NCHI za Afrika Mashariki Tanzania zimehimizwa kuiga mfano wa Kenya
katika kuweka Sera na Sheria kali ya kudhibiti unywaji mbaya wa pombe
wenye madhara makubwa kwa familia na taifa.
Ushauri huo umetolewa na Wajumbe Washiriki wa Mkutano wa Tatu wa
Kimataifa kuhusu pombe katika Kanda ya Afrika Mashariki wenye mada kuu
‘pombe ni tatizo chukua hatua sasa’ wametoa ushauri huo mjini Arusha
baada ya kuelezwa mafanikio ambayo Kenya imepata kutokana na sheria ya
kudhibiti unywaji pombe iliyopitishwa na Bunge la nchi hiyo mwaka 2010.
Mkurugenzi mkuu wa TAMWA, Ananiliea Nkya |
Mambo yaliyozingatiwa katika sheria hiyo ya Kenya ni pamoja na
kudhibiti usalama na ubora wa viwango vya kilevi kwenye pombe na unywaji
holela. Sheria hiyo inapiga marufuku utengenezaji wa pombe kwa kutumia
vitu haramu kama vile kemikali ya methanol, mitishamba na kinyesi cha
wanyama.
Kwa mujibu wa sheria hiyo mtu akipatikana na hatia ya kutengeneza
pombe kwa kutumia vitu hivyo hatari vya kuongeza kiwango cha ulevi
adhabu yake ni kifungo jela miaka mitano na faini ya shilingi milioni 10
za Kenya ambazo ni sawa na shilingi milioni 170 za Tanzania au adhabu
zote mbili.
Kuhusu kudhibiti unywaji pombe holela, sheria hiyo ya Kenya, tofauti
na hapo awali, maalum hivi sasa ni kuanzia saa 11 jioni hadi saa tano
usiku. Kadhalika inapiga marufuku watoto kwenda baa au kunywa pombe.Mtu akipatikana na hatia ya kukiuka taratibu za unywaji adhabu yake ni
kifungo cha miaka miwili hadi mitano jela au faini ya shilingi 100,000
za Kenya ambazo ni sawa na shilingi milioni moja na laki saba za
Tanzania au vyote viwili.
Mwandishi wa TAMWA anayehudhuria mkutano huo amemnukuu Afisa Mtendaji
Mkuu wa taasisi ya Serikali iliyopewa mamlaka ya kuratibu utekelezaji
wa vifungu vya sheria hiyo (NACADA), Dakta William Okedi akisema
utekelezaji wa sheria hiyo umekuwa na mafanikio makubwa.
Dakta Okedi amesema sheria hiyo ya kudhibiti ulevi nchini Kenya
imekuwa na mafanikio kwa sababu kabla ya kutungwa kulifanyika utafiti
ambao ulibaini kuwa pombe nyingi za kienyeji zinatengenezwa kwa kutumia
vitu ambavyo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Mafanikio hayo ni kufungwa kwa karibu nusu ya vilabu vya pombe,
kupungua kwa idadi ya vijana wenye umri mdogo wanaokunywa pombe na
kuongezeka kwa uzalishaji kutokana na watu kutumia muda mwingi kufanya
kazi badala ya kulewa pombe.
Akitoa ushuhuda kuhusu mafanikio ya sheria hiyo, Mbunge John Mututho
alisema eneo la Kahuno Murang’a Central Kenya wakulima wa kahawa kwa
muda wa miaka kumi mfululizo walikuwa wanapata tani za Kimarekani 57 kwa
mwaka lakini katika kipindi cha mwaka 2011/2012 wamepata tani 178
katika ukubwa wa ardhi ile ile ambayo wanalima.
Mbunge huyo ambaye ndiye aliyepeleka Muswada binafsi bungeni ambao
uliwezesha kutungwa kwa sheria hiyo amesema utafiti umeonyesha pia
kwamba viwanda vya pombe Kenya vimeongeza faida kwa wastani wa asilimia
24 kwa sababu watu wengi wameacha kunywa pombe haramu badala yake
wanakunywa bia.
Kadhalika amesema familia zimepata amani na maendeleo kwa sababu
wanaume wengi tofauti na zamani ambapo walikuwa wanakesha vilabuni, sasa
wanarejea nyumbani mapema .Vile vile makosa ya jinai kama vile ubakaji
na mauaji yamepungua kwa zaidi ya asilimia 50.
Mututho ambaye ni mbunge wa jimbo la Naivasha nchini Kenya amesema
sheria hiyo inakusudiwa kurejeshwa tena bungeni Septemba 26, 2012 ili
kuongezewa makali kupiga marufuku unywaji pombe siku mbili kabla ya siku
ya uchaguzi na siku moja baada ya uchaguzi kuzuia ulevi wa pombe
kuharibu uchaguzi. Nchi za Afrika Mashariki zinajumuisha Burundi,
Rwanda, Uganda, Kenya na Tanzania.
*Habari hii ni Kwa Hisani ya TAMWA
Post a Comment