WAKATI serikali ikishindwa kuwataja vigogo walioficha mabilioni
ya fedha nchini Uswisi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto
Kabwe, anatarajia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano wa tisa
unaotarajiwa kuanza wiki ijayo mjini Dodoma, kutaka serikali irejeshe
fedha hizo.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, amesema tayari hoja hiyo imeshapata baraka za Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Mbunge huyo wa CHADEMA alisema hayo jana wakati wa akifunga mkutano wa
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Nanjarareha, wilayani
Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika leo, CHADEMA imemsimamisha,
Frank Salakana.
Alisema sh bilioni 349 zilizofichwa Uswisi na baadhi ya vigogo wa
serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), lazima zirejeshwe nchini, huku
akimtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), Edward Hosea, kueleza umma barua aliyoituma nchini humo kwa
ajili ya kashfa hiyo ilikuwa na lengo gani.
Alisema barua ya Dk. Hosea imesababisha ugumu wa upatikanaji wa
taarifa za mabenki ya nchini Uswisi ambayo yameshindwa kutoa ushirikiano
kwa kamati inayofuatilia kashfa hiyo.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wanachama wa CHADEMA waliofurika
kusikiliza mkutano huo, Zitto alisema wizi wa mabilioni hayo umetokana
na kuporomoka kwa maadili ya viongozi nchini ambao wengi wanajali
zaidi masilahi binafsi badala ya umma.
Mbunge huyo machachari wa CHADEMA, alisema kuna haja kama taifa
kurejesha maadili ya uongozi kama enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere ili
viongozi wachague kitu kimoja, kati ya biashara na siasa.Alisema CHADEMA imepania kuhakikisha mabilioni hayo yanarejeshwa ili
yaweze kutumika kuwasaidia Watanzania katika kujenga na kuboresha
miundombinu ya barabara, maji na afya.
Aliwataka viongozi walioficha mabilioni hayo kujitokeza mapema na kueleza jinsi walivyozipata badala ya kusubiri kuumbuliwa.
“Nawataka viongozi waliohusika wajitokeze wenyewe, waeleze
walivyozipata na kisha wazirejeshe nchini, vinginevyo patachimbika,
kwani nitahakikisha kama chama tunashirikiana na Benki ya Dunia
kuhakikisha fedha hizo zinarudi nchini,” alisema Zitto.
Alisema CHADEMA inapigania fedha hizo zirejeshwe kwani zimetokana na
wizi wa rasilimali za Watanzania kupitia mikataba mibovu ya mafuta na
wizi wa madini na nyingine.
Katika ripoti ya Swiss Central Bank, iliyotolewa hivi karibuni,
inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 barani Afrika ambazo
vigogo wake wa kibiashara, kitawala na kisiasa wameficha kwa siri
mabilioni ya fedha katika mabenki ya Uswisi.
Nchini nyingine za Afrika zilizoficha fedha hizo ni Kenya, Uganda,
Zimbabwe, Misri, Shelisheli, Afrika Kusini, Rwanda, Sierra Leone,
Somalia na Sudan.
Kwa upande wa Tanzania, mapesa ambayo yamefichwa huko ni dola milioni 196.87, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 315.5!
Hebu jiulize; mapesa haya tuliyoibiwa yangetusaidia kiasi gani kama
yangerejeshwa nchini na kutumbukizwa kwenye miradi ya kuboresha huduma
za jamii?
Pia jiulize swali jingine: Je, hata baada ya Benki Kuu ya Uswisi
kuturahisishia mambo kwa kututobolea ukweli kwamba tumeibiwa, na kwamba
wezi wetu wameficha hizo fedha nchini mwao, watawala wetu wana dhamira
ya kuanzisha mchakato ili wahusika wafikishwe mahakamani na fedha hizo
zirejeshwe nchini?
Post a Comment