AJIRA KWA VIJANA ZAATHIRIWA
NA UKUAJI MDOGO
WA UCHUMI ULIMWENGUNI
Ripoti mpya ya ILO inayohusu Hali ya Ajira kwa vijana Ulimwenguni – 2013 imeeleza kuwa athari
hizi za muda mrefu za tatizo kubwa la ajira kwa vijana zitaendelea kuwapo kwa
miongo mingi na hivyo kukiweka kizazi hiki kwenye hatari kubwa ya kutokuwa
kwenye kazi zenye staha kwa kipindi chote cha maisha yao.
Pamoja na tofauti zilizopo katika mabara mbalimbali,
kiwango cha ajira kwa vijana ulimwenguni kinaendelea kukua na kinategemewa
kufikia asilimia 12.8 ifikapo mwaka 2018 – hivyo kuondoa mafanikio yote
yaliyopatikana kutokana na kupambana na mproromoko wa uchumi duniani.
Linaloogopesha zaidi ni swala la ukosefu wa ajira
kuendelea kuwepo, kuwepo kwa ajira za muda mfupi na kukatishwa tamaa kwa vijana
hasa katika nchi zilizoendelea, na pia ajira za kiwango cha chini na zisizo
rasmi hasa kwa nchi zinazoendelea.
Kutokana na ripori hii, inakadiriwa kuwa vijana wapatao
milioni 73.4 (asilimia 12.6) hawatakuwa na ajira mwaka huu ukilinganisha na asilimia
12.4 mwaka 2012, kiwango karibu sawa na kile cha mwaka 2009 tulipokuwa kwenye
kilele cha mporomoko wa uchumi duniani.
Hili ni ongezeko la vijana milioni 3.5 kati ya mwaka 2007 na 2013.
“Viwango hivi vinatuhimiza kulenga sera zetu kwenye
kukuza uchumi zaidi, kuboresha mifumo ya elimu na mafunzo, na kuwa na shughuli
zinazotoa kipaumbele kwenye kukuza ajira za vijana” kama ilivyosemwa na Jose
Manuel Salazar-Xirinachs, Mkurugenzi Msaidizi wa ILO, kuhusu Sera. Pia ameongeza kuwa “ Makundi haya, Waajiri,
wale wanaotoa elimu na vijana mara nyingi hawashirikiani katika jambo hili;
kufanya kazi kwa pamoja kwa wadau hawa na kushirikiana kwa karibu ndio
kutakakoleta mafanikio”.
Hali katika mabara ulimwenguni
Kiwango kikubwa zaidi cha kukosekana kwa ajira
kimekuwepo kwenye eneo la Mashariki ya Kati (Middle East), yaani asilimia 28.3,
ikiwa ni zaidi ya robo ya idadi ya vijana wanaostahili kuajiriwa. Kiwango hiki kinategemewa kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2018. Afrika ya Kaskazini pia ina kiwango kikubwa
kinachofikia asilimia 23.7
Vijana wa kike ndio waathirika wakubwa katika maeneo
haya – asilimia 42.6 kwa mashariki ya kati na asilimia 37 kwa Afrika ya
Kaskazini.
Waliokuwa na kiwango cha chini cha kukosekana kwa ajira
mwaka 2012 ni Asia ya Mashariki (asilimia 9.5) na Asia ya kusini (asilimia
9.3).
Matarajio ya baadaye
Kwa nchi zilizoendelea, kiwango cha kukosekana kwa ajira
kwa vijana kwa mwaka 2012 kilikuwa asilimia 18.1 na kinategemewa kuendelea kubaki
kuwa zaidi ya asilimia 17 hadi kufikia mwaka 2015/16. Kwa nchi za Greece na Spain zaidi ya asilimia
50 ya vijana hawana ajira.
Vijana wengi wamekatishwa tamaa na swala la kutafuta
ajira. Kwa mfano katika nchi zilizoendelea
kwa ujumla vijana waliokata tamaa na wale wasio na ajira walifikia idadi ya
milioni 13 kwa mwaka 2012.
Kupungua kwa fursa
Vijana wengi wanalazimika kutochagua kazi – hufanya kazi
za muda maalum au zile za masaa ili kujipatia kipato. Bwana Salazar anaeleza kuwa, “Ajira za kudumu
na za uhakika lilikuwa jambo la kawaida kwa vizazi vilivyopita na hali hiyo
imebadilika kwa vijana wa sasa. Kutokana
na kuongezeka kwa ajira za muda maalum na zile za masaa tangu mgogoro wa uchumi
ulipotokea, inaonyesha kuwa hiyo ndiyo aina ya ajira pekee iliyopo kwa
wafanyakazi vijana”.
Taarifa hii inaonyesha pia kuwa kuwepo kwa tatizo hili
la ajira kwa muda mrefu kunaleta athari nyingi zikiwemo – kupungua kwa uzoefu
wao kwenye kazi na kupotea kwa ujuzi walio nao katika nyanja mbalimbali; Pia tatizo hili huwafanya vijana kuendelea
kukata tamaa ya kupata ajira na/au kipato kwa muda mrefu.
Kuoanisha ujuzi na aina ya ajira
Kutooanisha ujuzi na aina ya ajira pia kunaongezeka. Hali hii ni ya hatari hasa kama hapatakuwepo
na sera za kuwanedeleza kiujuzi vijana wanaotaka kuajiriwa. Waathirika zaidi katika hali hii ni pamoja na
wasichana na wale ambao wapo tayari kwenye
tatizo la kutoajiriwa.
Athari hizi zitaendelea kuongezeka endapo tatizo la
ajira kwa vijana litaendelea kuwepo, na litaongeza gharama kiuchumi na kijamii
– yaani kuongezeka kwa umaskini na ukuaji finyu wa uchumi.
Hatua zenye malengo zinahitajika
Ripoti hii inazitaka serikali za nchi mbalimbali
kuchukua hatua za haraka kupambana na tatizo hili sugu la ukosefu wa ajira kwa
vijana. Juhudi za pekee pia kutoka kwa
vyama vya waajiri na wafanyakazi zinahitajika.
Inasisitiza pia kuwa ni vyema kila nchi ikazingatia maeneo ya sera
yaliyopendekezwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwezi Juni 2012. Hatua zifuatazo zilipendekezwa na taarifa
hii:
-
Kulenga kwenye ukuaji wa
uchumi unaokuza ajira na kazi zenye staha kupitia sera mbalimbali, sera za soko
la ajira, ujasiriamali kwa vijana na haki yao ya kupambana na tatizo la ajira
na athari zake, na pia kuhakikisha uwepo wa uwezo kifedha.
-
Hatua za makusudi
zichukuliwe zikilenga vijana wenye ulemavu na wasiojiweza hasa kwa nchi zile
zenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kwa vijana. Hatua hizo zijumuishe elimu, mafunzo,
kuhimiza mashirika kutoa ajira na kuwasaidia vijana kupata uzoefu katika kazi.
-
Kuandaa mikakati na mipango
ya kuwapatia vijana ajira na kipato has katika nchi zinazoendelea ikiwa ni
pamoja na kutoa mafunzo, kuwapatia ujuzi katika kazi na mbinu za ujasiriamali
na uendeshaji wa biashara.
Kwa maelezo
zaidi wasiliana nasi: ILO Office Dar es
Salaam, P. O. Box 9212, Tel: 2196700, Fax: 2126627, Email: daressalaam@ilo.org au ILO
Department of Communication, Geneva, at: +4122/799-7912, communication@ilo.org,
Post a Comment