Dodoma/Dar. Serikali imechukua uamuzi mgumu na kuamua kuwafariji
wanafunzi waliofeli mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2012
baada ya kufuta matokeo hayo na kuamua yaandaliwe upya kwa kutumia
utaratibu uliotumika mwaka 2011.
Uamuzi huo wa Serikali umetokana na matokeo mabaya
ya mitihani huo yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi
kupata sifuri.
Kutokana na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume
inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza matokeo hayo ili kupata
ufumbuzi wa kudumu.
Muda mfupi baada ya tamko la Serikali, baadhi ya
wadau wa elimu wameeleza kufurahishwa na uamuzi huo, huku Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) kikiikosoa hatua hiyo, kuwa imekiuka sheria na
kupora madaraka ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
Akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu taarifa ya
awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa Taifa Kidato
cha nne mwaka 2012 jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu
na Bunge), William Lukuvi alisema wameagiza Necta kuweka viwango ili
matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.
“Standardization ifanyike ili matokeo ya wanafunzi
yalingane na juhudi wazizoziweka katika kusoma kwa mazingira, hali
halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa kuongeza idadi ya shule na
wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea,” alisema Lukuvi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akiwasilisha kauli ya serikali Bungeni Dodoma jana kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza matokeo ya mtihani wa taifa wa Kidato cha nne wa mwaka 2012. Picha na Edwin Mjwahuzi |
Lukuvi alisema Necta imeelekezwa kuwa licha ya
sheria ya kuanzishwa kwake kuruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa
mtihani, marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango
vya ufaulu na madaraja ya mitihani yanatakiwa yahusishe wadau wote
wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mtihani.
“Wakati Tume inaendelea kukamilisha kazi yake,
uamuzi wa Necta kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na
madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika 2012 usitishwe,” alisema
Lukuvi na kuongeza:
“Badala yake Necta itumie utaratibu uliotumika
mwaka 2011 kwa kidato cha nne na sita kwa mitihani yote, ikiwamo
utaratibu wa Standardization na kutoa matokeo mapya kwa kuzingatia
maelekezo haya.”
Pia, Serikalli imeagiza mchakato wa tuzo wa taifa
(National Qualifications Framework) na Mfumo wa Kutahiniwa/ kuthamini
maendeleo ya mwanafunzi masomo yake (National Assessment Framework)
ukamilishwe haraka iwezekanavyo.
Katika mtihani wa mwaka 2012, wanafunzi 367,756
walifanya mtihani huo na waliofaulu ni 126,847. Waliofaulu kwa kwa
madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na daraja
la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni asilimia
65.5 wakipata daraja sifuri.
Kauli ya CWT
Habari kwa msaada wa Gazetui la kila siku la Mwananchi
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1841582/-/item/3/-/s03mvmz/-/index.html
Kauli ya CWT
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel
Oluoch alisema Baraza la Mawaziri limepora kazi za Bodi ya Baraza la
Mitihani kwani ndio yenye jukumu la kufuta matokeo kisheria.
Mbali na hilo Oluoch alisema bado wanafanya
utafiti ili kuona kama Baraza la Mawaziri lina uwezo wa kufuta matokeo
na kuamuru mitihani isahihishwe upya, badala ya Bodi ya Baraza la
Mitihani.
Oluoch aliyesema tamko rasmi la CWT kuhusu uamuzi
huo wa Serikali litatolewa wiki ijayo, alieleza kuwa kwa sasa
wanachunguza kuona kama jambo hilo lina usahihi kwa kiasi gani.
“Mitihani iliyofutwa ilitolewa na Bodi ya Necta
ambayo ndio itakuwa na jukumu la kusimamia usahihishaji mpya na
kutangaza tena matokeo.
Kama hali yenyewe ndio hiyo ni wazi kuwa haina
tena uwezo wa kusimamia jambo hilo, inatakiwa kung’oka na kuundwa bodi
mpya,” alisema Oluoch na kuongeza;
“Nasema hivyo kwa sababu hawawezi kula matapishi
yao kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya kutoa tena matokeo hayo na
walishasema kuwa yalikuwa mabaya, sasa uzuri wake utatoka wapi tena.”
Alisema kuwa kufutwa kwa matokeo hayo kunaonesha
wazi kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeshindwa kazi ya
kusimamia elimu nchini.
“Pia katika utangazaji wa matokeo anatakiwa waziri
mpya wa kufanya hivyo kwa kuwa huyu wa sasa alieleza sababu za
wanafunzi kufeli, sasa akiwa anatangaza matokeo mapya atatueleza nini,”
alihoji.
Sababu za matokeo mabaya
Waziri Lukuvi alisema takwimu zinaonyesha kushuka
kwa ufaulu huo unahusu shule zote na asilimia kwenye mabano, shule za
wananchi (1.82); Shule za umma yaani kongwe (6.43); Binafsi (6.39) na
Seminari (7.29).
Kuhusu matokeo ya kidato cha nne 2012, Lukuvi
alisema tume imebaini licha ya wanafunzi kuwa kwenye mazingira
yanayofanana na wenzao waliopita, ufanisi umekuwa ukishuka kwa sababu
mbalimbali.
“Ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya
mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani mwaka
2012, mfumo uliotumika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule
uliotumika miaka iliyotangulia,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Uchunguzi unaonyesha kuwa mwaka 2011, Necta lilikuwa
linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika
kutegemea hali ya ufaulu kwa mwanafunzi ambao ni National Mean
Difference (NMD).
Alisema uataribu huo ulitokana na tofauti ya
wastani wa kitaifa wa alama za maendeleo, kutoka alama ya maendeleo
endelevu (Continued Assessment-CA) za watahiniwa wote na wastani wa
kitaifa wa ufaulu wa mtihani wa mwisho kwa somo husika.
Aliendelea kuwa kila mtahiniwa aliongezewa NMD
iliyokokotolewa kwenye alama za mtihani wa mwisho, ili kupata alama
itakayotumika kupada daraja la ufaulu.
“Lakini mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na
viwango maalumu vya kutunuku (Fixed Grade Range). Tume imebaini kwamba
licha ya mfumo huo ulioandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya
hakufanyiwa utafiti wa maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika,”
alisema.
Lukuvi alisema taarifa ya awali ya tume, inaonyesha kutokana na uchunguzi uliofanyika kwa muhtasari imebaini mambo mbalimbali.
Alisema matokeo ya kidato cha nne kuanzia mwaka
2008 yamekuwa na mserereko wa kushuka tofauti na miaka iliyotangulia,
kwa sababu ya changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya
kuongezeka kwa idadi ya shule za msingi na sekondari, hususan mwaka 2011
na 2013 hivyo kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
“Mwaka 1961 hadi 2011 idadi ya wanafunzi kwa shule
za msingi imeongezeka kutoka 486,470 hadi 4,875,764, sawa na ongezeko
la wanafunzi 4,389,294 kwa takriban miaka 40,” alisema.
Alisema wanafunzi wameongezeka kutoka 4,875,764
mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012, sawa na ongezeko la wanafunzi
3,371,708 kwa kipindi cha miaka 11.
Sekondari wanafunzi wameongezeka kutoka 11,832
mwaka 1961 hadi 289,699 mwaka 2001 sawa na ongezeko la wanafunzi 274,867
kwa miaka 40.
Lukuvi alisema kati ya mwaka 2001 hadi 2012
wanafunzi wameongezeka kutoka 289,699 hadi 1,884,270 sawa na ongezeko la
watu 1,594,571.
Tume hiyo imebaini changamoto nyingine ni
mazingira yasiyo ya kuridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ikiwamo
upungufu wa miundombinu muhimu ya shule; madarasa, madawati, maktaba,
nyumba za walimu, bweni na majengo mengine muhimu.
“Kuna tatizo la uhaba wa walimu, vitabu, zana za
kufundishia na matatizo ya ukaguzi wa shule. Vilevile tumebaini Mfumo wa
Elimu ya Msingi na Sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine
mbalimbali ambazo taifa linapitia kwa sasa,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Yapo masuala ya sera, sheria, mfumo, muundo na changamoto za uhaba wa
rasilimali fedha na watu. Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa
kushirikiana na wataalamu na wadau wengine.”
Habari kwa msaada wa Gazetui la kila siku la Mwananchi
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/1841582/-/item/3/-/s03mvmz/-/index.html
Post a Comment