MAHAKAMA ya Mwanzo Tarime Mjini, imempa Zablon Kinogo siku tano
kuhakikisha anampeleka chuo binti yake Deborah Zablon aliyegoma kuolewa
ilihali alifaulu kidato cha Sita na kutakiwa kujiunga Chuo cha Ualimu
Marangu, mkoani Kilimanjaro.
Kwa amri
hiyo ya Mahakama iliyotolewa na Hakimu Jarome Migera, ni sawa na
‘ushindi’ kwa binti huyo mwenye umri wa miaka 20 aliyesisitiza kuipenda
elimu kuliko ndoa.
Akitoa agizo hilo
juzi, Hakimu Migera alimtaka Kinogo kuhakikisha analipa ada na gharama
nyingine zitakazomfanya Deborah kujiunga na masomo yake ndani ya siku
tano kuanzia juzi; Kinyume cha hapo, alionya hatua kali dhidi ya mzazi
huyo zitachukuliwa kwa kuteketeza familia.
Akitoa
agizo hilo alisema: “Mahakama yangu imekupa siku tano kuanzia leo
Ijumaa (juzi) hadi Jumanne(keshokutwa) uwe umewasiliana na Mkuu wa Chuo
cha Ualimu Marangu Moshi kuhusu sababu zilizofanya mwanao huyu achelewe
kuripoti chuoni hadi ushitakiwe na kufikishwa hapa mbele ya mahakama
hii. Mwanao alitakiwa kuripoti Agosti 21 mwaka huu, lakini
umemchelewesha kwa kutaka ashindwe kwenda chuoni kwa nia ya kutaka
umuoze anavyodai binti yako huyu hapa mbele ya mahakama hii.” alisema
Hakimu Migera na kumtaka kuhakikisha anaripoti keshokutwa akiwa na
vielelezo vya kulipa ada.
Hata hivyo,
mzazi huyo alisema alikwenda mahakamani hapo akiwa na Shilingi 200,000
kama nauli na matumizi ya bintiye aweze kwenda chuoni, hivyo ameahidi
kujipanga zaidi.Nje ya mahakama, Kinogo alisema: “Nilifika hapa na
Shilingi 200,000 nimpe binti yangu huyu aende huko chuoni kwani naona
mambo ya kuolewa yameshaharibika.”
Post a Comment