YEYE, WENZAKE WANNE WANASHIKILIWA POLISI IRINGA.
ASKARI
watano wa Jeshi la Polisi akiwamo anayetuhumiwa kumlipua kwa bomu
Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, marehemu
Daud Mwangosi wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo mkoani
Iringa.
Taarifa ya kukamatwa kwa askari hao imekuja siku moja
baada ya kubainika kwamba, askari kadhaa walioendesha operesheni dhidi
ya wafuasi wa Chadema mkoani Iringa na kusababisha kifo cha Mwangosi
walitoka mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro.
Taarifa za uhakika
zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na baadhi ya askari
polisi mkoani Iringa na Makao makuu jijini Dares Salaam, zilisema kuwa
polisi hao, akiwamo yule aliyeonekana kwenye picha za video na za mnato
akimlipua kwa mtarimbo wa bomu la machozi (jina tunalo) wamekamatwa na
kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Iringa.
Kwa mujibu
wa habari hizo, askari hao walikamatwa Jumatatu wiki hii ikiwa ni siku
moja baada ya mauaji hayo yanayoaminika kufanywa na Jeshi la Polisi kwa
kutumia askari wa mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani.
"Hivi sasa
(jana mnamo saa 8:30 mchana) ninapozungumza na wewe bado hao askari
wanaendelea kuhojiwa. Wako watano," alisema askari polisi mmoja
aliyekuwa karibu na chumba wanachoshikiliwa askari hao.
Chanzo hicho kilieleza kuwa askari aliyemuua Mwangosi alionyesha kusikitikia tukio hilo akisema hakukusudia kufanya hivyo.
"Anasema
ni kwamba, yeye mwenyewe hakupenda kuona tukio hilo likitokea.
Aliniambia kuwa kifo cha mwandishi huyo kimemsikitisha sana, na
nilipomuuliza nini hasa kilitokea, alisema; ahh hilo niache nitaeleza
nitakapohojiwa," kiliongeza chanzo kilichokuwa karibu na askari huyo.
Afisa
Upelelezi wa Ukoa wa Iringa, (RCO), SSP Nyigesa Wankyo hakuthibitisha
kuwashikilia askari hao, badala yake akataka kazi hiyo ifanywe na polisi
Makao Makuu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso
hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo na simu yake ya mkononi haikuwa
inapatikana hadi tunaenda mitamboni.
Naye Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kamishna Robert Manumba alisema;
"Wakati ukifika mtaambiwa. Kwa sasa muda haujafika, subirini uchunguzi
uendelee, mtaambiwa".
Polisi aliyelipuliwa mguu anena
Katika
hatua nyingine, mmoja kati ya askari waliokuwapo wakati tukio zima
lililosababisha kifo cha Mwangosi ambaye alijeruhiwa katika mguu wake wa
kushoto na kupoteza fahamu kabla hajafikishwa hospitali ya wilaya ya
Mufindi, mkoani Iringa anaendelea vizuri na matibabu.
Akizungumza
na waandishi wa habari walipotembelea majeruhi waliolazwa katika
hospitali hiyo, Aseri Mwampamba alisema alipoteza fahamu baada ya
kujeruhiwa katika mguu wake wa kushoto.
"Ni kweli nilikuwa eneo la
tukio baada ya kuona hali ya amani katika eneo hilo imekuwa si nzuri,
wanachama hawakutaka kuondoka eneo la mkutano. Wakaanza kufanya vurugu
na kusababisha nikajeruhiwa mguuni kama unavyoona," alisema Mwambapa.
Alipotakiwa
kueleza majeraha hayo aliyapataje, askari huyo alisema hata yeye
hafahamu isipokuwa akiwa amesimama alishangaa kuona kitu kikitua mguuni
na kwamba anadhani kilitoka chini na kutua katika mguu wake wa kushoto.
Hata
hivyo, picha za mnato zilizochapishwa kwenye magazeti mbalimbali nchini
baada ya tukio hilo, zimeonyesha kuwa mara ya mwisho Mwampamba
alionekana amekumbatiwa na marehemu Mwangosi huku askari mmoja alilenga
mtarimbo wa kufyatua mabomu ya machozi.
Jaji Ihema aja juu
Mwenyekiti
wa Kamati ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi, Jaji Mstaafu Stephen
Ihema amesema katika historia yake ya utumishi wa umma hajawahi
kushindwa kazi.
Alisema amesikitishwa na kauli za kubeza uteuzi wake zilizotolewa na viongozi wa Chadema, waliopinga uteuzi wake.
Huku
akitumia kitabu cha Bibilia kutetea utendaji wake, Jaji Ihema alisema
amesikitishwa na matamshi hayo ambayo yanavunja moyo na hayakupaswa
kutolewa.
“Haya ni maoni tu ya mtu ambayo yanaweza kuwa sahihi kwa mtoaji na yakawa siyo sahihi kwa upande wa mwingine.
“Pili,
napenda niseme kwamba hayo maoni is not biblical conclusive(msaafu
ambao hautiliwi shaka)” alisema Jaji Ihema alipoulizwa na gazeti hili
jana.
Pamoja na kukataa kujibu tuhuma hizo, Jaji Ihema
alisisitiza kwamba, anafahamu vema siasa za nchi hii na kuwataka
wanaohoji utendaji wake wafuatilie rekodi yake ya nyuma.
Wakati
akiwasilisha msimamo wa Chadema kupinga uteuzi wa jaji huyo kuongoza
kamati hiyo, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama
hicho, Tundu Lissu alidai kuwa kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Ihema hana
uwezo na kazi ya ujaji na mpaka sasa alikuwa ana kesi 300 ambazo
anashindwa kuzitolea uamuzi.
Lakini, Jaji Ihema amepuza tuhuma hizo akisema; “Haya ni matamshi ya kisiasa tu, na mimi nazijua siasa za Tanzania”.
Aliongeza;
“Ninachoweza kusema mimi ni kwamba, nimeteuliwa kuwa kiongozi wa kamati
hii, na ukiniuliza mimi nimepokeaje nitakuambia, this is not any issue
(yaani siyo jambo la kujadiliwa sasa). Kama unataka kujua vigezo vipi
vilivyotumika nitakuambia nenda kwa Waziri nadhani yeye anajua, alipokea
ushari wa watu gani na baadaye akafikia uteuzi huo.”
Katibu WAPC aonya
Wakati
huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC),
Christopher Conybeare, amelaani mauaji ya mwanahabari Mwangosi,
yanayodaiwa kufanywa na polisi na kuagiza hatua za haraka zichukuliwe
dhidi ya wahusika wa tukio hilo.
Conybeare alisema hayo jana
katika hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Baraza la Habari
Tanzania(MCT), kwa ajili ya WAPC na kusisitiza kuwa uchunguzi wa tukio
hilo hauna budi kufanyika haraka iwezekanavyo ili hatua zichukuliwe
mapema kutokana na unyeti wa sekta ya habari duniani.
Katibu
huyo ambaye yupo nchini kwa ajili ya mkutano mkuu wa WAPC pamoja na
wajumbe 15 kutoka mabaraza mbalimbali ya habari duniani, alisema tukio
hilo linaweza kuiharibia sifa Tanzania kwani ni moja ya nchi zenye
taswira nzuri duniani katika tasnia ya habari na kuongeza kuwa
wanahabari wanapouwawa, demokrasia nayo hufa.
“Mauaji ya
mwandishi nimeyasikia kwa sababu nipo hapa nchini tangu Agosti 29, na ni
jambo ambalo linatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa haraka kwani linaharibu
maana ya demokrasia,” alisema Conybeare.
Conybeare aliimwagia sifa
MCT na kusema kuwa ni miongoni mwa mabaraza makini duniani ambalo
watanzania wanatakiwa wajisifie kwa kuwa nalo.
“Nimeifahamu MCT
mwaka 2003 katika moja ya mikutano ya WAPC, na tangu wakati huo tumekuwa
tukifanya kazi pamoja na nimefurahi sana mkutano huu kufanyika
Tanzania.” Alisema
Jukwaa la Katiba
Nalo Jukwaa la Katiba
Tanzania limesema Kamati ya watu watano iliyoundwa na waziri Nchimbi
kuchunguza kifo cha Mwangosi ni batili.
Akizungumza katika
mkutano na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa jukwaa
hilo Deus Kibamba alisema; “Kwa kuwa uchunguzi unaofanywa hauhusiani na
kilichomuua Mwangosi wala kundi gani limemuua, tunataka Kamanda wa
Iringa asimamishwe kazi kupisha uchunguzi, tume iundwe na rais na
kusimamiwa na mahakama.”
Alisema kuwa taarifa ya uchunguzi wa
tukio hilo ipelekwe bungeni na rais Kikwete ili wabunge wapate fursa ya
kuijadili na kutoa maamuzi ya kibunge.
“Kamati ya Nchimbi ni
batili kwa sababu mtu au kundi hawezi kuwa hakimu wa kesi inayomhusu
mwenyewe, isipofanyika hivyo, tume hiyo haiwezi kufanya kazi yake kwa
uhuru” alisema Kibamba na kuongeza:
“Athari za matukio ya mauaji
na fujo zinazosababishwa na jeshi la polisi kutawanya waandamanaji au
mikusanyiko ya watu kutaathiri hata mchakato wa kupatikana kwa katiba
mpya, kwa kuwa watu wataogopa kujitokeza”
Bavicha Iringa
Wakati
huo huo, siku moja baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John
Tendwa kutishia kukifuta Chadema kutokana na matukio ya vurugu katika
mikutano yake, Katibu mkuu wa Baraza Vijana Tanzania (Bavicha),
Deogratias Munishi amesema kabla ya kuifuta Chadema ni vyema akaanza
kukifuta Chama Cha Mapinduzi(CCM), kwa madai Serikali yake ndiyo chanzo.
Munishi
alitoa kauli hiyo, akijibu kauli ya Tendwa akisisitiza kuwa, ushahidi
wa tukio lililotokea Nyololo, Mkoani Iringa juu ya nani aliyeanzisha
vurugu na namna mauaji hayo yalivyotokea wanao na kwamba, wapo tayari
kuutoa wakati wowote kwa kamati huru na ya kuheshimika.
“Kama
Tendwa anataka kuifuta Chadema, basi aanze na CCM kwa sababu tunamjua
anatumwa na CCM kukiharibu chama chetu wakati Serikali yake kupitia
Jeshi la Polisi ndiyo yenye vurugu, na imekuwa ikisababisha mauaji mengi
ambayo, hakuna asiyeyajua,” alisema.
Alisema jeshi hilo halina
namna yoyote ya kukwepa, mauaji ya Mwangosi na kulitaka kuacha kutoa
kauli za kuwasingizia wananchi kwamba, kuna mmoja wao alirusha bomu
kuelekea kwa mwandishi huo, wakati wapo waliokuwa wakishuhudia na
wengine walichukua picha za tukio zima, wakiwemo waandishi wa habari
wenyewe.
“Polisi ndio ambao wamekuwa wakiua raia, ukiangalia picha
zilizopigwa eneo la tukio hakuna mtu asiyeona jinsi polisi
walivyomuadhibu Mwangosi kabla ya kumuua,” alisema Minishi
Habari hii imeandaliwa na George Njogopa, Florence Majani na Fidelis Butahe, Dar; Zulfa Shomari naFredrick Siwale, Iringa
Chanzo gazeti la Mwananchi
Post a Comment