|
Askari wakiwa lindoni/doriani, Mtwara |
Hali ya usalama katika
Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa imezidi kuwa mbaya baada ya
askari polisi kudaiwa kufanya unyama kwa kuwabaka wanawake na kumpiga
risasi mjamzito
Mbali na unyama huo polisi pia wanadaiwa kuchoma
moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na vibanda vya
maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.
Hata hivyo Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa anasema hali ni shwari na
kwamba wananchi watoke nje kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Kaimu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi
amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni,
zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti
zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18: “Ni kweli
kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi
saba, amepigwa risasi tumboni...” “...pia tumepokea mwanafunzi wa shule
ya sekondari ya Chuno, amevunjwa miguu yote kwa risasi.”
Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake.
Huduma
za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyo wazi, hakuna usafiri wa
daladala wala pikipiki, mji upo kimya, sauti za milio ya mabomu na
bunduki zimetawala, wanajeshi waliovalia sare wameuzingira mji wakiwa
katika magari na pikipiki.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari
kwa nyakati tofauti wakazi hao wamelalamikia kitendo cha askari wa jeshi
la polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga, kuwabaka na kuwapora
mali zao:
“Magomeni A hatuna amani askari wanaingia majumbani mwetu wanatupiga
na kutunyang’anya simu, yani huku Magomeni hatuna amani kabisa,
tumepoteza watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi” alisema Paulina
Idd na kuongeza: “Majumba yetu yamechomwa moto wanaofanya fujo ni polisi
wenyewe halafu wanakuja wanatubaka na kuiba mali zetu halafu tunateseka
sisi yaani tumechoka kabisa na serikali yenyewe,” alisema Paulina.
Kamanda Sinzumwa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa atapingana na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Emmanuel Mchimbi aliyewasili Mtwara leo: “Kuhusiana na suala
hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani nitapingana na Waziri wangu
kwani leo ametoa tamko bungeni na leo atawasili,” alieleza Sinzumwa
Wakazi wakimbia maeneo yao
Wakazi
wa maeneo mbalimbali wamekimbia makazi yao hususani wanawake na watoto
na kuhamia hospitali ya rufaa kwa kuhofia usalama wao huku wengi wao
wakipotezana na ndugu zao.
Hali
hiyo imetokea kufuatia kuwepo kwa milipuko ya mobomu katika maeneo
mbalimbali mjini hapa huku huduma za kijamii zikiwa bado
zimesitishwa. Hali hiyo imetokea baada ya kusambazwa kwa vipeperushi
vilivyokuwa vikihamasisha wananchi wa mkoani hapa kusitisha huduma zote
hapo jana ili kusikiliza hotuba ya wizara ya nishati na madini.
Kufuatia
hali hiyo imesababisha kifo kwa raia mmoja aliyefahamika kwa jina Karim
Shaibu (22) mkazi wa Chikongola ambaye alipigwa risasi wakati wa fujo
kati ya jeshi la polisi na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa
habari mganga mkuu wa mkoa hospitali ya rufaa ya Ligula Dk Sadun Kabuma
alithibitisha kupokea kwa kifo hicho ikiwa ni pamoja na majeruhi 17
wakiwemo askari watatu: “Ni kweli jana kuanzia majira ya saa 10 hadi saa
11 nilipokea majeruhi 17 ambapo kati ya hao wamishtuko ni wanawake
watano na askari watatu na kijana mwingine ambaye alikuwa na jeraha na
katika harakati zan kumwokoa maisha yake alifariki akiwa chumba cha
upasuaji,” alisema Dk Kabuma
Wananchi wazungumzia bajeti
Wakizungumzia
uwasilishwaji wa hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini wakazi wa hapa
wamesema kuwa hawakubaliani na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwani
mpango huo utawaletea dhuluma: “Mpango wa kusafirishwa kwa gesi asilia
hatuna mpango nao kwa wakazi wote wa Mtwara kwa kifupi akina mama wa
mtwara hatutaki itoke,” alisema Fatuma Abdallah.
.........................
Imenukuliwa kutoka mtandao wa www.wavuti.com
Post a Comment