Na Fidelis Butahe,
Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO

KASHFA mpya imeibuka ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), baada ya kubainika kuwa vikombe vya kufungia nyaya za umeme vyenye thamani ya mamilioni ya fedha vimetelekezwa kutokana na baadhi ya vigogo wa shirika hilo kushindwa kunufaika na mradi huo.

Habari kutoka ndani ya shirika hilo zinaeleza kuwa vigogo hao wanadaiwa kuvikataa vikombe hivyo kwa maelezo kuwa ni vibovu, baada ya mzabuni kushindwa kuwaona vigogo hao.

Wakati vigogo hao wakivikataa vikombe hivyo kwa madai kuwa ni vibovu, taarifa zinaeleza kuwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamethibitisha kuwa vikombe hivyo ni vizuri na havina matatizo yoyote.

Hatua ya Tanesco kupeleka vikombe hivyo kuthibitishwa na wataalamu wa Chuo Kikuu, Kitengo cha Uhandisi ilitokana na mvutano uliokuwapo baada ya vigogo walioshindwa kunufaika na mradi huo kutoa maelezo kuwa vikombe hivyo havina viwango bora.

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa licha ya vigogo hao kuvikataa vikombe hivyo zaidi ya 40,000 vyenye thamani ya Sh900 milioni kwa madai kuwa vibovu, tayari shirika hilo limekuwa likivitumia katika nguzo zake zenye umeme mkubwa kwa miaka mingi.

Mvutano wa viongozi hao ndani ya shirika hilo, umesababisha mradi wa kukarabati njia za umeme mkubwa bila ya kuzima umeme kwa kuondoa vikombe vilivyochakaa uliokuwa ukifanyika katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kusimamishwa mapema mwaka huu.

Baadhi ya wataalamu wa Tanesco wanaeleza kuwa vikombe hivyo kama vitatumika vina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya kufunga vikombe vipya katika njia ya umeme mkubwa wa kutoka kwenye mtambo wa kuzalishia umeme wa Kidatu mkoani Morogoro hadi Ubungo jijini Dar es Salaam.

Pia, kumalizia ukarabati wa njia ya umeme ya Arusha hadi Moshi mkoani Kilimanjaro iliyositishwa. 

Chanzo chetu kutoka ndani ya Tanesco kinaeleza kuwa vikombe vilivyopo katika njia ya umeme ya Kidatu hadi Ubungo  havijabadilishwa kwa miaka mingi hali ambayo inafanya umeme kupotea njiani kwa asilimia nyingi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Tanesco, Felschami Mramba alisema kuwa mikataba ndani ya shirika hilo ni mingi na kusisitiza kuwa hawezi kulijibu suala hilo mpaka atakapowasiliana na kitengo cha ununuzi cha shirika hilo.

“Kwa sasa sina maelezo ya kina ya mikataba, hasa kuhusu suala hilo unaloniuliza, lakini mpaka wiki ijayo nitakuwa nimefuatilia na kupata jibu sahihi,” alisema Mramba.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulika Nishati, George  Simbachawene alisema suala hilo halijafika kwake.

Simbachawene alisisitiza: “Mambo yanayofika katika ofisi yangu huwa kama malalamiko yanayoletwa na watu kutoka Tanesco na sehemu nyingine. Nikiyapata naanza kufuatilia ili kujua nini kinaendelea.”

Alisema kuwa Tanesco ni shirika linalojitegemea katika utendaji wake wa kazi na ndiyo maana lina bodi yake, ambayo hukaa na kupanga mambo mbalimbali ya kufanya.

“Wakati mwingine wizara inaingilia utendaji wa Tanesco kama tunaona kuna mambo hayaendi sawa, ila hili la ununuzi kwa kweli sijui kwa sababu halijafika ofisini kwangu kama lalamiko,” alisema Simbachawene na kushauri kuwa atafutwe Mramba.

Hoja ya kuvikataa vikombe hivyo ambayo imekuwa ikitolewa na baadhi ya vigogo hao wa Tanesco ni kwamba vikombe hivyo ni vizito na nguzo haziwezi kuvibeba, vibovu na kwamba havifai katika ule utaratibu wa kufanya matengenezo bila kuzima umeme.

Tanesco imekuwa ikikumbwa na kashfa mbalimbali zikiwamo matumizi mabaya ya fedha za shirika kwa baadhi ya maofisa kutumia zabuni kujinufaisha.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi William Mhando alisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ilieleza kuwa Mhando alisimamishwa kazi pamoja na watendaji wakuu wengine wa Tanesco ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.


Viongozi wengine wa Tanesco waliosimamishwa kazi ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Ununuzi, Haruni Mattambo.

Matatizo mengine ambayo yanadaiwa kuikumba Tanesco ni pamoja na uchakavu wa mitambo ya Tanesco, hujuma za miundombinu na kuingiwa kwa mikataba mibovu.

Chanzo gazeti la Mwananchi
Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.