Mwandishi Wetu, Tabora
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
amemlipua Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akidai kuwa hana ubavu
wa kupambana na rushwa kwa kuwa chama chake kiliingia madarakani kwa
rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
Akihutubia katika
mikutano ya hadhara katika Vijiji vya Kata za Kiloleli na Ipole,
wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora, Dk Slaa alisema rushwa inazidi kukua
siku hadi siku nchini.
Alidai kwa kuwa viongozi wa CCM waliingia madarakani kwa njia ya rushwa ndiyo maana hawawezi kulimaliza tatizo hilo.
Dk Slaa alisema Rais Kikwete anatania kuhusu tatizo la rushwa kwa kuzungumza tu majukwaani, huku akiwalinda washirika wake.
Alisema
kama Rais Kikwete angekuwa mkweli angewakamata wamiliki wa Kampuni ya
Kagoda ambao ni watuhumiwa wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje
(Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alidai kuwa ameshindwa kuwakamata kwa sababu fedha hizo ndizo zilitumika kumwingiza madarakani katika uchaguzi wa 2005.
Katibu
mkuu huyo wa Chadema alisema vitendo vya rushwa vilivyojitokeza katika
uchaguzi wa viongozi wa CCM ni kielelezo tosha kwamba, chama hicho
hakina uwezo tena wa kupambana na rushwa.
"Tunawaambia CCM kuwa chama chao kimeoza kuanzia juu hadi chini, sasa mafisadi wameshika hatamu ndani ya chama hicho,” alisema.
Dk
Slaa alisema, “Hivi Watanzania tunahitaji ushahidi wa namna gani ili
kubaini uozo katika CCM na tuungane kukiondoa madarakani.”
Aliongeza,
"Wakati chama hicho kinatopea kwenye lindi la rushwa na ufisadi,
kiongozi wake mkuu ambaye Rais Kikwete naye anaishia kulalamika tu.”
Slaa alisema Rais Kikwete angekuwa na nia ya dhati
katika
kupambana na rushwa, angeifanyia kazi orodha ya majina 11 ya watuhumiwa
wakubwa wa ufisadi iliyotolewa katika Viwanja Mwembeyanga, jijini Dar
es Salaam Septemba 2007.
Alisema kuendelea kulalamikia kuhusu
rushwa bila kuchukua hatua yoyote, kunawashangaza wananchi ambao wanaona
hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) bora
ingevunjwa.
Hatuwezi kukubali taifa liangamie kwa sababu Rais anashindwa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi na wala rushwa.
Rais Kikwete
Hivi
karibuni Rais Kikwete wakati akifungua Mkutano Mkuu wa UVCCM mjini
Dodoma aliwaasa vijana wa chama hicho kutojihusisha na rushwa hatua
ambayo inaonekana sawa na kumpigia mbuzi gitaa.
Katika hotuba yake, Kikwete aliwaambia 'watajuta', ikiwa watachagua viongozi kwa misingi ya rushwa.
“Nawaambieni,
mkifanya mchezo ipo siku mtakuja kujuta maana mkishamchagua kiongozi
asiyefaa, mtalazimika kuwa naye huyohuyo hadi 2017, na kama Waswahili
wanavyosema majuto ni mjukuu,” alisema Kikwete.
Kauli hiyo ya
Kikwete ni kama aliyoitoa wakati akiahirisha Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya
Wanawake ya chama hicho (UWT)aliposema kuwa, CCM kinakwenda kubaya
kutokana na chaguzi zake kugubikwa na vitendo vya rushwa.
Kikwete
alisema siku zilizopita vitendo hivyo vilikuwa vikihusishwa zaidi na
wanaume, lakini akaeleza kushangazwa kwake na makundi ya kina mama nao
kuanza kujihusisha na rushwa.
Msekwa alonga
Makamu
Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa amezidi kuwasha moto ndani ya
chama hicho, baada ya kuvitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua za
kisheria wote waliotuhumiwa na rushwa katika uchaguzi wa ndani wa chama
hicho.
Kauli ya Msekwa imekuja ikiwa ni siku tatu baada ya kuwapo
kwa tuhuma za rushwa kutawala ndani ya uchaguzi wa Jumuiya ya Umoja wa
Vijana( UVCCM) na ule wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) zilizomalizika mjini
Dodoma.
Hata hivyo, kauli ya Msekwa inapingana na mawazo ya
makada wengi wa chama hicho wanaopinga rushwa wakisema kuwa, uongozi wa
chama unapaswa kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kweli ya kukiokoa chama
hicho ambacho hata Mwenyikiti wake, Rais Jakaya Kikwete alisema; “Rushwa
inatupeleka kubaya.”
Matokeo ya uchaguzi wa UVCCM ndiyo
yaliyozua tafrani kubwa kiasi cha baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa
jumuiya hiyo, kumsindikiza kwa mabango Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein baada ya kufunga mkutano huo.
Mabango hayo
yaliyokuwa na ujumbe wa kulalamikia mchakato wa uchaguzi kwamba
ulitawaliwa na rushwa, yalitanguliwa na kauli za walalamikaji ambao
tayari walikuwa wamewaambia waandishi wa habari kuwa wanamwomba Rais
Kikwete atengue matokeo hayo, ikiwezekana katika muda wa saa 24.
Akizungumza
jana asubuhi jijini Dar es Salaam, Msekwa alisema; "Kwanza nataka
kusema, wote wenye malalamiko walitakiwa kuyapeleka kwenye ngazi husika,
nimesikitishwa na hao ambao wamempa Rais saa 24 kufuta matokeo ya
uchaguzi”.
"Hizi ni fujo tu, wapi kuna mamlaka inayomwamuru Rais
au mwenyekiti kufanya hivyo, wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni za
uchaguzi... Hivi ni kifungu gani cha sheria kinachosema hivyo?," alihoji
Msekwa.
Msekwa ambaye alikuwa akihojiwa na Kituo cha Radio One
jana alisema kuwa kuna kanuni na taratibu mbalimbali za kuwasilisha
malalamiko, ndipo hoja zinaweza kusikilizwa na kupata mafanikio.
Akizungumzia
suala la rushwa ndani ya uchaguzi, alisema ni tatizo lililosambaa
kwenye jamii na ni kasoro na upungufu uliokuwa sugu.
"Rushwa
imesambaa kila mahali, polisi kuna rushwa, mahakamani rushwa, lazima
tukemee, nimewahi kuzungumzia hili la rushwa kuwa ni kosa la jinai,
lakini bado nasema kukemea haitoshi.
Waaswa kukataa mizigo mizito
Naye
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk akiwaambia wananchi
wa kata hizo kwamba ugumu wa maisha unaowakabili unatoka na sera mbaya
ya chama tawala.
Mbarook alisema CCM ya Mwalimu Julius Nyerere
iliyokuwa ikishughulikia matatizo ya watu sasa haipo tena, badala yake
wameichukua mafisadi.
Alisema chama hicho sasa kimebaki kuwa adui wa kuminya haki za raia.
"Miaka
mingi sisi tumewabeba, tena wanatumia maneno yaleyale ya ‘Mzigo mzito
mpatie Mnyamwezi akubebee’. Kwa hiyo Watanzania wa Tabora kwa muda mrefu
tumekuwa tukiibeba CCM wakati wenzetu mikoa mingine wameshaikataa.
Aliongeza,
Sasa ni wakati mwafaka kuanza kuutua huu mzigo, umetuchosha,” alisema
huku akimpigia debe mgombea wa Chadema, David William katika
kinyanganyiro cha udiwani kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika kesho
katika eneo hilo.
Chanzo Gazeti la mwananchi
Post a Comment