RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri
Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Meja Jenerali Samuel Albert
Ndomba kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Meja Jenerali Ndomba kuwa
Luteni Jenerali. Taarifa iliyotolewa, Septemba 21, 2012, mjini Dar es
Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue kupitia Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, imesema kuwa uteuzi huo unaanza mara
moja.
Meja Jenerali Samuel Albert Ndomba |
Taarifa hiyo ya Balozi Sefue imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Meja
Jenerali Ndomba alikuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Jenerali
Ndomba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Abdulrahman
A. Shimbo ambaye amestaafu Jeshi kwa mujibu wa sheria baada ya kufikisha
umri wa miaka 60.
Taarifa ya Balozi Sefue pia imesema kuwa Rais Kikwete amemteua
Brigedia Jenerali Raphael Mugoya Muhuga kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga
Taifa kuanzia leo, Ijumaa, Septemba 21, 2012.Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Brigedia Jenerali Muhuga kuwa Meja
Jenerali. Kabla ya uteuzi wake, Brigedia Jenerali Muhuga alikuwa Mkuu
wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Post a Comment