Ni Wilfred Moshi.
Amekuwa Mtanzania wa kwanza kufika kilele cha mlima mrefu kuliko yote duniani.
Na Freddy Macha
kwa ushirikiano
wa Urban
Pulse
KIJANA Wilfred Moshi, ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania
wa kwanza kupanda mlima Everest - mlima mrefu kuliko yote duniani.
Huyu ni “Mbongo” wa kawaida tu, mzoefu wa kufanya
kazi ya upagazi ya kuwahudumia watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro.
Hivi karibuni, Moshi alialikwa nchini Uingereza
kutembelea shule mbalimbali za Scotland. Alikuwako kwa majuma matano na kuweza
kukutana na takribani wanafunzi 5,000.
Wanafunzi walitaka kufahamu namna alivyopanda
mlima Everest wenye mita 8,848 (futi 29, 029). Watu 4,000 wamewahi kupanda
mlima huu mgumu kukwea kuliko yote duniani, tangu Edmund Hillary na Sherpa
Tenzig Norgay walipofika kileleni mwaka 1953. Watu 200 kati ya waliokwea mlima
huo walifariki.
Mwaka huu wanne wameshafariki wakijaribu shughuli
hii inayochukua miezi miwili na kugharimu
Dola 100,000 (Shilingi milioni 157,500,000). Hapa, linganisha na Mlima
Kilimanjaro unaopandwa kwa siku tano na kwa gharama (ikiwepo ya vifaa husika),
Dola 2,000 (Shilingi milioni 3.1).
Wilfred Moshi ni Mtanzania wa kwanza na Mwafrika
wa tatu kufikia kilele cha kitendawili hiki cha “Chomolungma” – jina la wenyeji
kabla mlima huu haujabandikwa jina la Everest, enzi za ukoloni wa Uingereza. Alikanyaga kileleni tarehe 19 Mei mwaka huu.
Wilfred alizaliwa mwaka 1979. Alimaliza Kidato cha
VI shule ya Kilimanjaro Boys. Amekuwa akipanda Mlima Kilimanjaro tangu angali
bado shuleni – akiwa na miaka 19.
Mara baada ya kuwasili Edinburgh, Scotland, Wilfredalikaribishwa bungeni; akakutana na
Waziri wa Sheria, Mheshimiwa Kenneth MacAskill na viongozi wengine. Safari hii ilikirimiwa
na shirika la “Twende Pamoja” lililoanzishwa na Mike Knox miaka 30 iliyopita.
“Twende Pamoja” limejenga ushirikiano kati ya
wanafunzi wa Scotland na shule 34 za Tanzania.
Ni moja ya mashirika, watu binafsi na wafadhili mbalimbali duniani waliochangia
fedha za kumwezesha Moshi kupanda mlima Everest.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa
Peter Kallaghe, naye alisafiri toka London kumtembelea Wilfred Moshi na kumpa
heko. Umbali wa London hadi Scotland ni kama Dar es Salaam na Kigoma.
Lakini kwanini Moshi anahusudu kupanda milima.
Yeye anasema, kwanza lengo lake lilikuwa kutimiza
ndoto yake ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda Everest. Ameitimiza.
Pili, upandaji milima ni moja ya njia zinazoweza
kusaidia kujenga jamii kwa misaada na fadhila za mashirika yasiyo ya kiserikali
(NGO). Tujiulize vipi alisaidiwa na watu wengi kuchanga fedha nyingi kiasi
hicho.
Tatu, Moshi amethibitisha ukiwa na moyo na
jitihada unaweza kufanya lolote. Ushujaa na ushupavu wake utasaidia
kuwahamasisha Watanzania kuwa, ukitaka kufanya jambo lolote lile, unaweza ili
mradi uwe na moyo na nidhamu.
Mpanda milima mashuhuri, Mike Hamill, aliyekwishafika
vilele vyote vya milima mikubwa saba duniani, anasema katika kitabu chake kipya
– Climbing Seven Summits – kwamba wapanda milima ni watu wenye moyo wa
kufikia malengo na kufanikiwa katika maisha yao.
Akiwa Uingereza, Moshi alipanda mlima wa Ben Nevis, mrefu kuzidi yote katika nchi hii – wenye
mita 1,344 (futi 4, 409).
Baada ya kuimudu milima mitatu, sasa Wilfred Moshi
ameazimia kupanda milima katika mabara yote saba duniani. Anasema amebakisha
milima ya Aconcagua (Marekani ya Kusini ), Kosciuszko (Australia), Vinson
Massif (Antarctica), McKinley (Alaska) na
Elbrus (Urusi).
Mungu ambariki Mtanzania huyu mwenye hamasa na
anayetuletea sifa.
Soma habari zaidi:
http://wilfredmoshi.wordpress.com/
Post a Comment