WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, amekumbana na fadhaa ambayo
haikutarajia wakati alipotimuliwa katika maandamano ya waandishi wa
habari ya kupinga mauaji ya mwandishi mwenzao wa kituo cha televisheni
cha Channel Ten, David Mwangosi, wakati alipozuka bila mwaliko.
Huku
wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti, waandishi waliandamana
kuanzia kwenye ofisi za Channel Ten katikati ya jiji la Dar es Salaam na
kutembea hadi katika viwanja vya Jangawani lakini walipofika mwisho wa
maandamano yao walipigwa na butwaa baada ya kumkuta Waziri Nchimbi akiwa
wa kwanza kufika katika eneo hilo tayari kupokea maandamano.
Wakati
Nchimbi akijiandaa kuanza kuzungumza mbele ya wanahabari, upinzani
mkali ukazuka kwa waandishi dhidi ya kiongozi huyo wa serikali wakitaka
aondoke mahala hapo kwani maandamano hayo yalikuwa hayamuhusu.
"Atokee....
aondokee.... hatumtakiiii.... nani kamleta hapa?" yalikuwa ni baadhi ya
maneo yaliyokuwa wakitolewa kwa sauti kubwa kupinga uwapo wa waziri
Nchimbi mahala hapo.
Huku akizomewa, Waziri Nchimbi alijaribu
kuvumilia aibu hiyo kwa takriban dakika tano huku pengine akitumai
kwamba watamruhusu kuzungumza kilichompeleka mahala hapo.
Mwandishi
wa habari mkongwe, ambaye pia ni mwanasheria, Nyaronyo Kicheere,
alisogea mbele ya umati wa waandishi na kusimama jirani na alipokuwapo
waziri Nchimbi na kusema: "Tumeambiwa tunakuja hapa kwa ajili ya mkutano
wa waandishi wa habari na utapokewa na jukwaa la wahariri, inakuwaje
tupokewe na mtu mwingine. Hatumhitaji mtu mwingine hapa, aondoke."
Baada
ya kauli hiyo, waziri Nchimbi aliondoka mahala hapo na kuzua shangwe
kubwa kwa waandishi ambao pia walimsindikiza kwa kumzomea mpaka
alipoingia katika gari lake la wizara. Hakuja na gari lake la waziri.
Wahariri
wa vyombo mbalimbali vya habari walizungumza na kukemea mauaji hayo na
bila ya kuuma-uma maneno walisema kwamba Mwangosi aliuawa kwa kulipuliwa
na polisi na kwamba waliohusika wote wachukuliwe hatua za kisheria.
"Waandishi
na wafanyakazi wengine wanalipa kodi ilipolisi wapate magwanda, wapate
bunduki, wapate mabuti na wanalipwa ili walinde raia na sio kuua raia,
vitendo kama hivi havikubaliki," alisema Jesse Kwayu, mhariri mkuu wa
gazeti la NIPASHE.
Mwandishi mkongwe, Masoud Sanani, aliongeza:
"Waarabu wanasema 'wal kiswaswa haq' yaani 'kisasi ni haki', lakini sisi
kwa busara tunasema kwamba hatuna kisasi ila tunataka mambo haya yawe
mwisho, waandishi waachwe wafanye kazi zao kama askari wanavyoachwa
wafanye kazi zao."
Waandishi wakisapoti jambo wakati wa mkutano wao baada ya maandamano ya
kupinga mauaji ya David Mwangosi asubuhi ya leo (picha: Staika Mkali
blog)
Post a Comment