Baadhi ya magari ya mizigo yakiwa yameegeshwa katika moja ya vituo vilivyopo kandokando ya Barabara Dar es Salaam- Morogoro yakisubiri kuendelea na safari 


Licha ya kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Ukimwi, Mkoa wa Mbeya bado unatajwa kuwa eneo lililokithiri kwa vitendo vya ngono bila kuwa na tahadhari (ngono zembe).
Dar es Salaam. 

Sababu kubwa ya hali hiyo inaelezwa kuwa ni kuwepo kwa maegesho ya malori ya mizigo yanayoelekea Zambia huku madereva wake wakitajwa kuwa wateja wakubwa wa ngono.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumamosi katika maeneo yanayotajwa kwa biashara ya ngono yaani Kata ya Igawa na Igurusi, umethibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo.
  
Igawa
Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa madereva wa taxi eneo la Igawa aliyejitambulisha kwa jina la Felix, alisema kuwa kwa sasa biashara hiyo imedorora kwa sababu madereva wa malori wamepunguza kusimama hapo.  
“Zamani ungefika hapa saa hizi ungewakuta barabarani kabisa. Lakini siku hizi, malori yameacha kusimama hapa, ndiyo maana nao wamepungua. Lakini wapo baadhi yao ni wahudumu wa baa,” alisema dereva huyo.
Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda na usafiri usiku ni wa shida, mwandishi aliendelea Kata ya Igurusi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Igurusi
Ni majira ya saa mbili usiku, baada ya kuchukua chumba kwenye nyumba ya wageni iliyo mbali na barabara kuu, nikarudi kwenye baa moja. Kabla sijaondoka, nikamuuliza mama mwenye gesti kama naweza kuleta mwanamke wa kulala naye. Akanijibu kuwa ni uamuzi wangu kwani haizuiwi.
Nilipofika katika baa moja iliyo pembeni mwa barabara (jina linahifadhiwa) nilikuwa nikipata kinywaji huku nikiangalia jinsi ya kumpata mtu wa kuzungumza naye kwa kina.
Namjaribu mhudumu mmoja wa baa hiyo kwa kumtongoza, lakini akasema hawezi kutoka na mimi kwa kuwa bado yuko kazini.
Nahamia baa nyingine ng’ambo ya barabara kwa lengo hilohilo. Hapo nakutana na mama mmoja wa makamo, kisha kumweleza shida yangu kwamba natafuta mwanamke wa kulala naye usiku huo.
“Ni kweli hapa wapo kina dada, ukiwataka mnaelewana tu. Mimi mwenyewe ninaye binti yangu ila nimetuma dukani, labda umsubiri. Lakini kama unaona utachelewa, basi nenda baa ya jirani hapo wapo wengi tu,” alisema mama huyo.
Nikaamua kwenda kwenye baa hiyo jirani na hapo nawakuta kina dada wapatao watano, huku wateja wakiwa wachache tu. Nikaagiza soda na kuanza kuinywa taratibu. Bila kupoteza muda nikamuuliza dada aliyeniletea soda (jina linahifadhiwa)  kama naweza kupata mshichana wa kulala naye usiku huo. Mahojiano yetu yakawa hivi
Mhudumu: Hapa wapo wengi tu… wote unaowaona hapa ndiyo kazi zao, sijui unamtaka nani?

Mwandishi: Mimi nakutaka wewe..


Mhudumu: Mh! Sawa lakini ujue bado niko kazini hadi saa tano usiku. Labda unipe Sh5,000 nikalipe kwa meneja ili aniruhusu.

Mwandishi: Hiyo haina shida, kuna gharama nyingine?
Mhudumu: Ndiyo itabidi pia unilipe hela ya penzi, Sh10,000 na Sh5,000 ya kulipia gesti.

Mwandishi: Mh! Mbona kubwa hivyo? Kwani ni lazima tufanyie kwenye gesti ya hapa?

Mhudumu: Hiyo ndiyo bei yetu ya kawaida. Siyo lazima tulale hapa, kama kuna sehemu nyingine twende tu.
Nampa Sh5,000 ya kulipa kwa meneja wake, huku nikimalizia soda yangu. Mara akawa tayari, tukaondoka kuelekea gesti niliyofikia.
Katika gesti hiyo pia kuna baa na sehemu ya chips. Mazungumzo yetu yakaendelea.


Mhudumu: Kwanza uninunulie chips na samaki maana nina njaa sana. Halafu uninunulie na bia.
Mwandishi: Usihofu utakula tu. Lakini bia mimi situmii kwa hiyo itabidi unisamehe kwa leo. Enhee, hebu nijulishe jina lako na kwa nini umeipenda hii kazi ya baa?

Mhudumu: Mimi naitwa…(jina linahifadhiwa), sina muda mrefu sana hapa Igurusi. Nimekuja kutoka Mbeya mjini kwa mama yangu mzazi. Nilimtoroka mama baada ya rafiki yangu kunirubuni.
Mwandishi; Umefikika kidato cha nne?
Mhudumu: Shule sikumaliza mwaka … aah, nilimaliza mwaka juzi, lakini sikufanya vizuri.
Mwandishi: Ulipata divisheni gani?

Mhudumu: Usinikumbushe machungu… nilipata ‘C’ moja tu, nilikuwa shule ya Southern Highland ya Mbeya. Kilichosababisha nishindwe kuendelea na masomo ni kupata mimba na kuzaa mtoto ambaye sasa ana miaka miwili na yuko kwa mama.
Mwandishi: Kumbe una mpenzi, anajua kwamba uko hapa?
Mhudumu: Wala hajui, kwanza tulikorofishana, japo hatujaachana na anamhudumia mtoto wake vizuri tu.
Baada ya chips kuwa tayari nikamwomba tuingie chumbani. Mazungumzo yakaendelea.
Mwandishi: Sasa tule halafu kazi ianze

Mhudumu: Sawa.
Mwandishi: Hivi tukifanya bila kondomu utanifanyia shilingi ngapi?

Mhudumu: Mh! Mimi naogopa kufanya bila kondomu. Si unipe hela tu nikanunue kondomu hapo nje?
Mwandishi: Kwani nikitafuta mwanamke huko nje wa kufanya naye bila kondomu sipati?

Mhudumu: Wapo wengi tu, hata pale baa uliyoniyonitoa, wanawake wanajiuza na wengine wanaletwa pale ni wake za watu wanakuja wakiwa wamejifunika khanga. Kwa ujumla hapa ngono inafanyika mno.
Baada ya mazungumzo kuendelea nikamwambia, basi kama hataki bila kondomu basi na mimi sitaki kufanya. Nikamlipa Sh5,000 kwa kuwa hatujafanya na kumrudisha nilipomtoa ikiwa ni saa tano usiku.
Utafiti wa NIMR
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Binadamu (NIMR) mwaka 2012, kuhusu upatikanaji na matumizi ya kondomu kwenye maeneo yenye maambukizi makubwa ya Ukimwi hasa katika Barabara ya Tanzania na Zambia wilayani Mbarali, umeonyesha kuwapo kondomu kwa asilimia 52 tu.
Akizungumzia utafiti huo, Mtafiti wa Nimr Emmanuel Makundi alisema kuwa Wilaya ya Mbarali ilichaguliwa hasa katika maeneo ya Igawa, Chimala na Igurusi ikiwa ni njia za kuelekea mipaka ya Zambia na Malawi, ambazo zimekithiri kwa vitendo vya ngono.
“Utafiti wetu umebainisha matumizi hafifu ya kondomu katika maeneo yaliyoathirika zaidi na Ukimwi ya kuelekea mpaka wa Zambia,” alisema Makundi.
Madereva wa malori
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Madereva wa Malori nchini (Chamamata-CMMT), Rocket Matogolo amekiri tabia ya madereva wa malori kujihusisha na vitendo vya ngono wawapo safarini, lakini akasema kuwa hawashirikishwi katika mapambano hayo:
“Tunalifahamu hilo na tunapigana nalo kwa sababu ni janga linalovunja nguvu kazi ya Watanzania. Tulichotarajia kutoka Serikalini na wadau wengine ni kutushirikisha kama ilivyo kwenye polisi jamii kuliko kulihamishia kwenye sekta nyingine wakati wahusika ni sisi.”
Tacaids
Akizungumzia suala hilo, Mratibu wa miradi maalumu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini, Renatus Kihongo anakiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa tume hiyo imeshaainisha barabara za masafa marefu na kuziwekea vituo vya huduma za Ukimwi.
“Kuna barabara za Dar es Salaam- Tunduma, Dar es Salaam, Kahama, Ngara kwenda Burundi na Rwanda, kuna Dar es Salaam, Arusha kwenda Kenya na ule mpaka wa Horohoro Tanga. Kote huko kuna maeneo ambayo malori huegeshwa na kuna biashara nyingi ikiwemo ya ngono,” anasema Kihongo.
Anaongeza kuwa Tacaids imefanya tafiti kubaini tatizo hilo ikishirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi ya Kenya (NACC) na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM).
Anasema kuwa katika utafiti huo wamepata taarifa za moja kwa moja za tabia za watu, idadi yao na kiwango cha huduma wanachotakiwa kupata.
Anataja pia mkakati unaooanisha shughuli za Ukimwi kwa nchi za Afrika Mashariki, ambapo huduma zake zinatarajiwa kutolewa katika vituo vya huduma ya pamoja vya mipakani (One stop border post).


Habari hii kama ilivyoandikwa na gazeti la siku la Mwananchi


















































































Labels:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.