WAKRISTO GEITA WACHARUKA, WADAI HAWATAVUMILIA KUCHOMEWA MAKANISA
Habari imeandikwa na MAGRETH CHABA
UMOJA
wa Makanisa ya Kikristo ya Katoro wilayani Geita na Buseresere wilayani
Chato, mkoani Geita umecharuka na kulaani kitendo cha hivi karibuni
kilichofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam cha kuchoma moto
Makanisa na kuharibu mali za Wakristo.
Kitendo hicho
kilisababisha vurugu zilizotokea Oktoba 12 mwaka huu, huko Mbagala
Kizuiani jijini Dar es Salaam ambapo Makanisa saba yalichomwa moto
kutokana na kitendo kinachodaiwa na mtoto mwenye umri wa miaka 14
kukojolea Qu’ran.
Umoja huo umetoa tamko kuhusiana na kitendo
hicho katika mkutano wa uliofanyika juzi mjini Katoro na kuwakutanisha
waumini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na viongozi wao.
Akitoa
tamko hilo, mwenyekiti wa umoja huo, Mchungaji Joseph Mwanzalima Hewa,
alisema serikali ikishindwa kudhibiti matukio ya vurugu za baadhi ya
Waislam kujichukulia sheria mkononi kutokana na udini, Taifa halitakuwa
na amani.
Alisema kuna hatari ya Taifa, likaingia katika umwagaji
wa damu kwani kwa Wakristo kuzidi kupumbazika kwa kuharibiwa mali zao
ni jambo lisilovumilika.
Hewa alisema zaidi ya Biblia 50
ziliwahi kuchomwa moto lakini Wakristo hawakuchukua hatua zozote dhidi
ya wahusika wala hakuna Msikiti uliochomwa moto na hakuna vurugu
zilizotokea na hivyo kuhoji uhalali wa baadhi ya Waislam kuiweka nchi
kwenye rehani ya vita ya kidini.
Alisema Serikali
inapaswa kuingilia kati kukomesha matukio hayo yanayofanywa na baadhi ya
makundi ya waumini wa dini ya Kiislam ili nchi iendelee kuwa kisiwa cha
amani.
Aidha, alisema kama Serikali itashindwa kudhibiti matukio
hayo, hawatavumilia kuendelea kuharibiwa Makanisa yao na kudai kuwa
wako tayari kufa wakitetea haki zao.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa
waliohusika katika matukio hayo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za
kisheria akiwemo kinara wa kikundi cha Uamsho Zanzibar, Sheikh Farid
Hadi Ahmed.
“Serikali imekuwa ikiwakumbatia Waislam, sasa
tunasema yatosha. Hatuwezi kuona mali zetu zinaharibiwa. Kama itakuwa
kimya katika hili nchi itaingia katika vurugu kubwa na vita kutokana na
udini ulioanza kujipenyeza,” alisema Hewa.
Naye aliyewahi kuwa
mwenyekiti wa umoja huo, Isaya Ikili alisema anasikitishwa na watendaji
wa Kata pamoja na viongozi wa Serikali kushindwa kuhudhuria katika
mkutano huo licha kupewa mwaliko ili kujua matamko yao.
Alisema
wako tayari kupambana na maadui wao wanaoharibu Makanisa yao na kwamba
polisi wasiingilie vurugu hizo kama serikali itashindwa kuyadhibiti.
Post a Comment