(vijana) sio kigezo cha chama
kufanya vyema kwa sababu hawawezi kubadili sera na mtizamo wa chama
husika,” alisema Mpangala.
Dkt. Kitila Mkumbo
alisema kuingiza vijana wengi katika mpambano huo ni hatua ya ukomavu wa
kisiasa kwa kuwa chama hicho awali hakikuwa na utaratibu mzuri wa
kuwapa nafasi ya uongozi vijana, “Awali CHADEMA ndio kilionekana chama
kinachowapa nafasi zaidi vijana, lakini kwa hatua hii ya CCM ni nzuri,
sasa tunasubiri utendaji wao kama utakuwa na manufaa kwa taifa,” alisema
Mkumbo.
Bashiru Ally alisema kama kigezo cha
kuweka vijana wengi kitazingatia msimamo, fikra na ufanisi katika
utendaji kazi wao basi taifa lina kila sababu ya kuunga mkono hatua
hiyo. Alisema kwa kuwa vijana ndio chachu ya maendeleo kwa mataifa
mbalimbali duniani, hatua ya CCM kuwapa nafasi vijana ni nzuri kama
wakiifanya kazi hiyo kwa manufaa ya taifa kwanza.
Post a Comment