Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Ramadhan Manento akionyesha taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari wa wa Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mahfoudha.A. Hamid akijibu moja ya Swali kutoka kwa Mwandishi wa Habari (hayupo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari wa wa Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa. (Picha: Mwanakombo Jumaa-MAELEZO)
MUHTASARI WA TAARIFA
YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YA UCHUNGUZI WA TUKIO
LILILOPELEKEA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI KILICHOTOKEA SEPTEMBA 2, 2012
KIJIJINI NYOLOLO, WILAYA YA MUFINDI, MKOANI IRINGA
- UTANGULIZI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
ni idara huru ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha
129(1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na
Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka
2001. Jukumu kubwa la Tume ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za
binadamu nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo Tume imepewa mamlaka ya
kupokea malalamiko (kwa njia mbalimbali) kutoka kwa mtu yeyote au
kuanzisha uchunguzi wake yenyewe endapo itaona kuna uvunjifu wa haki za
binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Kwa
kuzingatia majukumu hayo, Tume ilianzisha uchunguzi wake yenyewe baada
ya vyombo vya habari kutoa taarifa ya tukio la kifo cha Daudi Mwangosi.
Tume iliunda timu ya watu watatu iliyoongozwa na Mhe. Kamishna Bernadeta
Gambishi akisaidiwa na maafisa wawili, Bwana Gabriel Lubyagila na Bwana
Yohana Mcharo. Timu hiyo ilifanya uchunguzi wake kuanzia tarehe 13-19
Septemba, 2012.
Katika uchunguzi uliofanywa, Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo
basi, Tume ilitilia maanani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
sheria mbalimbali za nchi na mikataba ya kimataifa na ya kikanda
inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.
Kwa
kuzingatia matakwa ya sheria ya Tume Na. 7 ya mwaka 2001, baada ya
uchunguzi huo kukamilika, Tume imeandaa taarifa yake na kuiwasilisha
kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Taarifa ya uchunguzi wa Tume imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo ni:
- Maelezo ya viongozi, watendaji na wananchi waliohojiwa
- Uchambuzi wa taarifa/vielelezo vilivyopokelewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu
- Matokeo ya uchunguzi
- Maoni na mapendekezo.
Kwa kuwa
tukio la kifo cha Daudi Mwangosi liligusa hisia za jamii, Tume imeona
ni vyema kukutana na wawakilishi wa vyombo vya habari ili kutoa taarifa
yake.
2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
Katika uchunguzi wake Tume imebaini kuwa:
- Tarehe 02/09/2012 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi (OCD) kufanya mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe 01/09/2012 Kamanda wa Polisiwa Mkoa wa Iringa (RPC), alizuia CHADEMA kufanya mikutano iliyoruhusiwa na OCD ambaye ni “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.
- Viongozi wa CHADEMA walikuwa na mazungumzo na Mkuu wa Polisi Mkoa Upelelezi (RCO) na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.
- Msajili wa vyama vya siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa.
- Wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, RPC alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe; na kuwa wafuasi wa CHADEMA walipingakukamatwa kwa viongozi wao.
- RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
- Baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo; na kuwa marehemu Daudi Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwaalipigwa bomu na kufa hapo hapo.
- Daudi Mwangosi aliuwawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.
- Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo Mwandishi wa Habari wa Nipashe, Bwana Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Bibi Winnie Sanga na Mkuu wa Kituo cha PolisiMufindi, Asseli Mwampamba aliyekuwa akifanya jitihada zakumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.
Kutokana
na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo cha
Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji
wa misingi ya utawala bora.
2.1 Uvunjwaji wa Haki za Binadamu
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu
(Universal Declaration of Human Rights of 1948),
Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa (International
Covenant on Civil and Political Rights of 1966) na Mkataba wa mataifa ya
Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and
Peoples Rights of 1981), Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi
limevunja haki zifuatazo:
- Haki ya kuishi,
- Haki ya kutoteswa na kupigwa,
- Haki ya usawa mbele ya sheria na
- Haki ya kukusanyika na kutoa maoni.
CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu. Chini ya sheria ya vyama vya siasa (Cap. 258 RE.
2002), vyama vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano
na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa “Afisa wa
Polisi” wa eneo husika. Baada ya taarifa kutolewa chama husika
kinatakiwa kipewe ulinzi na “security agencies” (mawakala wa usalama).
2.2 Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora
Ili pawepo
utawala bora mamlaka zote za serikali ni lazima zifuate utawala wa
sheria. Uchunguzi umebaini kuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake
alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a)
na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa
Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa
“Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika. Kwa maana hiyo amri
aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na
mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka,
hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Aidha,
hatua ya Msajili wa vyama vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia barua
viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu
ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa
ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka 2002
inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia
ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) Kifungu cha
11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake
bila ya kuingiliwa.
Ibara ya
8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelezea kwamba
Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na Haki ya Kijamii,
aidha ibara 18(b) na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya
kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari) na haki ya kutoingiliwa katika
mawasiliano yake. Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la
Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa waandishi wa habari na
wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya shughuli zao za kupata
habari na za kisiasa. Huu ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa
kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha uhuru wa habari.
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
Kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001 Kifungu cha 15(2)(c) na 28 Tume inapendekeza yafuatayo:
- Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wamisingi ya utalawa bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao. Aidha, kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
- Viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa navyombo hivyo bila shuruti. Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
- Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi auupendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huoChama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampeni huko Zanzibar. Aidha, rai ya Msajili wa vyama vya siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo.
- Demokrasia ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
- Elimu ya vyama vya siasa na sheria ya Polisi kuhusu vyama vya siasa itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.
4.0 HITIMISHO
Jukumu
la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania, mkulima na
mfanyakazi, viongozi wa serikali na watumishi wa umma wote
wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli wakati wanapotekeleza majukumu yao ya
kila siku. Tume inatoa wito kwa watanzania wote kuheshimu haki za
binadamu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya utalawa bora. Kwa kufanya
hivi Taifa letu litaendelea kuwa na amani na utulivu. Tume inatoa rai
kwa jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa
raia bila kutumia jazba.
Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala.
.............................. ......................
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri R. Manento
MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Post a Comment